Apr 25, 2019 07:27 UTC
  • Associated Press: Washington kuchunguza upya kibali cha ununuzi wa mafuta ya Iran

Shirika la Habari la Associated Press limetangaza kulegeza msimamo kwa mara nyingine serikali ya Marekani kwa lengo la kuchunguza hatua ya kutoa kibali kipya kwa wanunuzi wa mafuta ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maafisa na washauri kadhaa katika Kongresi ya Marekani ambao hawakutaka kutaja majina yao wamefichua kwamba, moja ya mambo yanayochunguzwa ni serikali ya Marekani kuwaruhusu wanunuzi wa mafuta ya Iran  kudumisha miamala yao ya mafuta na Iran hata baada ya tarehe pili mwezi Mei mwaka huu. Aidha maafisa hao wameongeza kwamba baada ya hatua hiyo, serikali ya Marekani itatoa kibali cha kusafirisha na kusafisha mafuta ya Iran.

Shirika la Habari la Associated Press lililofichua habari hiyo

Aidha Shirika la Habari la Associated Press limeandika kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inafikiria pia uwezekano wa kuziruhusu baadhi ya nchi wanunuzi wa mafuta ya Iran kuendelea kufanya hivyo bila kuwekewa vikwazo. Jumatatu iliyopita, serikali ya Marekani na sambamba na kukaribia kutimia mwaka mmoja tangu nchi hiyo ilipojiondoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, ilitangaza kwamba kuanzia tarehe pili Mei mwaka huu haitarefusha tena kibali kwa ajili ya nchi zinazonunua mafuta ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hatua ambayo imepelekea kupanda kwa bei ya mafuta ndani na nje ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa duru za habari nchini Marekani, bei ya mafuta katika maeneo tofauti ya nchi hiyo kama vile jimbo la California imepanda kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa huko nyuma kiasi cha nishati hiyo kuuzwa kwa Dola nne na senti 70 kwa kila galoni moja.

Tags

Maoni