Apr 25, 2019 14:10 UTC
  • Mafuta yapanda bei baada ya vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran

Bei ya mafuta katika soko la dunia imeongezeka na kufikia kiwango cha juu kabisa katika kipindi cha miezi sita iliyopita kutokana na vikwazo vipya vya mafuta vya Marekani dhidi ya Iran

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, leo Alkhamisi bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia imeongezeka sana kutokana na hofu ya kupungua bidhaa hivyo muhimu baada ya Marekani kuweka vikwazo vipya dhidi ya mafuta ya Iran na Venezuela. Kwa mujibu wa shirika hilo la habari la Uingereza, bei ya mafuta imefika kiwango cha juu kabisa katika kipindi cha miezi sita iliyopita kiasi kwamba mafuta ya Brent ya Bahari ya Kaskazini leo yameuzwa kwa dola 74 na senti 57 kwa pipa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mafuta ya Marekani ya West Texas Intermediate yameongezeka bei na leo yameuzwa kwa dola 65 na senti 89 kwa pipa kutokana na mashinikizo mengi ya kuongeza akiba ya mafuta hayo ghafi.

Marekani kamwe haiwezi kuizuia Iran kuuza mafuta yake na hakuna nchi yoyote itakayoruhusiwa kuchukuka nafasi ya Iran katika soko la mafuta duniani

 

Bei ya juu kabisa ya mafuta ilikuwa ni ile ya tarehe 31 Oktoba 2018 ambapo siku hiyo kila pipa moja la mafuta ya West Texas Intermediate liliuzwa kwa dola 66 na senti 60.

Tangu siku ya Jumatatu bei ya mafuta imekuwa ikipanda kutokana na Marekani kutangaza kuwa haitaongeza muda wa ruhusa ya kununua mafuta ya Iran kwa wanunuzi wakuu wa bidhaa hiyo muhimu.

Mwaka jana Marekani ilidai kuwa itaizuia kikamilifu Iran kuuza mafuta yake hata hivyo baada ya kuona kuwa ndoto yake hiyo ni muhali kuaguka, ilitoa ruhusa kwa baadhi ya nchi kama China, India, Japan, Korea Kusini, Uturuki, Italia, Ugiriki na Taiwan kuendelea kununua mafuta ya Iran.

Maoni