Mar 25, 2019 00:18 UTC
  • Malalamiko ya China kwa hatua ya Marekani ya kuiuzia silaha Taiwan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema kuwa, Beijing imewasilisha hati ya malalamiko kwa Marekani kufuatia hatua ya nchi hiyo kutangaza kwamba itakiuzia silaha kisiwa cha Taiwan.

Geng Shuang, ameyasema hayo akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kwamba, China inaitaka Marekani isimamishe uuzaji wowote ule wa silaha na mahusiano yake ya kijeshi na Taiwan. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amebainisha kuwa, Beijing inapinga vikali uuzaji wa shehena za silaha wa Washington kwa kisiwa hicho na akaongeza kwamba, China itakabiliana na mwenendo huo. Aidha ameonya kuwa hatua za Marekani za kuiunga mkono kijeshi Taiwan zitasababisha hatari kama ambavyo kwa kufanya hivyo inakiuka pia msingi wa China moja iliyoungana. Hii ni katika hali ambayo awali viongozi wa Taiwan walikuwa wameitaka Marekani iliuzie eneo hilo zaidi ya ndege 60 za kivita aina ya F16, suala ambalo liliungwa mkono pia na Washington, licha ya serikali ya China kutangaza wazi kwamba inapinga vikali mauziano yoyote ya silaha au ushirikiano wa kijeshi wa kigeni na eneo hilo. 

Geng Shuang, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China

Mpango wa Marekani wa kuiuzia silaha Taiwan ni moja ya mambo ambayo yameibua mivutano na changamoto kali kati ya Marekani na China katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Hata kama serikali ya zamani ya Marekani ilizipa umuhimu wa kiasi fulani siasa zake kulihusu eneo la Taiwan hasa kutokana na mikwaruzano iliyokuwepo kati yake na serikali ya Beijing, lakini serikali ya sasa ya Trump imefuata mkondo mpya katika suala hilo kutokana na kuzidisha kiwango cha hujuma katika siasa zake za kigeni. Hasa kwa kuzingatia kuwa katika fremu ya stratijia zake Trump anakusudia kuongeza pato kubwa katika mradi wa usalama ikijumuisha mauzo ya silaha na kupata kiwango kikubwa cha fedha kutoka kwa nchi za kigeni, bila kuzingatia athari mbaya ya stratijia hiyo katika mfumo wake wa kijeshi katika eneo na kimataifa. Hata hivyo isisahulike kwamba, mbali na rais huyo wa Marekani kuyaongezea soko la mauzo kimataifa mashirika yanayotengeza silaha nchini Marekani kwa kuiuzia silaha na zana za kivita Taiwan, anakusudia pia kuizidishia mashinikizo ya kisiasa na kibiashara serikali ya China ambayo ni mshindani wake mkubwa katika uwanja huo.

Mgogoro wa kibiashara unaoendelea kati ya China na Marekani

Kwa kuzingatia kwamba tangu mwanzo wa mwaka jana 2018, Marekani ilianzisha vita vya kibiashara dhidi ya China na hadi sasa tayari kumefanyika duru kadhaa za mazungumzo bila kufikiwa natija kati ya nchi mbili kwa ajili ya kuhitimisha vita hivyo, hivyo inakisiwa kwamba White House inakusudia kutumia mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Beijing kwa masuala nyeti na hasasi kwa nchi hiyo likiwemo suala la Taiwan na bahari ya China ya Kusini mwa nchi hiyo, ili kuilazimisha Beijing ikubaliane na mipango mipya ya kibiashara ya Washington. Aidha Washington inaitaka China ipunguze idadi ya raia wake wanaofanya kazi katika mashirika ya China yanayoendesha shughuli zake nchini Marekani na badala yake nafasi hizo zichukuliwe na Wamarekani sambamba na kuondolewa mipaka mashirika ya Marekani katika soko la China. Kwa kuzingatia kuwa suala la Taiwan ni mstari mwekundu kwa China, si baidi kwamba Beijing itakubaliana na matakwa hayo ya Marekani mkabala wa kusimamishwa mauzo ya silaha kwa eneo hilo linalotaka kujitenga na China.

 

Maoni