Apr 24, 2019 14:19 UTC
  • Reuters: Hatua ya serikali ya Trump dhidi ya Iran, imewatumbukiza raia wa Kimarekani katika matatizo makubwa

Shirika la Habari la Reuters limeandika kuwa hatua ya serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kutorefusha kibali kwa wanunuzi wa mafuta ya Iran, imepelekea kupanda kwa bei ya mafuta na kuibuka changamoto kubwa kwa raia wenyewe wa Marekani.

Shirika hilo limeongeza kwamba, hivi sasa watu wa tabaka la kati nchini Marekani wanalipwa mishahara ya muongo mmoja uliopita hivyo kitendo cha kupanda kwa bei ya mafuta kunakotokana na kushadidisha vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran, kimepelekea kuibuka matatizo makubwa kwa raia wa nchi hiyo. Aidha Shirika la Habari la Reuters limetabiri kwamba, mwenendo huo wa Marekani utasababisha kupanda zaidi kwa bei ya mafuta duniani. Jumatatu iliyopita ikulu ya Marekani ya White House ilitoa taarifa ikisema kuwa kuanzia tarehe pili Mei mwaka huu, Washington haitorefusha kibali cha kuendelea kununua mafuta ya Iran kwa ajili ya nchi kadhaa ambazo hadi sasa zimekuwa zikinunua mafuta ya nchi hii.

Shirika la Habari la Reuters

Mwaka jana Marekani ilikuwa imetangaza kwamba itafikisha uuzaji wa mafuta ya Iran kwenye kiwango cha sifuri, hata hivyo siasa hizo zilifeli na hivyo ikalazimika kuziruhusu nchi za China, India, Japan, Korea Kusini, Taiwan, Uturuki, Italia na Ugiriki kuendelea kununua mafuta ya Iran. Kutokana na tangazo la Marekani la kufuta kibali hicho, bei ya mafuta katika maeneo tofauti ya Marekani kama vile jimbo la California imepanda kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa huko nyuma kiasi cha nishati hiyo kuuzwa kwa Dola nne na senti 70 kwa kila galoni moja.

Tags

Maoni