Apr 25, 2019 07:34 UTC
  • Marekani yalazimika kurudi nyuma, yatoa msamaha kwa vikwazo vya Jeshi la Iran la IRGC

Serikali ya Marekani imelazimika kulegeza hatua yake ya awali ambapo imetoa msamaha wa baadhi ya vikwazo vya nchi hiyo dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH

Taarifa iliyotolewa na Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, imeweka wazi msamaha huo. Kwa mujibu wa msamaha huo mpya, viongozi wa serikali za kigeni, mashirika na asasi za kiraia ambazo zimekuwa zikishirikiana na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) sasa hawatazuiwa kuingia Marekani. Msamaha huo umechapishwa na jarida rasmi la serikali linaloitwa 'Federal Register.' Aidha Pompeo amedai kuwa, kutolewa msamaha huo wa vikwazo ni kwa maslahi ya usalama wa taifa la Marekani.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC)

Jumatatu ya tarehe nane mwezi huu, serikali ya Marekani na katika hatua chafu na isiyo ya kisheria, ililiweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH katika orodha yake ya kigaidi sambamba na kutishia kuziwekea vikwazo taasisi, mashirika na watu watakaoshirikiana na jeshi hilo. Hatua hiyo ilikabiliwa na radiamali kali kutoka kwa jamii ya kimataifa. Aidha hivi karibuni, Pompeo alikiri kwamba Washington ililiweka jeshi hilo la (IRGC) katika orodha ya makundi ya kigaidi kwa sababu ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Hii ni kwa sababu jeshi hilo limekuwa na nafasi kubwa katika kupambana na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani na utawala haramu wa Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi.

Maoni