Mar 25, 2018 08:04 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 780 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 18 ambayo inasema:

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ وَإِن تَدْعُ مُثْقَلَةٌ إِلَىٰ حِمْلِهَا لَا يُحْمَلْ مِنْهُ شَيْءٌ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۗ إِنَّمَا تُنذِرُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالْغَيْبِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ ۚ وَمَن تَزَكَّىٰ فَإِنَّمَا يَتَزَكَّىٰ لِنَفْسِهِ ۚ وَإِلَى اللَّـهِ الْمَصِيرُ

Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine. Na kama aliyeelemewa akiomba achukuliwe mzigo wake, hautachukuliwa hata kidogo, ingawa ana ujamaa. Hakika wewe unawaonya wale tu wamchao Mola wao Mlezi kwa ghaibu, na wakasimamisha Sala. Na anaye jitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.

Aya hii inaashiria moja ya misingi ya itikadi za Waislamu ambao ni uadilifu wa Mwenyezi Mungu SW na kueleza kwamba: Siku ya Kiyama kipimo kitakachotumika kutoa malipo ya thawabu au adhabu na ikabu ni amali na matendo ya mtu mwenyewe, na hakuna mtu yeyote ambaye atabeba mzigo wa dhambi za mtu mwengine kutokana na uhusiano wa kidunia aliokuwa nao na mtu huyo kama urafiki, ujamaa na nasaba. Na katika kuhesabu amali za waja, Allah SW yeye pia hatombebesha mtu mzigo wa dhambi za mtu mwengine. Kila mtu siku hiyo atapaswa kuwajibika na kutoa majibu kwa amali zake.  Mtu yeyote yule hatoweza kujivua na mzigo wa madhambi na maovu aliyofanya kwa kuibebesha lawama ya taksiri jamii na mazingira aliyoishi. Lakini ni wazi pia kwamba ikiwa mtu aliwachochea watu kufanya dhambi, atakuwa mshirika katika adhabu watakayopewa watu hao kulingana na kiwango cha dhambi walizofanya kwa ushawishi wake. Ni sawa na mtu anayewashajiisha na kuwalingania watu kufanya mema, ambaye naye pia atakuwa mshirika wao katika jaza na thawabu watakazopata kwa kufanya wema huo. Kisha aya inaendelea kwa kutaja chanzo hasa cha ufanyaji madhambi, yaani uchafu wa kiroho na kueleza kwamba: watu pekee wanaosikiliza maneno ya haki na kujiweka mbali na maovu na machafu ni wale wenye moyo na kiu ya kuijua na kuifuata haki na kutaka kuzitakasa na kuzisafisha roho zao. Vinginevyo mtu asiye tayari kuikubali haki, hatoathiriwa na kuzinduka kwa maneno hata ya Mtume pia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Siku ya Kiyama madhambi yatakuwa mzigo mzito utakaomuelemea mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, katika dunia hii tusihadaiwe na watu wanaotulaghai na kutushawishi kufanya madhambi kwa kutuambia: msiogope kitu, kama kutakuwa adhabu, sisi tutabeba mzigo wa madhambi yenu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kila mtu anabeba dhima ya madhambi yake na hakuna yeyote miongoni mwetu atakayeadhibiwa kwa dhambi ya mtu mwengine. Lakini kama hatutatekeleza wajibu wetu wa kukataza maovu na kutowakanya watu wasifanye madhambi na machafu, nasi pia tutaadhibiwa kwa wanayoyafanya kwa sababu ya kuyanyamazia kimya. Vilevile aya hii inatutaka tuelewe kuwa Siku ya Kiyama kila mtu atatingwa na kushughulishwa na daftari la amali zake, wala hatoweza kufanya chochote kile kuwasaidia wenzake hata kama watakuwa jamaa zake wa karibu kabisa.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 19 hadi ya 21 ambazo zinasema:

وَمَا يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ

Na hawi sawa kipofu na mwenye kuona.

وَلَا الظُّلُمَاتُ وَلَا النُّورُ

Wala giza na mwangaza.

وَلَا الظِّلُّ وَلَا الْحَرُورُ

Wala kivuli na joto.

Aya hizi zimetumia mbinu ya ufananishaji na umithilishaji kuwalinganisha waumini na makafiri kwa kuhoji: Hivi kwa mtazamo wenu nyinyi, mtu kipofu na asiyeona chochote yuko sawa na mtu mwenye macho mazima aonaye kila kitu? Ni dhahiri kwamba hawako sawa; na utambuzi wao juu ya hakika za ulimwengu huu unatafautiana. Kwa sababu mmoja wao hahisi kingine chochote kile zaidi ya kiza, wakati mwenzake anaweza kukiona kila kitu kupitia nuru ya mwangaza. Ni kama kwamba mmoja huwa muda wote anaishi penye kivuli kisicho na mwanga, na mwengine anaangaziwa muda wote na mwangaza wa jua. Bila shaka kuona na kutoweza kuona ni mambo mawili yanayohusiana na uumbwaji, ambapo katika hilo viumbe hawana nafasi yoyote ile. Lakini imani na ukafiri ni mambo ya hiyari na ya kujichagulia mtu mwenyewe. Kila mtu anaweza kuamua kufuata njia ya ukafiri; na matokeo yake yakawa ni kutopea kwenye giza la kufru na kuikosesha nafsi yake kuona hakika za kimaanawi na kighaibu; au kinyume chake akaifuata nuru ya imani itakayomwezesha kuona haki na kuufikia uongofu utokao kwa Allah. Kuna aya nyengine kadhaa za Qur’ani tukufu zinazotilia mkazo suala hili kwa kueleza kwamba, Mwenyezi Mungu SW amewatuma Mitume wake na vitabu vya mbinguni ili kuwatoa watu kwenye viza na kuwaelekeza kwenye nuru ya uongofu huku viongozi wa ukafiri na utaghuti wakifanya kila njia kuwatoa watu kwenye nuru na kuwazamisha kwenye lindi la viza vya dhalala na upotofu. Katika ulimwengu wa maumbile, maisha ya viumbe hai kuanzia mimea, wanyama na watu yanategemea mwanga na joto la jua; na endapo mwanga na joto hilo la jua havitofika ardhini na sayari hii ikagubikwa na giza, viumbe vyote vitakufa na kutoweka. Hayo yakiwa ni mahitaji ya kimaada; kwa upande wa kimaanawi roho ya mwanadamu iko vivyo hivyo pia, yaani uhai wa roho ya mwanadamu unategemea mwanga wa nuru ya Allah; nuru ambayo inapatikana kwa njia ya akili na fitra, yaani maumbile ya ndani ya mwanadamu na wito wa nje anaofikishiwa na Manabii wa Allah. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kwa kulinganisha kati ya mazuri na mabaya au baina ya maisha ya waumini wafanya mema na makafiri watenda mabaya tutaweza kupambanua kati ya njia sahihi na ya upotofu na kujiepusha na hatari ya shirki na ukafiri. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dini inampa mwanadamu uono mpana wa basira na mwanga wa uongofu ili aweze kujikomboa na kujitoa kwenye viza vya dhalala na upotofu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kutokana na kutajwa nuru katika hali ya umoja na giza katika hali ya wingi yaani viza, hii inamaanisha kwamba hakuna njia zaidi ya moja ya haki, lakini njia za upotofu na batili ni nyingi mno. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 780 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atuwafikishe kuifuata, na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags

Maoni