Mei 04, 2017 07:28 UTC
  • Mwanasayansi Muirani achangia kuunda miwani maalumu ya kuona usiku

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika makala hii ambayo huangazia mafanikio ya wanasayansi nchini Iran na maeneo mengine duniani katika sekta za sayansi na teknolojia.

Mwezi Desemba mwaka jana wanasayansi wa Australia kwa kushirikiana na mwanasayansi Muirani waliweza kuunda nano  fuwele (nano crystal) ambayo ni mara 500 ndogo zaidi ya unywele wa mwanadamu na ambayo huibua uwezo wa kuona katika giza. Kwa msingi huo nano fuwele hiyo inaweza kutumika kutegeneza miwani isiyo mizito yenye uwezo wa kuona usiku.

Profesa Dragomir Neshev wa Chuo Kikuu cha Australia (ANU) amesema miwani hiyo miepesi ya kuona usiku inaweza kuchukua sehemu ya ile mizito ya sasa ambayo hutumika kuona siku.

Miwani ya kuona usiku

Mtafiti msaidizi katika mradi huo ni mwanasansi Muirani Dkt. Muhsin Rahmani wa Chuo Kikuu cha Australia ambaye anasema mafanikio hayo ni ya kihistoria katika uga wa nanophotonics ambao unajumuisha kuchunguza tabia ya nuru na maingiliano ya vitu vingine na nuru katika kiwango cha nano.

Akifafanua zaidi Dkt. Rahmani anasema nano fuele hizo zinaweza kuhamisha kiwango kikubwa cha mwangaza na kuibua miale mikubwa ya mwanga. Uvumbuzi huu ambao ni wa kwanza kabisa duniani umechapishwa katika jarida la Nano Letters na tayari Dkt Rahmani ameshahutubia Kongamano la Taasisi ya Fizikia ya Australia kuhusu mafanikio hayo. Dkt. Rahmani amepokea zawadi ya uvumbizi  ya ARC nchini Australia kutokana na utafiti wake katika Kitivo cha Fizikia na Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Australia.

Katika mafanikio mengine, watafiti Wairani wa shirika la kutengeneza madawa la Cedrindaru mkoani Alborz magharibi mwa Tehran, wamefanikiwa kutumia mbegu za mmea wa Lin (Flaxseed) kutegeneza  dawa ya kuzuia ugonjwa wa moyo.

Kapsuli za Iraflax

Jina la kisayansi la mmea wa Flaxseed ni Limum Usitatissimum na huchukua muda wa mwaka mmoja kukua hadi kiwango cha kichaka. Mafuta ya Flaxseed ni chanzo muhimu sana ya asidi ya mafuta aina ya Omega 3. Aina hii ya asidi  huwa ya mafuta ambayo hayajakolea au non-saturated na ni muhimu katika kulinda kiwango cha kolestroli au mafuta yanayosababisha unene mwilini.

Daktari Vahid Qaravi Kashani mtekelezaji wa maradi huu na ambaye ni mkurugenzi wa Shirika la Cedrindaru anafafanua kuhusu dawa walioyzalisha kwa kutumia mbegu za mmea wa Lin au Flaxseed na kusema: "Kapsuli ya Iraflax imezalishwa kwa kutumia mafuta ya flaxseed na tumetumia mmea ambao umekuzwa kwa kutegemea mbolea asilia pasina kuwepo kemikali. Dawa hii ina Omega 3 na 9 na inatumika katika kuzuia magonjwa ya moyo. Dawa hii ni ya kutimiliza na si yenye kujitegemea kikamilifu na inazalishwa katika muundo wa kapsuli zijulkanazo kama geSoft."

Hali kadhalika kiwanda hicho kimezalisha poda ya dawa hiyo ambayo hutumika kuzuia aina mbali mbali za saratani. Poda hii ina kiasi kikubwa cha madini ya potasimu ambayo inaweza kutumika katika kuzuia kuibuka saratani.

Kwa mara ya kwanza nchini Iran wanasayansi wamefanikiwa kuunda maabara inayotegemea teknolojia ya Virtual Reality maarufu kama VR. Kwa kifupi, Virtual Reality ni mazingira ya picha au mazingira ya dhania na ni teknolojia iliyoenea sana katika intaneti. Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Sanaa cha Tehran wameanzisha maabara hiyo ambayo ni maalumu kwa ajili ya michoro ya miji na usanifu majengo.

Maabara ya Virtual Reality nchini Iran

Mchakato wa awali wa kuanzisha kituo hicho cha utafiti na maabara ulianza  zaidi ya miaka mitatu iliyopita. Mtayarishaji wa maabara hii ya VR anasema lengo kuu la kuanzisha mradi huo ni kutumia Virtual Reality yaani mazingira ya picha au mazingira ya dhania pamoja na teknolojia nyingine za kisasa katika utafiti kuhusu ujenzi wa miji na usanifu majengo. Aidha anasema teknolojia hii inaweza kutumika katika animation na kuunda michezo ya kompyuta.

Lengo jingine la kuanzishwa maabara ya Virtual Reality nchini Iran ni kuimarisha uhusiano wa baina ya sekta ya viwanda na mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali ili kuwepo ushirikiano katika ramani na miradi ya kujenga miji na kuimarisha miradi inayoendelea ya ujenzi.

Moja ya faida za maabara ya VR  ni kuwa hupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kufanyika makosa wakati wa ujenzi kwani maabara hiyo huwa imeshafanya majaribio yenye lengo la kurahisisha kazi. Maabara hii hivi sasa ina suhula bora zaidi za utaifti wa VR yaani  HMD na mfumo wa Motion Leap. 

Na katika mafanikio mengine, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilishika nafasi ya tatu duniani mwaka 2015 katika makala za jarida  lenye itibari zaidi la kisayansi duniani linajulikana kama Science International. 

Mwezi Aprili, Mkurugenzi wa  Kituo cha Kimataifa cha Makala za Kisayansi Katika Ulimwengu wa Kiislamu alisema Iran imestawi kwa kasi sana kwa mtazamo wa utafiti na makala  zinazochapishwa katika majarida ya kimataifa.

Iran inastawi kisayansi

Mohammad Javad Dehqani anasema: "Kutokana na ustawi wa asilimia 15 kwa matazamo wa makala za kisayansi, Iran imezipita nchi kama vile Russia, Malaysia, China, Uturuki, India na Poland na hivyo iko katika nchi 25 bora kwa utafiti duniani.

Mwaka 2015 Iran iliwasilisha makala 43,111 katika Scopus, kituo kikubwa zaidi cha marejeo ya makala za kisayansi duniani ambazo huchunguzwa na wataalamu wa kila fani husika. Kituo hiki huwa na makala za sayansi, teknolojia, tiba, sayansi za kijamii na sanaa. Mwaka 2016 kiwango hicho kiliongezeka kwa asilimia 15 ambapo makala 49,535 za Iran ziliwekwa katika kituo cha data cha Scopus.

Dehqani anasema, kwa kuzingatia kuwa takwimu za mwaka 2016 bado hazijakamilika, na data za mwaka 2017 baado zinakusanywa, Iran sasa imeorodheshwa katika nafasi ya 14 duniani kwa mtazamo wa makala za kisayansi.

Afisa huyo anasema kuwa mwaka 2011 Iran ilizalisha asilimia 1.5 ya makala za kisayansi duniani na mwaka 2016 kiwango hicho kilifika asilimia 1.8 huku mwaka 2017 idadi hiyo ikitarajiwa kuwa asilimia 2.1

Wapenzi  wasikilizaji tunafikia mwisho wa makala yetu kwa leo na tunawashukuruni nyote, kwaherini.

Tags

Maoni