Apr 24, 2019 10:23 UTC
  • Ukosoaji wa Rais wa China kwa siasa za kimabavu za Marekani dhidi ya mataifa mengine

Rais Xi Jinping wa China amesema kuwa, anapinga siasa za kibabe, utumiaji mabavu za baadhi ya madola makubwa dhidi ya mataifa mengine.

Rais Xi Jinping amesema hayo alipokutana na makamanda wa kigeni wa majeshi ya majini walioshiriki katika maadhimisho ya miaka 70 ya kuasisiwa jeshi la majini la China katika bandari wa Qingdao ya mashariki mwa nchi hiyo na kuongeza kuwa, mataifa ya dunia hayapaswi kutumia wenzo wa mabavu kwa ajili ya kuzitisha nchi nyingine. Rais wa China amesisitiza kuwa, mataifa yote yanapaswa kufungamana na suala la kuboresha mahusiano wakati wa migogoro na kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kieneo kama ambavyo yanapaswa pia kudhamini suala la kutatua hitilafu na mivutano inayohusiana na bahari. Rais Xi Jinping amesema bayana kwamba, usalama na utulivu wa bahari una uhusiano na usalama na maslahi ya mataifa ya dunia na ili kudhamini usalama wa bahari kunahitajika kuweko ulinzi wa pamoja. Matamshi ya Rais wa China ya kukosoa siasa za kibabe na utumiaji mabavu za Marekani katika kukabiliana na nchi nyingine aliyoyatoa katika maadhimisho ya mwaka wa 70 wa kuasisiwa jeshi la majini la China ni ishara ya wazi ya kupinga siasa za Marekani za kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine ambazo zinakwenda sambamba na ubabe wake huko katika eneo la majini la kusini mwa China.

Rais Xi Jinping

Siasa za kibabe na utumiaji mabavu za Marekani katika uga wa kimataifa hususan tangu aingie madarakani Rais Donald Trump zinaonekana kuchukua kasi na wigo mpana zaidi. Hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujiondoa katika makublaiano ya nyuklia ya JCPOA ambayo yaliungwa mkono na azimio 2231 la Baraza la Usalama la UUmoja wa Mataifa na madola makubwa duniani, ni sehemu ya utendaji mbovu wa Washington wa kupenda makuu ambao ni mfano wa wazi wa siasa za kimabavu za White House katika uga wa kimataifa ambazo zimekabiliwa na ukosoaji mkubwa wa jamii ya kimataifa.

Kuingilia masuala ya ndani ya Venezuela na kufanya njama za kutaka kuipundua serikali halali ya Rais Nicolas Maduro na hata kutoa vitisho vya kutaka kuishambulia kijershi nchi hiyo ya Amerika ya Latini na kisha kuweka madarakani serikali kibaraka sambamba na kutambua rasmi umiliki wa utawala haramu wa Israel kwa miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo vamizi, hatua ambayo inakiuka wazi maazimio ya Umoja wa Mataifa, ni mifano mingine ya wazi ya kushadidi siasa za kibabe na utumiaji mabavu za Marekani katika uga wa kimataifa. Hatua hizo za Marekani zimeibua wasiwasi na malalamiko ya jamii ya kimataifa dhidi ya siasa za kuchupa mipaka za Rais Donald Trump.

Maadhimisho ya miaka 70 ya kuasisiwa jeshi la majini la China katika mji wa bandari wa Qingdao

Kujiondoa Marekani katika mikataba ya kimataifa kama vile mkataba wa Biashara Huru ya Amerika ya Kaskazini (NAFTA), mkataba wa biashara katika ukanda wa Pasifiki na mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris, Ufaransa ni mifano mingine ya wazi inayodhihirisha siasa za kimabavu za Washington zenye lengo la kuyatwisha mataifa mengine matakwa yake.

Hata hivyo wenzo wa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya mataifa mengine hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umekuwa na madhara makubwa zaidi kwa wananchi wa nchi zilizowekewa vikwazo hivyo. Huu nao ni upande mwingine wa utumiaji mabavu kwa ajili ya kukabiliana na nchi na tawala ambazo haziko tayari kufuata siasa za Marekani.

Tab'an siasa za utumiaji mabavu za Marekani zimezifanya nchi pinzani kukurubiana na kuwa na aina fulani ya kauli moja katika kukabiliana na uafiriti na siasa hizi hatari za Marekani katika uga wa kimataifa. Inaonekana kuwa, msimamo wa China na Russia sambamba na nchi nyingine zinazopinga ubabe na utumiaji mabavu wa Marekani unaweza kushadidisha na kuongeza changamoto ya chuki dhidi ya siasa za viongozi wa Marekani katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Maoni