Mar 25, 2018 08:30 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 783 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 31 na 32 ambazo zinasema:

وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ هُوَ الْحَقُّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِعِبَادِهِ لَخَبِيرٌ بَصِيرٌ

Na hayo tuliyo kufunulia kutoka Kitabuni ni haki yenye kusadikisha yaliyo kuwa kabla yake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni Mwenye khabari, Mwenye kuona.

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ

Kisha tumewarithisha Kitabu hao ambao tumewateua miongoni mwa waja wetu. Kati yao yupo aliye jidhulumu nafsi yake, na yupo wa katikati, na yupo aliyetangulia katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kuu.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyozungumzia kukisoma Kitabu cha mbinguni cha Qur’ani na kutekeleza maamrisho yaliyomo ndani yake. Aya hizi tulizosoma zinasema: yale yaliyoteremeshwa moyoni mwa Bwana Mtume SAW kwa sura ya Qur’ani ni maneno ya haki, kwa sababu chimbuko na asili yake ni haki, yaani ni wahyi uliotoka kwa Allah SW unaowiyana pia na akili na fitra, yaani maumbile ya batini ya mwanadamu. Isitoshe, Qur’ani inaafikiana na kuwiyana na vitabu vya Mitume waliotangulia na inawasadikisha Mitume hao na Vitabu walivyoteremshiwa; na kuwaamini wao ni sehemu ya sharti la kumwamini Mwenyezi Mungu. Kisha aya zinaendelea kwa kueleza kwamba: umma wote wa Kiislamu, ambao ni umma mteule miongoni mwa umma nyinginezo kutokana na kumwamini Allah SW na Bwana Mtume Muhammad SAW, ni mrithi wa Qur’ani na unapaswa ufanye jitihada za kuifahamu, kuitekeleza na kuitangaza kwa wengine. Lakini kwa masikitiko ni kwamba, kundi miongoni mwa watu wa umma huu wamejidhulumu nafsi zao na kujitenga na Qur’ani, kundi jengine linaifuata, na kuna kundi liko mstari wa mbele katika kuitekeleza na kuitangaza katika jamii. Kwa mujibu wa Hadithi, Ahlul Bayt wa Bwana Mtume SAW ambao ni makhalifa wa mtukufu huyo ndio hao walio mstari wa mbele katika kuitekeleza na kuitangaza Qur’ani katika jamii na ndio Maimamu na viongozi wa watu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ndani ya Qur’ani tukufu hamna neno lolote la batili, la porojo au la khurafa, bali aya zake zote zina msingi wa haki, hakika na ukweli. Kwa hivyo iko makini na thabiti. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Vitabu vya mbinguni na Manabii wote wa Allah wana lengo na muelekeo mmoja. Na ndiyo maana kila mmoja ni mwenye kuthibitisha na kusadikisha yaliyoletwa na Nabii mwenzake aliyemtangulia. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kwa kujiweka mbali na Qur’ani na mafundisho yake, mtu anaidhulumu nafsi yake mwenyewe, si kumdhulumu Mwenyezi Mungu wala Mtume wake. Aya hizi zinatutaka pia tuelewe kuwa warithi halisi wa elimu za Qur’ani ni wale wanaoshindana kuwa wa mbele katika kheri. Kwa maneno mengine ni kwamba, sharti la kupokea urithi wa Qur’ani ni kuwa wa mbele katika kufanya mema na kufikisha mambo ya kheri kwa wengine.

Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 33 hadi ya 35 ambazo zinasema:

جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَلُؤْلُؤًا ۖ وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ

Mabustani ya milele watayaingia. Humo watavikwa vikuku vya dhahabu, na lulu, na nguo zao humo ni za hariri.

وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَذْهَبَ عَنَّا الْحَزَنَ ۖ إِنَّ رَبَّنَا لَغَفُورٌ شَكُورٌ

Na watasema: Alhamdulillahi, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye tuondolea huzuni zote. Hakika Mola wetu Mlezi ni Mwingi wa maghufira, Mwenye shukrani.

الَّذِي أَحَلَّنَا دَارَ الْمُقَامَةِ مِن فَضْلِهِ لَا يَمَسُّنَا فِيهَا نَصَبٌ وَلَا يَمَسُّنَا فِيهَا لُغُوبٌ

Ambaye kwa fadhila yake ametuweka makao ya kukaa daima; humu haitugusi taabu wala humu hakutugusi kuchoka.

Aya zilizotangulia zimeugawa umma wa Kiislamu katika makundi matatu, ambayo ni ya waliojidhulumu, wafuataji na maimamu au walio wa mbele. Aya hizi tulizosoma zinatoa ahadi ya malipo mema kwa kundi la pili na la tatu kati ya makundi hayo. Malipo ambayo yatathibiti Siku ya Kiyama kwa kupatiwa makao ya milele kwenye Pepo iliyoahidiwa na Mola. Hapo sio tu ni pahala pazuri kabisa na penye kuuburudisha moyo, lakini ndani yake pia mtu atasuhubiana na watu wazuri na waliopendeza kimavazi kiasi cha kuifanya nafsi yake isiwe na ghamu wala huzuni yoyote. Ni wazi kwamba katika mazingira kama hayo, hakuwezi kuwepo na kitu cha kumtia mtu simanzi wala kumfanya aone dhiki au tabu yoyote. Hapa duniani kuna mambo mawili yanayomtia mtu simanzi na kumfanya awe na msongo wa mawazo. Moja, ni kuwa na neema na raha zinazojikariri hizo kwa hizo; na jengine ni hofu ya kuondokewa na neema na raha hizo. Lakini huko akhera kuna chungu na anuai za neema kiasi kwamba hazitouchosha moyo wa mtu wala kumfanya awe na hofu ya kuondokewa nazo. Wakati watu wa Peponi watakapopatiwa makazi hayo na kupata watu wazuri kama hao wa kusuhubiana nao watamhimidi na kumshukuru Mola wao, wakijua kwa yakini kwamba Pepo waliyoipata ni fadhila waliyofanyiwa na Mola na si malipo halisi ya amali zenye mpaka maalumu walizofanya hapa duniani; kwa sababu Yeye Allah amewatunukia Pepo hiyo kwa kuwaghufiria madhambi yao na kuyasitiri makosa yao; na lau kama asingewasamehe na kuwafanyia wema huo isingepatikana njia ya wao kuipata neema hiyo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wale ambao hapa duniani walizinyima nafsi zao baadhi ya raha za kupita kwa ajili ya kupata radhi za Allah SW, huko akhera Yeye Mola atawafidia hayo waliyojinyima kwa neema na raha za milele. Mfano wake ni dhahabu na hariri, ambazo wameharamishiwa wanaume hapa duniani lakini watatumia na kuneemeka nazo huko Peponi. Allah atujaalie kuwa miongoni mwa hao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Peponi kuna raha za kuburudisha mwili na kuipa utulivu roho na akili ya mtu. Ni kinyume na hapa duniani, ambapo watu wengi wenye nguvu za madaraka na utajiri wa mali wana kila aina ya raha za kimaada na kimwili lakini hawapati utulivu wa nafsi na akili. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Mwenyezi Mungu ni msamehevu kwa makosa tunayoyafanya; na mshukurivu na mthamini wa mema tunayoyatenda. Kwa hivyo na sisi waja wake pia tujitahidi kupambika na sifa hizo tukufu za Mola wetu. Aidha tunabainikiwa kutokana na aya hizi kuwa watu wa Peponi watajua kwamba kuwako kwao huko kumetokana na fadhila na ukarimu wa Allah, si amali zao njema walizofanya; kwa sababu neema za milele zisizo na mfano na zisizo hesabika za akhera haziwezi kulingana katu na amali njema zenye mpaka maalumu walizofanya hapa duniani. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 783 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake atakaowarithisha Pepo yake ya milele na atuepushe na adhabu ya Moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags

Maoni