Mar 25, 2019 07:50 UTC
  • Ndege za Russia zilizobeba shehena ya misaada zatua Venezuela zikiwa na maafisa wa kijeshi

Ndege mbili za Russia zilizobeba tani elfu 35 za misaada zimetua mjini Caracas, mji mkuu wa Venezuela.

Mbali na misaada hiyo, ndege hizo zimewashusha pia karibu askari 100 wa Russia. Vyombo vya habari nchini Venezuela vimeripoti kwamba askari hao walipokelewa na viongozi wa ngazi ya juu wa kijeshi wa Venezuela pamoja na viongozi wa ubalozi wa Russia nchini humo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Simón Bolívar. Aidha vyombo hivyo vya habari havikuashiria lengo kuu la ujumbe huo wa kijeshi wa Russia au kilichomo kwenye shehena ya misaada hiyo. Kutangazwa habari ya kutumwa ndege hizo za misaada kutoka Russia, kumejiri baada ya Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani aliyejitangaza kuwa rais wa Venezuela kudai kwamba, Rais Nicolás Maduro wa nchi hiyo amekosa uungaji mkono wa ndani na kimataifa.

Rais Vladmir Putin wa Russia, kulia akiwa na Rais Maduro wa Venezuela wakionyesha urafiki wao

Katika wiki za hivi karibuni Marekani sambamba na kutangaza uungaji mkono kwa Guaidó, imefanya pia njama za kutekeleza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Maduro aliyechaguliwa na wananchi. Kabla ya hapo pia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza utayarifu wake wa kutuma misaada ya dawa na vifaa vya tiba nchini Venezuela. Juan Guaidó alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela hapo tarehe 23 Januari mwaka huu kupitia uungaji mkono kamili wa Marekani na washirika wa Washington. Hata hivyo licha ya njama hizo za kutaka kumuondoa madarakani Rais Maduro, jeshi na wananchi pamoja na nchi kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, China na mataifa kadhaa ya dunia yameendelea kusisitizia ulazima wa kuheshimiwa haki ya kujitawala nchi hiyo ya Amerika ya Latini. 

Tags

Maoni