Mar 25, 2018 08:24 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 782 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 27 na 28 ambazo zinasema:

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ ثَمَرَاتٍ مُّخْتَلِفًا أَلْوَانُهَا ۚ وَمِنَ الْجِبَالِ جُدَدٌ بِيضٌ وَحُمْرٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهَا وَغَرَابِيبُ سُودٌ

Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo tumetoa matunda yenye rangi mbali mbali. Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbali mbali, na myeusi sana.

وَمِنَ النَّاسِ وَالدَّوَابِّ وَالْأَنْعَامِ مُخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ كَذَٰلِكَ ۗ إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ

Na katika watu, na wanyama, na mifugo, pia rangi zao zinakhitalifiana. Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye maghufira.

Aya hizi kama zilivyo aya za mwanzoni mwa sura hii zinaashiria alama mbalimbali za qudra, uwezo na upekee wa Allah SW na kueleza kwamba: Anuai za vitu visivyo na uhai, mimea, wanyama na watu zina rangi, sura na hali namna tofauti; na tofauti hizo zinatoa taswira na picha ya kuvutia na kupendeza ya ulimwengu wa maumbile. Wachoraji waliobobea zaidi duniani, kazi zao bora za uchoraji ni za mandhari za maumbile, ambazo hujitahidi kuzichora ili zionekane mithili ya mandhari halisi za maumbile pasina mtu kuweza kutafautisha kati ya picha ya mchoro na taswira halisi ya mandhari ya maumbile. Au hata mchoraji wa picha za watu, naye pia hujitahidi kuhakikisha anachora picha ya mtu itakayomfanya mtazamaji adhani na kuhisi kwamba athari hiyo ya mchoro ni ya picha halisi ya mtu iliyopigwa kwa kutumia kamera. Kwa maneno mengine ni kwamba, Mwenyezi Mungu ameuumba ulimwengu wa maumbile na mwanadamu kwa namna nzuri na ya kupendeza mno, kiasi kwamba katika kufikia kilele cha sanaa yake, mwanadamu hujitahidi kuhakikisha kazi inayofanywa na kalamu yake ya uchoraji inatoa picha na taswira inayofanana zaidi na ya mandhari halisi ya maumbile. Lakini mbali na anuai za rangi tofauti tofuati zilizoko kwenye mandhari za maumbile, ambazo zenyewe ni upeo wa juu wa utaalamu wa uumbaji, rangi mbalimbali na ladha tofauti za aina kwa aina za matunda pamoja na mazao ya mashambani na mabustanini, ambayo yote hayo yanastawishwa kwa maji ya aina moja, nao pia ni muujiza mwengine wa uumbaji wa Allah SW. Maji ya mvua, ambayo hayana rangi wala ladha maalumu, wakati yanapopenya kwenye mti na mmea kupitia mizizi na shina na kufikia kwenye matawi hadi maua humtunukia mwanadamu matunda na mazao ya rangi na ladha aina mbalimbali. Kisha aya zinaendelea kuashiria mas-ulia na jukumu kubwa walilonalo wanazuoni na maulamaa kwa kueleza kwamba: wao, ambao ni watu wanaoelewa adhama ya uumbaji na kuutambua uwezo usio na kikomo wa Allah SW huwa wanyenyekevu mbele ya adhama hiyo; na daima huwa na hofu juu ya taksiri na kushindwa kwao kutekeleza ipasavyo majukumu yao mbele ya Mola wao. Elimu na uelewa juu ya adhama ya ulimwengu wa maumbile humfanya mtu awe na khushuu na unyenyekevu mbele ya Muumba wa ulimwengu huo, ambapo athari ndogo kabisa ya unyenyekevu huo ni hofu ya kuwa na taksiri katika kutekeleza jukumu na wajibu wake mbele ya Mola wake. Bila ya shaka elimu iliyokusudiwa hapa si ya ugunduzi wa fomyula za fizikia, kemia na biolojia; kwa sababu fomyula hizo peke yake haziwezi kuwa na taathira hiyo ndani ya nafsi ya mwanadamu; lakini kama ilivyoashiriwa katika Hadithi, elimu inayomjaza mtu hofu iliyokusudiwa hapa ni ile ambayo kupitia maumbile ya kimaada humfikisha kwa Mola wake Muumba, ikaifanya imara zaidi imani yake hadi kufikia daraja ya yakini. Madhumuni ya elimu iliyokusudiwa katika aya tuliyosoma, ni kuwa na uelewa na uono mpana unaoifanya imani ya mtu kwa Muumba wa ulimwengu iwe imara zaidi. Kwa hivyo hata kama mtu atakuwa ametabahari katika elimu mbalimbali, lakini kama hatokuwa na uelewa wowote kuhusu adhama ya Mola, malengo ya kuumbwa kwake, hatima ya mwanadamu Siku ya Kiyama na mfano wa hayo, mtu huyo atakuwa kwenye kundi la wajinga. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba miongoni mwa ishara za qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu ni kwamba, kutokana na maji na udongo wa aina moja anatoa mazao na matunda ya aina mbalimbali yenye ladha na rangi tofauti. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dini haipingi jamali na uzuri. Allah SW mwenyewe ni mwanzishaji na muumbaji wa kila aina ya uzuri na jamali. Ameziumba mandhari nzuri kabisa za kupendeza na kuvutia katika milima, misitu na bahari na kuzitaja kuwa ni ishara za kuwepo kwake. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kuwepo kwa watu wa rangi mbalimbali ni katika ishara za qudra na adhama ya Allah SW, si sababu ya watu kujikweza au baadhi yao kujivuna na kujifaharisha mbele ya wengine. Vilevile tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba kuwa na elimu na ujuzi juu ya siri za ulimwengu inapasa kumfikishe mtu kwenye daraja ya kumhofu Mola wake. Mambo hayo si sababu za kumtia mtu ghururi, kiburi na majivuno.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 29 na 30 ambazo zinasema:

إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّـهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ

Hakika wale wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakasimamisha Sala, na wakatoa kwa siri na kwa dhaahiri katika tulivyo waruzuku, hao wanataraji biashara isiyo bwaga.

لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ

Ili Yeye awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie kutokana na fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye shukrani.

Baada ya aya zilizotangulia kuashiria hofu na unyenyekevu walionao wanazuoni na maulamaa kwa Mwenyezi Mungu mtukufu, aya hizi zinaeleza kwamba: hofu juu ya Allah huambatana na matumaini ya kupata rehma zake pia; matumaini ambayo huwa sababu ya kughufiriwa madhambi na kupata malipo ya thawabu. Ni wazi kwamba kuwa na matarajio matupu bila ya amali na matendo ni japo la kipuuzi ambalo haliendani na hekima ya Mola Muumba. Kwa sababu hiyo, aya hizi zinasema: watu wanaoweza kuwa na matumaini ya kupata rehma za Allah SW duniani na akhera ni wale wafanyaji wa amali na matendo mema. Wao wanajenga mawasiliano na Mola wao kwa kusoma Qur'ani na kusimamisha Sala, na wanafanya hivyo pia na waja wa Mwenyezi Mungu kwa kutoa mali zao kuwasaidia wahitaji katika jamii na kuwafikiria wanyonge. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, elimu na utaalamu peke yake hautoshi; inalazimu viambatane na dua na ibada. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, biashara ya kudumu na yenye faida kubwa ni ile ambayo mtaji na rasilimali yake tunaitumia katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuwasaidia watu. Rasilimali hiyo inaweza kuwa umri, elimu, mali, heshima na kila tulichonacho. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Sala bila ya utoaji, na utoaji mali tu bila ya kusimamisha Sala hauwezi kuwa na tija. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba, kama tunaitakidi kuwa kila tulichonacho kimetokana na Mwenyezi Mungu hatuwezi kuwa na ubakhili wa kukitoa wala hatutohisi kuwa tunapata hasara kwa kutoa kuwasaidia wengine. Aya hizi vilevile zinatutaka tuelewe kwamba, kuwa na matumaini ya kufuzu na kuokoka Siku ya Kiyama kunapasa kuambatane na amali na matendo mema, vinginevyo kutabaki kuwa ndoto na matarajio matupu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 782 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags

Maoni