Mar 25, 2018 07:56 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 779 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 14 ambayo inasema:

إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖوَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ

Mkiwaomba hawasikii maombi yenu; na hata wakisikia hawakujibuni. Na Siku ya Kiyama watakataa shirki yenu. Na hapana atakaye kupa khabari vilivyo kama Yeye Mwenye khabari.

Aya tuliyosoma katika darsa iliyopita ilieleza kwamba washirikina wanawaomba watu na vitu ambavyo havina uwezo wala mamlaka yoyote juu ya ulimwengu huu. Aya hii tuliyosoma inaendeleza maudhui hiyo kwa kueleza kwamba, wao wanaviomba vitu ambavyo havina uwezo wa kusikia wala kujibu vinayosemezwa. Ni masanamu ya mawe na miti ambayo hayana masikio, ndimi wala uwezo wa kuelewa na kufahamu jambo. Waabudiwa hao bandia sio tu hapa duniani hawana uwezo wa kukufanyieni chochote, lakini huko akhera pia, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, watawezeshwa kunena, ambapo watasema na kuzungumza dhidi yenu kwa namna ya kubainisha kwamba nyinyi washirikina, kiukweli hamkuwa mkituabudu sisi, isipokuwa mlikuwa mkiabudu dhana, hawaa na matamanio ya nafsi zenu. Japokuwa kidhahiri mlikuwa mkitunyenyekea na kuonyesha taadhima mbele yetu, lakini ukweli ni kwamba mliyafanya yale kwa ajili ya kupata matilaba na matakwa ya nafsi zenu. Kisha sehemu ya mwisho ya aya inaeleza kwamba: ni Allah SW peke yake ndiye Mjuzi na Mwelewa wa matukio hayo yatakayojiri Siku ya Kiyama; na Yeye anakupa wewe habari kupitia Kitabu chake ili usije ukamshirikisha na kupotoka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba utashi wa mtu wa kuathiriwa na hisia na dhana hufikia kiwango mpaka akaamua kuabudu vitu bubu, vipofu na visivyo na uhai wala hisia yoyote, na kumwacha Mwenyezi Mungu aliyemuumba yeye, mwenye kuona na mwenye kusikia! Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa shirki haimletei mtu faida yoyote; si hapa duniani wala si huko akhera. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba ghairi ya Mwenyezi Mungu, mwengine yeyote au kingine chochote kile tunachokiabudu kitakuja kutukataa, kujitenga nasi na kutushtaki Siku ya Kiyama. Wa aidha aya hii inatutaka tujue kwamba hatuwezi kujua kitu chochote kuhusu Kiyama isipokuwa kupitia wahyi na kitabu cha mbinguni.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 15, 16 na 17 ambazo zinasema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ

Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha, Msifiwa.

 إِن يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ وَيَأْتِ بِخَلْقٍ جَدِيدٍ

Akitaka atakuondoeni na alete viumbe wapya.

 وَمَا ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ بِعَزِيزٍ

Na hilo si gumu kwa Mwenyezi Mungu. 

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kuhusu tauhidi na kumpwekesha Allah na kueleza kwamba: msidhani kama Allah alipokuamrisheni musali na kumwomba Yeye ni kwa sababu ya kuhitaji ibada zenu. La hasha! Yeye si mhitaji wa chochote kwenu, lakini ni nyinyi ndio mnaomhitajia Yeye kwa kila hali. Ule wakati nyinyi mlipokuwa hamjaumbwa na kuja duniani Yeye alikuwepo tayari; na pale nyinyi nyote mtakapoondoka, Yeye Mola ataendelea kuwepo. Yeye si mhitaji wa uwepo wenu seuze awe na haja ya sala, dua na ibada zenu nyengine. Kama anakuamuruni musali, ni kwa ajili ya kuweza kuwasiliana na Yeye na kutaaradhia kwake Yeye shida zenu na mahitaji yenu, si kwa wengineo. Kwa kutoa mfano, ikiwa mwalimu anampa mwanafunzi kazi ya masomo, haimaanishi kwamba yeye mwalimu ni mhitaji kwa mwanafunzi. Hiyo ni alama ya tadbiri na uchungu alionao mwalimu huyo wa kutaka mwanafunzi wake ajengeke kielimu. Sala ni kitu kinachotujenga kiroho na kimaanawi sisi wanadamu; na Yeye Mola aliyetuumba anatupenda sisi waja wake. Yeye Allah hataki sisi tuishie kwenye dunia ya kimaada na ya uhayawani, lakini anataka tujengeke na kufikia daraja za juu za kiutu. Ni kwa sababu hiyo ametufaradhishia Sala na ibada nyenginezo. Kwa hakika sisi wanadamu tunahitajia rehma zake, si kwa ajili ya asili ya ujudi wetu tu lakini kwa ajili ya hata kubakia kwetu hapa duniani. Sababu ni kuwa sisi ni wakosefu na wahitaji wa kila kitu na wala hatuna chochote kinachotokana na sisi wenyewe cha kuweza kubaki nacho. Dhati yetu sisi ni wahitaji, na dhati yake Allah SW ni mkwasi na asiyehitaji chochote. Yeye yupo kwa dhati yake mwenyewe, na sisi tupo kutokana na dhati yake Yeye. Kwa hivyo ni Yeye tu ndiye anayestahiki kutukuzwa na kuhimidiwa; na kumwabudu kwetu sisi wanadamu hakumuongezei chochote, ila ni sisi ndio tunaoneemeka na kufaidika kwa mwangwi wa nuru yake tukufu. Mtu yeyote anayeamua kujenga nyumba yake mahali penye kizuizi cha kuangaziwa na mwanga wa jua huwa halidhuru jua kwa kufanya hivyo isipokuwa huwa anajikosesha mwenyewe neema ya mwanga huo. Kama ambavyo yule anayefungua dirisha lake na kuruhusu mwanga wa jua uingie ndani huwa ananufaika na mwanga huo wenye faida nyingi pasi na yeye kulinufaisha jua kwa chochote. Kisha aya zinaendelea kuashiria moja ya sababu za ukwasi wa Allah na uhitaji wa mwanadamu kwa kusema: Ikiwa Yeye Mola atataka, ni muweza wa kukuondoeni nyinyi watu wote katika uso wa dunia na badala yake akaleta watu au viumbe wengine; na hilo si jambo gumu wala lenye uzito wowote kwake Yeye. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wito wa Allah wa kututaka tumwabudu Yeye peke yake, haumaanishi kuwa Yeye ni mhitaji kwetu sisi, bali ni alama ya uhitaji wetu kwa kimbilio na hifadhi imara na ya uhakika. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ikiwa mwanadamu atajihisi si mhitaji, atatakabari mbele ya Mwenyezi Mungu na hatokuwa tayari kunyenyekea kwa Mola. Ndiyo maana Qur'ani inatilia mkazo sifa ya uhitaji aliyonayo mwanadamu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba watu matajiri huwa wanakabiliwa na husuda au ushindani wa matajiri wenzao, kwa hivyo kwa kawaida huwa hawapendezi kwa watu. Lakini Allah SW ni mkwasi na mhimidiwa; na kinyume na akthari ya wenye ukwasi, ukwasi na utajiri wake Yeye anautumia kukidhi mahitaji ya viumbe wake; kwa sababu hiyo muda wote huwa anahimidiwa na kushukuriwa. Vilevile kutokana na aya hizi inatupasa tujue kwamba Mwenyezi Mungu anaweza wakati wowote kufanya mabadiliko katika uumbaji wake; na hakuna mkwamo wowote katika uwezo mutlaki wa Mola. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 779 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, azitakase na shirki na upotofu nyoyo zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags

Maoni