Mar 26, 2019 03:05 UTC
  • Sisitizo la Rais Maduro kuwa Marekani inahusika na ugaidi na uharibifu nchini Venezuela

Rais Donald Trump wa Marekani katika chote cha utawala wake amekuwa akifuatilia sera za kuiangusha serikali halali ya Rais Nicolas Maduro nchini Venezuela kutokana na kuwa rais huyo anafuata sera za mrengo wa kushoto za kupinga ubeberu na ubepari wa Marekani na Wamagharibi.

Hivi sasa Marekani inatumia mbinu za kiuchumi kwa lengo la kuiangusha  serikali ya Venezuela na sambamba na hilo imetishia kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya serikali hiyo yenye mitazamo huru.

Marekani imeshadidisha uhasama wake sambamba na kutekeleza vitendo haribifu na vya kigaidi dhidi ya Venezuela jambo ambalo limepelekea Rais Maduro atoe matamshi makali. Katika hotuba yake ya hivi karibuni Maduro amesema kuwa, baada ya Marekani kuzuia mamilioni ya dola ya fedha za Venezuela katika benki za kimataifa sasa imepora fedha hizo na inazitumia kufadhili hujuma za kigaidi na hujuma haribifu dhidi ya Venezuela.

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake katika Ikulu ya Rais mjini Caracas, Maduro alisema: "Mamilioni ya dola zitokanazo na pato la uuzaji mafuta ya petroli ya Venezuela, ambazo Marekani imezizuia kwa kisingizio cha vikwazo na visingizio vingine, sasa zinatumika katika kutekekeza mipango ya kigaidi dhidi ya nchi yetu."

Maduro ameongeza kuwa Marekani inataka kumuweka kibaraka wake madarakani kama rais wa Venezuela na kwa msingi huo Juan Guiaido, kinara wa wapinzani nchini humo sasa anatumikia Marekani ili ifikie lengo lake hilo la kibeberu.

Rais Trump wa Marekani (kushoto) na kinara wa upinzani Venezuela, Juan Guaido

Wiki iliyopita, Guaido alitangaza kuwa ameingia katika duru mpya ya mpango wake wa kuiangusha serikali ya Nicolas Maduro, rais halali wa Venezuela. Aidha siku ya Jumapili alidai kuwa eti serikali ya Maduro inakaribia kuanguka.

Ikumbukwe kuwa mnamo Januari 23, Guaido alijitangaza kuwa rais wa Venezuela na punde baada ya hapo Marekani na baadhi ya madola ya Magharibi yalitangaza kumtambua. Wananchi wa Venezuela na wanajeshi wa nchi hiyo wamepinga hatua hiyo na kutangaza kumuunga mkono kikamilifu Maduro. Aidha nchi nyingi na muhimu duniani kama vile Russia, China, Afrika Kusini, Iran na Uturuki zimepinga vikali hatua hiyo ya Guaido na kuitaja kuwa ni sawa na kuipindua serikali halali ya nchi hiyo iliuyochaguliwa katika uchaguzi huru.

Rais Nicholas Maduro wa Venezuela ametaja njama hizo za madola ya Magharirbi dhidi yake kuwa ni sawa na mapinduzi dhidi yake.

Kwa kutegemea 'Kanuni ya Monroe' Marekani imekuwa ikilitazama eneo la Amerika ya Latini kuwa eneo ambalo ina haki ya kueneza satwa yake na kuingilia mambo ya ndani ya eneo hilo na hivyo ni kwa msingi wa nadharia hiyo ya kibeberu ndio Venezuela inalengwa.

Pamoja na hayo, sera hiyo ya kibeberu ya Marekani inapingwa vikali duninia. Kati ya nchi ambazo zimebainisha upinzani wao kwa sera hiyo ya Marekani ni Russia. Wakuu wa Russia wanasema Marekani inataka kuiangusha haraka iwezekanavyo serikali ya Venezuela ili ianze kuchukua hatua dhidi ya nchi zingine za mrengo wa kushoto Amerika ya Latini hasa Nicaragua.

Ingawa Marekani inadai kuwa hatua zake Venezuela ni kwa maslahi ya watu wa nchi hiyo lakini ukweli wa mambo ni kuwa, kuna malengo maalumu ambayo watawala wa Marekani wanafuatilia nyuma ya pazia.

Kwa matazamo wa Maduro, Marekani na madola mengine ya Magharibi yanalenga kupora utajiri mkubwa wa nchi hiyo hasa mafuta ya petroli. Ikumbukwe kuwa Venezuela ni kati ya nchi zenye hifadhi kubwa zaidi ya mafuta ghafi ya petroli duniani.

Wakuu wa Russia wameafikiana na Maduro katika mtaamo wake huo ambapo Nikolai Patrushev, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa Russia anaamini kuwa, njama za Marekani dhidi ya Venezuela zinatekelezwa kwa lengo la kudhibiti na kupora utajiri wa mafuta wa nchi hiyo.

Katika mahojiano Patrushev alisema: "Hatua za Marekani dhidi ya Venezuela ni mpango malaumu wa kisiasa wenye lengo la kufikia maslahi ya kiuchumi ya Washington."

Kwa mtazamo wa Russia, lengo la kistratijia la Markeani katika kuishinikiza Venezuela ni kupora mafuta ghafi ya nchi hiyo ili katika miaka ijayo iwezo kujidhaminia nishati hiyo muhimu ya nishati kwa masharti ambayo yenyewe itaweka ambayo bila shaka yatakuwa ni kwa hasara ya Venezuela.

Wakuu wa Russia wanasema serikali ya Trump inataka kumtumia kinara wa upinzani Venezuela, Juan Guaido kufikia mlengo yake nchini humo.

Patrushev anasema: "Marekani inamhitajia Juan Guaido kama kikaragosi na kibaraka wa kuiwezesha kufikia malengo yake nchini Venezuela."

 

 

Tags

Maoni