Mar 05, 2018 07:12 UTC
  • Aya na Hadithi (10)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana nanyi tena katika sehemu hii ya 10 ya mfululizo wa vipindi vya Aya na Hadithi.

Katika kipindi kilichopita tulipitia kwa ufupi Sura Tukufu ya at-Takaathur ili kupata maana na makusudio halisi ya neno 'neema' lililotumika humo ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasisitiza kuwa atawauliza waja wake Siku ya Kiama juu ya neema hiyo. Ilibainika wazi baada ya kuchunguza kwa kina Sura hiyo kwamba maana ya neema hiyo inapasa kuwa ni neema maalumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo inapasa kuwaokoa wanadamu na kuwakinga na kujifaharisha kusikokuwa na maana ambako kunatokana na ukusanyaji kupita kiasi wa neema za kimaada. Ni wazi kuwa kujifaharisha huko kunaweza kumfanya mwanadamu aghafilike na ukamilifu wake wa kimaanawi, ibada na kutembea kwenye njia nyoofu ambayo inakusudiwa kutengeneza na kuratibu maisha yake ya milele huko Akhera.

Wapenzi wasikilizaji, maana iliyokusudiwa na Aya hii tukufu imesisitizwa kwenye Hadithi kadhaa ambazo tulinukuu baadhi katika kipindi cha wiki iliyopita. Tunanukuu hapa hadithi nyingine kati ya hadithi hizo kama ilivyonukuliwa katika kitabu cha ad-Da'waat. Abu Hanifa amenukuliwa akimuuliza Imam Swadiq (as) maana halisi ya 'neema' inayokusudiwa katika Surat at-Takaathur baada ya kudhani kuwa maana yake ilikuwa ni chakula na vinywaji. Imam alimwambia: 'Ikiwa Mwenyezi Mungu atakusimamisha mbele yake Siku ya Kiama na kuuliza juu ya kila chakula na kinywaji ulichokunywa bila shaka utasimama mbele yake muda mrefu sana.  Akasema: Basi maana ya 'neema' ni nini kwako wewe, ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu? Aba Abdillah (as) akamjibu kwa kusema: Neema ni sisi Ahlul Beit ambao Mwenyezi Mungu amewaneemeshea waja. Waliungana kupitia kwetu baada ya kuhitilafiana, Mwenyezi Mungu akaleta upendo mioyoni mwao kupitia kwetu, akawaokoa kutoka kwenye shirki na maasi kupitia kwetu, akawafanya kuwa ndugu kupitia kwetu na kuwaongoza kupitia kwetu. Hivyo neema hii haikatiki na Mwenyezi Mungu atawauliza juu ya haki ya neema hii ambayo aliwaneemesha nayo, nayo ni Mtume na Aali zake.'

 

Ndugu wasikilizaji, Maimamu wotoharifu wa Kizazi cha Mtume (as) wamesisitiza katika Hadithi nyingi kwamba neema ambayo waja wa Mwenyezi Mungu wataulizwa Siku ya Kiama ni Mtume Mtukufu (saw) na Kizazi chake ili wapate kuwaongoza katika njia sahihi ya wongofu na hivyo kuwaepusha na moto mkali wa Jahannam. Jambo hilo linawezekana tu kwa waja wema wa Mwenyezi Mungu kufuata mafundisho na maagizo ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlul Beit wake watoharifu ambao wamekingwa na kila aina ya dhambi na maovu. Hebu tuzingatie kwa makini Riwaya hii ambayo imenukuliwa na Sheikh as-Swadouq katika kitabu chake cha Uyun Akh'bar ar-Ridha (as) kupitia Ibrahim bin Abbas as-Suli ambayo inasema: 'Siku moja tulikuwa mbele ya Ali bin Musa (as), baadhi ya mafuqaha waliokuwa hapo wakasema: Neema hii hapa duniani ni maji baridi. Imam Ridha akasema kwa sauti: Hivi ndivyo mnavyofasiri nyinyi kwa kubahatisha tu. Kundi moja linasema ni maji baridi, jingine ni chakula kitamu nao wengine wanasema ni usingizi mzuri (mnono). Hakika baba yangu ameniambia kwa kumnukuu baba yake Aba Abdillah as-Swadiq (as) kwamba kauli zenu hizi ziliwahi kutamkwa mbele yake kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema, naye (as) akakasirika na kusema: Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hawaulizi waja wake kuhusu kile alichowapa kwa wema na wala hawasimbulii au kuwasimanga. Kufanya simbulio au simango kutokana na wema ni jambo linalowachukiza viumbe basi ni vipi jambo hilo litahusishwa na Muumba Mtukufu hali ya kuwa viumbe hawaridhishwi nalo?! Lakini neema ni kutupenda sisi Ahlul Beit. Mwenyezi Mungu atawauliza waja wake kuhusu ufuasi wao kwetu, baada ya Tauhidi na Utume, kwa sababu iwapo mja atatekeleza hilo, humfikisha kwenye neema ya Pepo isiyokuwa na mwisho. Baba yangu aliniambia hilo kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu zake kutoka kwa Amir al-Mu'mineen Ali (as) kwamba alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema: 'Ewe Ali! Hakika jambo la kwanza atakaloulizwa mja baada ya kufariki kwake dunia ni shahada ya 'hakuna mungu isipokuwa Allah na kwamba Muhammad (saw) ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba wewe ni Walii wa waumini kuhusiana na kile alichokijalia Allah nami nikakujaalia wewe. Basi anayekiri hilo na kuliamini huelekea kwenye neema ambayo haina mwisho."

***********

Kwa maelezo haya wapenzi wasikilizaji, inabainika wazi kwamba jambo ambalo Mwenyezi Mungu atawauliza waja wake Siku ya Kiama ni Hoja na Maimamu Wake maasumina (as). Hii ni kwa sababu kuwafuata watukufu hao huwadhaminia waja wongofu kutokana na upotovu na kuwafikisha kwenye neema ya milele na isiyokuwa na mwisho.

Na kwa maelezo haya ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha juma hili cha Aya na Hadithi ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags

Maoni