Apr 24, 2019 07:24 UTC
  • Wasiwasi wa Marekani kuhusu matokeo hasi ya vikwazo dhidi ya mafuta ya Iran

Kutokana na wasiwasi wake wa uwezekano wa kufungwa lango bahari la Hormoz katika Ghuba ya Uajemi, serikali ya Marekani imetaka kutolewa dhamana ya kupita salama meli zinazobeba nishati ya mafuta katika lango hilo na la Bab al-Mandab katika Bahari ya Sham.

Afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kwamba Washington haikubaliani hata kidogo na tishio la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran la kufunga lango bahari la Hormoz ikiwa ni katika kujibu hatua ya hivi karibuni ya Marekani ya kutorefusha msamaha wa kununua mafuta uliokuwa umetolewa kwa maabdhi ya nchi zinazonunua mafuta kutoka Iran. Kutokana na wasiwasi wake huo Marekani imeitaka Iran na nchi nyingine zote kutoa dhamana ya kupita salama meli zote za mafuta katika malango hayo ya bahari. Siku ya Jumatatu na katika kukaribia mwaka wa kwanza tokea ijiondoe katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA, Marekani imetangaza kwamba haitarefusha tena msamaha huo tokea tarehe pili Mei mwaka huu.

Meli ya mafuta ikipita katika lango bahari la Hormor katika Ghuba ya Uajemi

Inasemekana kuwa Rais Trump wa Marekani pia anapanga kuziondolea msamaha wa vikwazo baadhi ya nchi zinazoendelea kushirikiana na Iran katika mradi wake wa nyuklia unaotekelezwa kwa malengo ya amani. Katika radiamali yake kuhusiana na suala hilo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa Tehran haiupi thamani wala itibari yoyote msamaha huo wa vikwazo na kwamba inafanya mashauriano ya ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kutoa jibu muafaka kwa hatua hiyo ya utawala wa Washington.

Tags

Maoni