Apr 25, 2019 07:11 UTC
  • Kikao cha Kim Jong-un na Rais Vladmir Putin wa Russia

Jumatano Kim Jong-un Kiongozi wa Korea Kaskazini aliwasili nchini Russia kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo kwa mara ya kwanza na Rais Vladmir Putin wa nchi hiyo.

Baada ya kuwasili mji wa Vladivostok wa mashariki mwa Russia Jong-un amekutana na kufanya mazungumzo ya kufana na Rais Putin. Kabla ya kuanza safari hiyo Kim Jong-un alisema kuwa, alitaraji kwamba katika mazungumzo na rais huyo wa Russia wangeweza kujadili masuala muhimu kuhusiana na mgogoro wa Rasi ya Korea na kustawishwa mahusiano kati ya Moscow na Pyongyang. Ukweli ni kwamba safari ya kiongozi huyo wa Korea Kaskazini nchini Russia kwa ajili ya mazungumzo ya kistratijia na rais wa nchi hiyo, na ambayo imekuja baada ya kuvunjika kwa duru mbili za mazungumzo kati yake na Rais Donald Trump wa Marekani nchini Singapore na Vietnam na katika muda ulio chini ya mwaka mmoja uliopita, imetoa ujumbe kwa White House kwamba sasa Pyongyang inaelekea upande wa kustawisha uhusiano wake na Russia. Hii ni katika hali ambayo kwa kuingia katika mazungumzo na Korea Kaskazini, Trump alitaraji kwamba angeweza kuishawishi Pyongyang ifuate siasa na sera za Washington, jambo ambalo halikufanikiwa. Kutofikiwa mwafaka kwenye duru mbili za mazungumzo kati ya Rais Donald Trump na Kim Jong-un, kumeifanya Korea Kaskazini ifikie natija hii kwamba, Marekani ni nchi isiyoaminika na isiyo na itibari, ambayo licha ya Pyongyang kutekeleza makubaliano ya kusimamisha majaribio yake ya makombora na silaha za nyuklia, lakini haikuweza kutekeleza hata sehemu ndogo tu ya mapatano yao.

Baada ya Kiongozi wa Korea Kaskazini kuwasili mji wa Vladivostok wa mashariki mwa Russia hapo jana

Katika uwanja huo, siku chache zilizopita, Korea Kaskazini sambamba na kulifanyia majaribio kombora lake jipya, ilitoa tahadhari kwa Marekani kwamba itarejea haraka kwenye hali yake ya huko nyuma ya kabla ya kuanza mazungumzo ya pande mbili, jambo ambalo litawashangaza viongozi wa White House. Aidha ilisisitiza kwamba Pyongyang haipo tayari kuendelea na subira yake mkabala wa kupenda makubwa kwa Marekani wala kufanya mazungumzo yasiyo na natija. Hata hivyo Kim Jong-un mbali na kutoa amri ya kufanya majaribio ya kombora hilo alimpa Rais Donald Trump muhula wa hadi mwisho wa mwaka huu, kuhakikisha anabadilisha mwenendo wake mbovu katika mazungumzo na Korea Kaskazini, ili kwa njia hiyo aweze kuokoa mazungumzo ya nchi mbili na kuyafanya yasivunjike kabisa. Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini anafahamu vyema kwamba Trump ambaye katika kipindi cha baada ya mazungumzo ya duru ya kwanza nchini Singapore na pia duru ya pili huko nchini Vietnam, aliiwekea vikwazo vingine vya mwaka mmoja serikali ya Pyongyang, hivyo hawezi kuwa tayari kuingia katika mazungumzo ambayo hayaishii kwenye mapatano ya ushindi wa pande mbili. Katika mazingira hayo, ni baada ya kuvunjika mazungumzo kati ya Korea Kaskazini na Marekani na baada ya Washington kushadidisha vikwazo dhidi ya nchi hiyo, ndipo Kim Jong-un akaamua kuimarisha uhusiano wake na Russia kwa ajili ya kupata msaada wake katika kipindi cha duru mpya ya vikwazo vya Washington.

Kim Jong-un ameonyesha kutokuwa na imani tena na Rais Donld Trump wa Marekani 

Katika uwanja huo, Artyom Lukin, muhadhiri wa Chuo Kikuu cha Vladivostok nchini Russia anasema: "Alipokutana na Rais Vladmir Putin, Kim Jong-un aliomba msaada wa kiuchumi, ambapo hata hivyo ni suala lililo mbali kwamba Putin ataweza kutekeleza matakwa ya Pyongyang." Pamoja na hayo kwa kuzingatia kuwa siku chache zilizopita kiongozi huyo wa Korea Kaskazini alimuandikia barua Rais Putin ambayo ndani yake alielezea azma ya Pyongyang ya kutaka kuimarisha usalama katika eneo la Rasi ya Korea, hivyo kuna uwezekano kwamba kiongozi huyo kijana anakusudia katika safari yake nchini Russia kumshawishi Rais Putin aweze kusaidia katika utatuzi wa mzozo wa Rasi ya Korea. Inasemekana kwamba huenda Kim Jong-un amechukua msimamo huo kutokana na kufeli mazungumzo ya pande mbili na rais wa Marekani na pia kuktokuwepo kwa upande wa upatanishi kwa ajili ya kuweka mambo sawa, ili kuepusha uzoefu mwingine mbaya wa kufeli mazungumzo ya pande kadhaa za Russia, China na nchi nyingine za eneo. Tajiriba chungu iliyoshuhudiwa mwaka 2007 kupitia mazungumzo ya pande sita ya nyuklia kwa kushirikishwa Korea Kaskazini, Korea Kusini, Japan, China, Marekani na Russia na ambayo yalifeli kutokana na Marekani kutotekeleza ahadi zake mkabala wa hatua chanya zilizotekelezwa na Pyongyang ikiwemo ya kusimamisha miradi yake ya nyuklia.

Maoni