Dec 18, 2017 08:16 UTC
  • Kojojo au babaje ambaye ni koa anayeishi baharini
    Kojojo au babaje ambaye ni koa anayeishi baharini

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia mafanikio ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.

Watafiti Wairani hivi karibuni wameunda dawa mpya ya kutibu saratani kwa kutumia kojojo au babaje ambaye ni koa anayeishi baharini na kwa Kiingereza hujulikana kama Sea Cucumber. Kwa karne nyingi,  watu wa bara Asia hasa Wachina wamekuwa wakitumia kojojo kama chakula kitamu na pia katika kuunda dawa za kienyeji zenye kutibu magonjwa kama vile ugonjwa wa pumu au asthma, shinikizo la damu, ugonjwa wa uvimbe wa mifupa na anaemia ambao ni ugonjwa wa kukosa idadi ya kutosha ya seli nyekundu za damu. Kojojo amekuwa akitumiwa kama dawa kutokana na kuwa ana aina mbali mbali za vitamini, madini na baadhi ya protini.

Hivi sasa viumbe vya habari vina nafasi muhimu sana katika sayansi ya tiba na dawa. Ni kwa sababu hii ndio mradi wa utafiti wa wanasayansi Wairani wakaamua kuchunguza faida za kitiba za kojojo au babaje ambaye anapatikana katika Ghuba ya Uajemi. Kufuatia uchunguzi wao, wanasayansi Wairani wamefanikiwa kutegeneza dawa zilizo dhidi ya saratani na dawa zinginezo zenye kutibu magonjwa mengine yalioenea sana miongoni mwa wanadamu.

kojojo au babaje

Kiumbe huyu wa baharini pia ana  virutubisho ambavyo huvunja vunja na kuondoa sumu mwilini, ambavyo kitaalamu huitwa antioxidants.

Mikanda ya tumbo yenye uwezo wa kuzuia mnunurisho

Katika uga wa sayansi na teknolojia, Wanasayansi Wairani hivi karibuni wameweza kufanikiwa kubuni na kuzalisha kwa wingi mikanda ya tumbo yenye uwezo wa kuzuia mnunurisho na mawimbi ya redio kufika tumboni. Mikanda hii ambayo ni maalumu kwa wanawake wajawazito imetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya nano inayotumika kuzuia mawimbi ya radio au electormagnetic na pia ina sifa ya kupambana na vijidudu. Kwa mfano simu za mkononi huwa na mnunurisho (radiation) ambao mbali na kuwa na madhara kwa mwanadamu pia huwa na athari hasi kwa kiumbe aliye katika tumbo la mwanamke mjamzito. Utumiaji wa mara kwa mara wa simu ya mkononi na kuzungumza kwa muda wa zaidi ya dakika 20 ni jambo linaloweza kuongeza hatua kwa hatua joto katika ubongo na hilo husababisha kubadilika muundo wa kibiolojia wa ubongo. Kadiri simu inavyokukaribia ndivyo miale na mawimbi ya chombo hicho huwa na athari mbaya zaidi. Kwa ujumla ni kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mawimbi ambayo huingia ubongoni kutoka katika simu ya mkononi huwa na athari mbaya katika utenda kazi wa ubongo wa mwanadamu. Kwa hivyo mikanda hiyo iliyoundwa na wanasayansi Wairani inaweza kutoa mchango mkubwa katika kumlinda mtoto kabla ya kuzaliwa. Watengenezaji wa mkanda ulio dhidi ya mnunurisho wanasema wametumia teknolojia ya nano na kuunda bidhaa ambayo inazalishwa kikamilifu nchini Iran. Kabla ya mafanakio hayo ya wanasayansi Wairani, ni Marekani na Italy pekee ndizo zimekuwa zikimiliki teknolojia hiyo. Lakini teknolojia ambayo imekuwa ikitumiwa na nchi hizo mbili ni ile yenye kutegemea nano yenye madini ya fedha ambayo hayapaswi kugusana na ngozi na hili ni tatizo ambalo wanasayansi Wairani wameweza kulitatua katika mkanda walioutengeneza. Nukta nyingine ni kuwa mkanda wa tumbo wenye uwezo wa kuzuia mnunurisho ambao umeundwa Iran unauzwa kwa bei nafuu mara tatu chini ya mshabaha wake uliotengenezwa katika nchi za kigeni. La muhimu zaidi ni kuwa mkanda huo wa tumbo uliotengenezwa Iran hauna matatizo kama yale ya mikanda mshabaha iliyotengenezwa katika nchi za kigeni.

Mikanda ya tumbo yenye uwezo wa kuzuia mnunurisho

Wataalamu Wairani wanasema mkanda waliounda una uwezo wa kuzuia zaidi ya asilimia 99 ya mawimbi na mnunurisho, kutoka simu za mkononi, microwave, WiFi na vifaa vingine vya kieletroniki ndani ya nyumba . Kwa msingi huo mkanda huo huweza kulinda kijusi kisipate madhara hatari yanayotokana na mnunurisho au mawimbi. Wataalamu wanasema kati ya madhara hayo ni kama vile hatari ya kuibuka saratani, kupoteza ujauzito n.k. Aidha athari haribifu za mawimbi na mnunurisho katika mazingira hupelekea kijusi kukumbwa na matatizo ya kijenetiki na kwa msingi huo kutumiwa mkanda huu wenye kuzuia mnunurisho na mawimbi ya redio ni jambo la dharura kwa wanawake wajawazito.

Mishipa bandia ya damu

Kwa mara ya kwanza duniaani hivi karibuni tulishuhudia kuvumbuliwa mbinu mpya ya kukuza mishipa bandia ya damu katika meno na hivyo kuwasaidia wanaopata matatizo wakati wa kung'olewa jino au meno.

Wakati jino linapooza au kukumbwa na vijidudu au ikiwa limevunjika sehemu moja, huwa hakuna budi ila kuling'oa. Katika kazi hiyo ya kung'oa jino ule mtandao wa kufikisha damu kwenye mfumo wa neva katika mzizi wa jino huharibika na hivyo kuacha eneo hilo likiwa katika hatari ya kukumbwa na maambukizi yanayotokana na vijidudu.

Mtaalamu wa kuunda mishipa bandia ya damu

Katika kukabiliana na tatizo hilo wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Oregon nchini Marekani wamefanikiwa kuunda mishipa bandia ili kuepusha tatizo la jino kukosa kumea baada ya kung'olewa.

"Wakati wa kukarabati jino, mfumo wa damu na neva huharibika na kukosa uhai au radiamali ya kibiolojia na uwezo wa kujihami", anasema Luir Bertassoni, profesa msaidizi katika kitengo cha ukarabati wa meno katika chuo hicho. Anaongeza kuwa iwapo meno ya mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 18 yatakumbwa na tatizo katika mfumo wa damu na neva anaweza kupoteza meno yake na hilo kupelekea kuwepo ulazima wa kuweka meno bandia.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, Bertassoni na timu yake wamefanikiwa kuunda mfumo bandia wa mishipa ya damu. Ambapo baada ya siku saba tishu ambazo huunda meno ya mwanadamu huanza kuibuka karibu na ukuta wa jino na hapo mishipa bandia huanza kuibukia katika jino.

 

Tags

Maoni