Apr 23, 2019 14:15 UTC
  • Jeshi la Marekani linawaruhusu wanachama wa Daesh waingie Afghanistan

Ripoti mpya imefichua kuwa, jeshi la Marekani limekuwa likiwaruhusu wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) pamoja na silaha zao kuingia nchini Afghanistan.

Ripoti hiyo iliyochapishwa na gazeti la Economic Times imebainisha kuwa, katika hali ambayo anga ya Afghanistan ipo chini ya udhibiti wa Marekani na vikosi vya Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO ambavyo viko nchini humo, lakini duru za kuaminika zimeliambia gazeti hilo kuwa, kuna  shehena za silaha zimekuwa zikiingizwa nchini humo kwa kutumia helikopta ambazo hazina nembo wala nambari za usajili.

Ripoti hiyo ya gazeti la Economic Times imeeleza kuwa, kwa sasa kuna wanachama zaidi ya 10,000 wa Daesh nchini Afghanistan, na idadi hiyo inaendelea kuongezeka kila uchao.

Hivi karibuni, Msaidizi na Mshauri Mwandamizi wa Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran alisema: Jamhuri ya Kiislamu ina taarifa za uhakika kuhusu hatua inazochukua Marekani za kuwahamishia magaidi wa kundi la ukufurishaji la DAESH (ISIS) nchini Afghanistan kutoka Syria na Iraq.

Daesh wakipanga mikakati ya ukatili wao

Kutokana na njama ya Wamarekani, Wazayuni na baadhi ya nchi za Kiarabu, magaidi zaidi ya laki moja wa kundi la kitakfiri la Daesh walizishambulia na kuzivamia kijeshi Syria na Iraq.

Hata hivyo Iran iliweza kuzima njama za maadui hao kwa hatua ilizochukua baada ya kuombwa msaada na nchi hizo mbili.

Tags

Maoni