Apr 24, 2019 03:39 UTC
  • Mtaalamu wa uchumi wa Uingereza: Vikwazo vya Marekani kwa mafuta ya Iran ni fursa kwa Tehran

Mtaalamu mmoja wa masuala ya mafuta na uchumi wa Uingereza amesema kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya mafuta ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni fursa kwa ajili ya Iran.

Chris Cook ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la IRNA na kuongeza kuwa uamuzi wa Marekani dhidi ya Iran, unaifanya Tehran kustafidi na machaguo mawili ya ima kufanya ushirikiano chanya au kufuata miamala isiyo chanya. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa masuala ya mafuta na uchumi, kwa sasa Iran haitozingatia sana upande usio chanya, kwa kuwa upande wa pili unaisukuma upande huo. Chris Cook amezidi kubainisha kwamba ametoa ushauri kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuangalia upya teknolojia ya kifedha na uwekezaji katika nishati na kwamba anataraji kuiona Tehran ikifunga mikataba ya kibiashara ya nishati na nchi jirani ikiwemo Iraq, Pakistan na Uturuki na hata mbali zaidi na nchi hizo. Amesema kuwa kwa kuingia katika ushindani wa kihistoria wa kieneo, Iran haitoweza kuhisi vikwazo vya Marekani. 

Barclays Bank ya nchini Uingereza

Wakati huo huo benki moja ya Uingereza imetangaza hatua ya Washington ya kutorefusha msamaha wake kwa wanunuzi wa mafuta ya Iran, kuwa kutaifanya bei ya nishati hiyo kupanda zaidi katika soko la dunia. Hayo yamesemwa na benki ya Barclays ambayo imetabiri kwamba Saudia na Imarati ambazo zinadai kuwa zina uwezo wa kuziba pengo la mafuta ghafi ya Iran, hazitaweza kudhamini nishati hiyo na badala yake inatazamiwa kuwa bei ya mafuta katika soko la dunia itapanda haraka. Jumatatu iliyopita Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alisema kuwa Saudia na Imarati zimeihakikishia Marekani kwamba hazitokubali soko la dunia la mafuta kupata dosari kutokana na kuwekewa vikwazo mafuta ya Iran. 

Maoni