Mar 25, 2018 08:10 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 781 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 22 na 23 ambazo zinasema:

وَمَا يَسْتَوِي الْأَحْيَاءُ وَلَا الْأَمْوَاتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُسْمِعُ مَن يَشَاءُ ۖ وَمَا أَنتَ بِمُسْمِعٍ مَّن فِي الْقُبُورِ

Na hawawi sawa walio hai na walio maiti. Hakika Mwenyezi Mungu humsikilizisha amtakaye. Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio makaburini.

إِنْ أَنتَ إِلَّا نَذِيرٌ

Hukuwa wewe ila ni mwonyaji.

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa kwenye aya tulizosoma katika darsa iliyopita kwa kuwafananisha makafiri na wafu na waumini na watu waliohai na kueleza kwamba: nyoyo za makafiri ni mithili ya wafu ambao huwa hawaoni wala hawasikii. Ukafiri ni sawa na nikabu iliyomgubika mtu na kumfanya ashindwe kuona na kusikia hakika za mambo. Ukweli ni kwamba watu wanaoweza kusikia ujumbe na wito wa Mwenyezi Mungu ni wale ambao nyoyo zao zinataka kuisikiliza haki na kuikubali. Lakini kama moyo hauko tayari kuikubali haki, masikio pia hayatokuwa tayari kuisikiliza. Ni sawa na pale mtu unapokuwa umeshughulika kusoma, huku televisheni ikiwa imewashwa. Ikiwa hutozingatia yale yanayoonyeshwa kwenye televisheni, hutoweza kuelewa chochote anachosema mtangazaji japokuwa maneno yote ayasemayo yanapenya na kuingia masikioni mwako. Sababu ni kwamba hukukusudia kuyasikiliza maneno hayo. Vivyo hivyo ndivyo walivyo makafiri, ambao maneno ya haki yanapenya masikioni mwao, lakini kwa kuwa hawana nia ya kuyasikiliza na kuyakubali huwa utadhani hawajayasikia wala hawajayafahamu asilani maneno hayo. Kisha aya zinaendelea kwa kumhutubu Bwana Mtume SAW ya kwamba: kazi na jukumu ulilopewa wewe ni kuonya na kutoa indhari; na mtu atakayezingatia maonyo hayo ni yule mwenye sikio la kusikia, si yule aliye mfano wa asiyesikia wala asiyeweza kuona. Kwa hivyo maneno yako wewe Mtume hata yawe na fasaha na mantiki kiasi gani, maadamu mtu hataki kuyasikiliza na kuyaelewa hayatokuwa na athari yoyote kwake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba imani humpa uhai na kumjenga mtu pamoja na jamii, kama ambavyo kufru huwa sababu ya kuporomoka mtu na jamii na kuwa mithili ya mfu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tablighi ya dini na kuwalingania watu wito wa tauhidi ni jambo la dharura; lakini kama watu wenyewe hawatokuwa na utayarifu unaotakiwa, isitarajiwe kwamba wataathirika na kuikubali haki. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kukufuru na kuipa mgongo haki kunakofanywa na watu kusitukatishe tamaa na kutuvunja moyo au kututia shaka na hatihati juu ya njia ya haki tunayofuata.

Ifuatayo sasa ni aya ya 24 ambayo inasema:

إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ بِالْحَقِّ بَشِيرًا وَنَذِيرًا ۚ وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ

Hakika Sisi tumekutuma wewe kwa Haki, uwe mbashiri na mwonyaji. Na hakuna umma wowote ila ulipata mwonyaji kati yao.

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kuhusu waumini na makafiri kwa kuashiria ujumbe asili wa Mitume na kueleza kwamba: kuwaongoza na kuwaelekeza watu kwenye uongofu, kuwapa bishara watenda mema na kuwapa indhari wafanyao mabaya lilikuwa jukumu la Mitume wote wa Allah. Kwanza walikuwa wakiwaonyesha watu njia yenyewe, kisha wakawashajiisha kufanya mema na kuwatahadharisha na mabaya kwa kubainishia adhabu na thawabu watakazopata duniani na akhera kutokana na matendo watakayofanya. Mbali na Mitume kufundisha mafundisho ya hukumu za dini walikuwa wakizilea pia nyoyo za watu na kutumia wenzo wa ushajiishaji na ukemeaji, kama alivyo mlezi na mwalimu mwenye uchungu na wanafunzi wake. Kwa vile wahutubiwa wengine wa Bwana Mtume SAW walikuwa watu wenye umimi, wakaidi na wenye taasubi, aya zilizotangulia na hii ya 24 imetilia mkazo zaidi mbinu ya uonyaji na utoaji indhari kwa kusema: ili kuwataka watu waache fikra na mienendo yao potofu, Mwenyezi Mungu Mtukufu amekuwa kila mara akiwatuma Mitume na mawalii wake wawaonye na kuwapa indhari watu juu ya matokeo ya amali zao na kuwahofisha juu ya mwisho na hatima mbaya inayowakabili. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kushajiisha na kukemea, na kuhofisha na kupa matumaini ni mambo yanayopasa kufanyika kwa pamoja. Kila moja peke yake bila ya mwenzake huwa lina kasoro na huifanya kazi ya malezi na kumjenga mtu kimaanawi iwe na walakini na upungufu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa jamii inayopatwa na mghafala inahitaji zaidi maonyo na ukumbusho kuliko kupewa matumaini na bishara njema. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Mwenyezi Mungu hajawahi hata mara moja kuiacha dunia bila ya kuwepo mja wa kutimiza dhima na hoja za kufikisha wito wa haki kwa watu, bali daima walii katika mawalii wa Allah huwepo miongoni mwa watu kwa ajili ya kufikisha wito wa Mwenyezi Mungu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 25 na 26 ambazo zinasema:

وَإِن يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ وَبِالزُّبُرِ وَبِالْكِتَابِ الْمُنِيرِ

Na kama wakikukadhibisha, basi walikwisha kadhibisha wale walio kuwa kabla yao. Mitume wao waliwajia kwa dalili wazi wazi na kwa maandiko na Kitabu chenye nuru.

ثُمَّ أَخَذْتُ الَّذِينَ كَفَرُوا ۖ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ

Kisha nikawakamata walio kufuru. Basi kulikuwaje kukanya kwangu?

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia na kumhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba: ikiwa washirikina wa Makka hawaukubali wito wako na wanaukadhibisha ujumbe uliowafikishia, hilo lisikustaajabishe wala kukutia wasiwasi. Kwa sababu katika kila zama za historia watu wengi wamesimama kukabiliana na Mitume kutokana na ujahili na taasubi, pamoja na kwamba Mitume hao wa Allah walikuwa na miujiza na pia walikuwa na hoja na mantiki za wazi kabisa. Baadhi ya Mitume walikuwa na Vitabu vya mbinguni pia, na walikuja na mfumo wa sharia na wakawabainishia watu mafundisho na hukumu za Mwenyezi Mungu. Hata hivyo kutokana na inadi na ukaidi wao, watu hao ambao waliamua kukabiliana na haki, walifikwa na misukosuko hapa duniani na kupatwa na adhabu ya Mola ili hatima yao iwe somo, ibra na mazingatio kwa wengine. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba uzungumzaji wa Mitume ulikuwa wadhiha na wa ufasaha na waliwalingania watu wito wa Allah kwa hoja na mantiki, si kwa kuwatolea porojo na mambo ya khurafa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mtu huwa anajiandalia mazingira ya kushukiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kuikana haki baada ya kuifahamu na kuielewa. Aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba adhabu ya Allah haihusiani na akhera tu. Wakati mwengine ghadhabu na adhabu yake Mola hudhihiri hata hapa duniani pia. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 781 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya Moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags

Maoni