Mar 26, 2019 10:43 UTC
  • Msuguano wa kisiasa nchini Uturuki, Kılıçdaroğlu ajibu vitisho vya Erdogan

Mkuu cha chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki cha CHP amesema kuwa haogopeshwi na vitisho vilivyotolewa na Rais Recep Tayyip Erdogan wa nchi hiyo.

Kemal Kılıçdaroğlu alitamka hayo juzi Jumapili mbele ya wafuasi wake na kusema kuwa, Rais Recep Tayyip Erdogan anamtuhumu kuwa anashirikiana na magaidi wakiwemo wa PKK na kutishia kuwa atamtia mbaroni. Hata hivyo amesema, haogopeshwi na vitisho hivyo na ataendelea kuikosoa serikali hata kama inamtuhumu kuwa anashirikiana na magaidi.

Ameongeza kuwa hivi sasa watu milioni 8 wamepoteza ajira nchini Uturuki kutokana na siasa mbovu za kiuchumi za chama tawala wa Uadilifu na Ustawi, suala ambalo amesema, limewafanya wananchi wa Uturuki wawe na mtazamo mbaya kuhusiana na serikali iliyoko madarakani. Inavyoonekana ni kwamba Kemal Kılıçdaroğlu naye yumo katika orodha nyeusi ya Erdogan kama walivyo wapinzani wengine wa chama tawala cha Uadilifu na Ustawi. Rais wa Uturuki anaonekana kutumia tuhuma za kuunga mkono ugaidi na kushiriki katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi kama silaha ya kuwamaliza wapinzani wake. Fimbo nyingine inayotumiwa na chama tawala nchini Uturuki, ni kuwatuhumu wapinzani kuwa ni wafuasi wa Fethullah Gülen ambaye anatuhumiwa na chama hicho kuwa ndiye aliyepanga jaribio la mapinduzi ya kijeshi huko Uturuki. Mara kwa mara Rais wa Uturuki amekuwa akiitaka Marekani imkabidhi Gülen na wafuasi wake kwa serikali ya Ankara, matakwa ambayo hadi hivi sasa yamekataliwa na Marekani.

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki

 

Watu wengi wamesukumwa jela nchini Uturuki kwa tuhuma hizo. Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, watu wanaolengwa zaidi na serikali y Uturuki ni wale wanaoonekana ni tishio cha chama cha Rais Edrogan. 

Kwa upande mwingine inaonekana kuwa siasa hizo za kuwalenga wapinzani na kuwaweka kizuizini zilikisaidia chama tawala kupata ushindi katika chaguzi zilizopita na kupelekea Erdogan na chama chake cha Uadilifu na Ustawi kujiimarisha zaidi madarakani.

Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanatoa tahadhari wakisema kuwa, Erdogan anapaswa kutilia maanani kwamba, kutumia siasa hizo kwa muda mrefu kunaweza kumuharibia katika siku za usoni, bali hata kuwa na matokeo mabaya dhidi yake. Wasiwasi na hofu ya kuogopa kufuatiliwa au kuingizwa kwenye orodha hiyo nyeusi kunaweza kuwachochea wapinzani kuanzisha miungano madhubuti ya kukabiliana na Erdogan na chama chake, bali hata kuongeza uwezekano wa kutokea jaribio jingine la mapinduzi.

Fethullah Gülen

 

Wachambuzi hao wa mambo wanapendekeza kwamba chama tawala cha Uadilifu na Ustawi chini ya uongozi wa Rais Recep Tayyip Erdogan, kinapaswa kufanya juhudi za kuboresha hali ya wananchi hasa katika upande wa kiuchumi na katika upande mwingine kitumie njia za kimantiki na zisizo za mabavu kuwamaliza kisiasa wapinzani wake, ili wasiwe na hoja ya kumkwamisha Erdogan na chama chake. 

Vile vile ni jambo la dharura kukabiliana na wahalifu kwa nguvu zote, sawa kabisa na kukabiliana na kila anayejihusisha na vitendo vya kigaidi au watu wenye nia ya kutoa pigo kwa taifa la Uturuki. Lakini njia bora zaidi ya kufanya hivyo ni kutumia taasisi za mahakama na za usalama na kutojiingiza moja kwa moja chama tawala katika masuala hayo, ili imani ya wananchi kwa serikali iliyoko madarakani isiwe mbaya. 

Maoni