Mar 25, 2018 07:36 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 778 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir.

Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 12 ambayo inasema:

وَمَا يَسْتَوِي الْبَحْرَانِ هَـٰذَا عَذْبٌ فُرَاتٌ سَائِغٌ شَرَابُهُ وَهَـٰذَا مِلْحٌ أُجَاجٌ ۖ وَمِن كُلٍّ تَأْكُلُونَ لَحْمًا طَرِيًّا وَتَسْتَخْرِجُونَ حِلْيَةً تَلْبَسُونَهَا ۖوَتَرَى الْفُلْكَ فِيهِ مَوَاخِرَ لِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

Na bahari mbili haziwi sawa; haya ni matamu yenye ladha, mazuri kunywa. Na haya ni ya chumvi, machungu. Na kutokana na bahari zote mnakula nyama freshi. Na mnatoa mapambo mnayo yavaa. Na unaona ndani yake marikebu zinakata maji ili mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru.

Aya tulizosoma kwenye darsa iliyopita ziliashiria nguvu na uwezo wa Allah SW katika kumuumba mwanadamu na baadhi ya sifa maalumu za kiumbe huyo. Aya hii ya 12 inagusia ishara na alama nyengine ya Mwenyezi Mungu katika dunia ya maumbile na kueleza kwamba: bahari za dunia hii zina hali namna mbili; baadhi yao ni za maji baridi na matamu, na baadhi yao ni za maji machungu ya chumvi, lakini Allah SW ameweka katika aina zote hizo mbili anuai za vyakula na vivazi kwa ajili ya mwanadamu. Ni aina mbalimbali za viumbe wa majini na aina tofauti za samaki ambao mwanadamu hakusumbuka wala hakuchangia kwa namna yoyote ile katika kuwepo na kuzaliana kwao; isipokuwa anachofanya ni kuwavua na kuwafikisha fukweni kwa ajili ya matumizi yake mwenyewe au kuwauzia wenziwe. Chanzo hicho muhimu na adhimu cha chakula hakikidhi mahitaji ya watu wanaoishi maeneo ya pwani pekee, bali kinatosheleza pia mahitaji ya wakazi wa maeneo yaliyo mbali kabisa na bahari. Lakini mbali na chakula, vito vya kuvutia na vyenye thamani kubwa mno kama lulu na marijani vinapatikana kwenye vina vya bahari kuu na kuingia mikononi mwa wazamiaji pasi na kuvitolea gharama yoyote. Ikiwa chini kwenye vina vya bahari zinapatikana anuai za vyakula kwa ajili ya wanadamu, juu ya bahari hizo ni njia kubwa na pana ambazo viumbe hao hawajazitolea gharama zozote katika ujenzi wala utunzaji wake, bali wanazitumia kupitishia vyombo vyao vya merikebu, meli na majahazi kwa ajili ya kusafirishia bidhaa na abiria kutoka pembe moja hadi nyengine ya dunia. Kiasi kwamba mameli makubwa makubwa ambayo isingewezekana katu kutembea ardhini au angani, hukata masafa kwa kuelea bila ya tabu yoyote juu ya mawimbi ya bahari. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, bahari ni moja ya vyanzo muhimu vinavyodhamini chakula, ambavyo Allah SW amewaandalia wanadamu bila ya wao kuvitolea gharama yoyote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, mwenendo wa maisha ya mwanadamu nao pia uko kama maji ya bahari; baadhi ya wakati huwa matamu, na wakati mwengine huwa machungu. Ikiwa mtu atakuwa nahodha na mvuvi hodari, anaweza kuchuma na kufanikiwa katika hali zote hizo mbili za maisha yake. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kuvitumia na kuneemeka navyo vitu vya mapambo ni jambo linalokubaliwa na Uislamu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 13 ambayo inasema:

يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ

 Anauingiza usiku katika mchana, na anauingiza mchana katika usiku. Na amelitiisha jua na mwezi, kila kimoja kinakwenda kwa muda maalumu. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Na hao mnao waomba badala yake hawamiliki hata utando wa kokwa ya tende. 

Baada ya aya tulizosoma zilizozungumzia ishara na alama za tauhidi katika nafsi ya mwanadamu na katika upeo wa ulimwengu wa maumbile, aya hii ya 13 inaashiria alama nyengine ya ulimwengu wa maumbile na kueleza kwamba: mzunguko wa sayari ya dunia kulizunguka jua unaowezesha kupatikana usiku na mchana kwa wakazi wa sayari hiyo kunafanyika kwa tadbiri na uendeshaji mambo wake Mola. Usiku na mchana ambao urefu wao unatafautiana katika misimu minne ya mwaka na ambao unaelezewa kama vitu viwili vinavyoingiliana, kila mmoja hautokei kwa ghafla tu, lakini huingia na kutoka taratibu, ambapo mchana humalizika kwa kuzama jua taratibu na nafasi yake kuchukuliwa na giza linalotanda kidogo kidogo la usiku. Huwa vivyo hivyo pia kutoweka kwa giza la usiku na kupambazuka alfajiri na kuchomoza jua asubuhi. Kisha aya inaendelea kwa kuitaja sababu ya kuwepo hali hiyo kuwa ni kutiishwa jua na mwezi na kueleza kwamba: kwa amri ya Allah SW, jua lenye adhama limetiishwa ili kuwatumikia wanadamu kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya mwangaza na joto unaoandaa mazingira ya kuota na kukua miti na mimea kutoka kwenye tumbo lisilo na uhai la ardhi. Wakati giza la usiku linapoingia pia, mwezi huwa mithili ya kioo kikubwa kinachoakisi mwangaza wa jua, ambapo kwa kutokuwepo jua huwa hauruhusu giza mutlaki litande angani na kuwagubika wakazi wa ardhini na kuwataabisha wanaosafiri usiku baharini au katika nchi kavu. Pamoja na yote hayo wanadamu wasidhani kama sayari hii ya dunia, jua na mwezi ni vitu vya kudumu milele na kubakia daima dawamu. Sayari na maumbo yote ya angani yamepangiwa kuwa na umri maalumu, na iko siku vyote hivyo vitasambaratika na kutoweka. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba: waumini, wao wanamwamini Mungu huyo, ambaye ulimwengu wote wa maumbile uko kwenye mamlaka yake na kila kitu kinaendeshwa kwa irada na tadbiri yake. Lakini washirikina na makafiri, ambao badala ya Mwenyezi Mungu wanawaendea na kuwaelekea wengine wanaodhani kuwa wana taathira katika mambo yao, wajue kwamba yeyote mwengine ghairi ya Allah hana uwezo wa kuumba na kumiliki hata ncha ya sindano katika ulimwengu na vilivyomo ndani yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kanuni za maumbile zimewekwa kwa hekima na tadbiri ya Mwenyezi Mungu na ziko chini ya mamlaka na utawala wa Allah, na si kanuni hizo kutawala irada yake Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kufupika na kurefuka kwa usiku na mchana au kuingia na kutoka kidogo kidogo kila kimoja kati ya viwili hivyo hakutokei kwa bahati na sadfa tu bali ni dhihirisho la kuwa na lengo uumbaji pamoja na nidhamu maalumu inayotawala juu yake. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba mfumo wa ulimwengu ikiwemo mwendo wa mwezi na jua umewekewa ratiba na muda maalumu; na kila kitu kinafuata njia yake kulingana na makadirio maalumu kilichowekewa. Vilevile aya hii inatutaka tumwabudu na kumuomba Mungu aliye Muweza mutlaki, si kuwaendea watu na vitu ambavyo havina uwezo wa kujisimamia wenyewe seuze kuweza kuwafanyia kitu wenginewe. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 778 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuwa washukurivu wa neema zake, kubwa na ndogo, tunazozijua na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags

Maoni