Mar 25, 2019 07:56 UTC
  • Raia wa New Zealand wataka waziri mkuu wao apewe zawadi ya Nobel kwa namna alivyoamiliana vyema na Waislamu

Idadi kubwa ya raia wa New Zealand wametaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Jacinda Ardern atunukiwe tuzo ya amani ya Nobel kutokana na namna alivyoamiliana kwa njia bora na Waislamu baada ya shambulizi la kigaidi la hivi karibuni ndanii ya misikiti.

Kwa mujibu wa raia hao, miamala ya kuvutia iliyofanywa na waziri mkuu huyo baada ya hujuma hiyo ya kinyama dhidi ya Waislamu, ilikuwa ya kuigwa kutokana na upendo aliouonyesha kwa jamii ya Waislamu wa New Zealand. Hii ni kwa kuwa siku moja baada ya shambulio la kigaidi la tarehe 15 mwezi huu katika misikiti miwili ya mji wa Christchurch, sambamba na kufika eneo la tukio akiwa amevaa mtandio kichwani na kukutana pia na wawakilishi wa Kiislamu na kutoa pole kwa kuwakumbatia wanawake Waislamu kutokana na hujuma hiyo, alilaani vikali jinai hiyo ya kigaidi. Aidha alisema kuwa, mateso wanayoyapata majeruhi wa hujuma hiyo ya kigaidi ni mateso ya taifa zima la New Zealand. Aidha Bi, Jacinda Ardern aliwataka raia wote wa nchi hiyo pamoja na dunia nzima kuwaunga mkono wahanga wa shambulizi hilo la kinyama.

Maelfu ya raia wa New Zealand akiweka mashada ya maua kwa ajili ya Waislamu waliouawa misikitini

Katika fremu hiyo Ijumaa iliyopita, kulifanyika marasimu ya kuwaenzi wahanga wa hujuma hiyo katika uwanja wa mapumziko ulioko kando na msikiti wa al-Noor katika mji wa Christchurch ambapo maelfu ya raia wa New Zealand walifika eneo hilo wakiwa na mabango au vipeperushi vyenye kutoa alama ya upendo wao kwa jamii ya Waislamu wa nchi hiyo. Mbali na hayo mwanzoni mwa wiki jana, bunge la nchi hiyo lilifunguliwa kwa kisomo cha Qur'an Tukufu kama ishara ya kuonyesha mshikamano na Waislamu huku Ijumaa iliyopita kukiadhiniwa adhana katika misikiti yote ya nchi hiyo ambapo Waziri Mkuu aliwataka wananchi kunyamanza kimya kwa dakika mbili wakati wa kusomwa adhana hiyo. Miamala hiyo ya kuvutia ndio imewafanya idadi kubwa ya raia wa New Zealand kutaka Jacinda Ardern apewe zawadi ya Nobel.

Maoni