Mar 25, 2018 08:36 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 784 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Darsa yetu ya leo itazungumzia aya ya 36, 37 na 38 za sura hiyo ambazo zinasema:

وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ نَارُ جَهَنَّمَ لَا يُقْضَىٰ عَلَيْهِمْ فَيَمُوتُوا وَلَا يُخَفَّفُ عَنْهُم مِّنْ عَذَابِهَا ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي كُلَّ كَفُورٍ

Na wale walio kufuru watakuwa na Moto wa Jahannamu, hawahukumiwi wakafa, wala hawatapunguziwa adhabu yake. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila mwenye kuzidi ukafiri. 

وَهُمْ يَصْطَرِخُونَ فِيهَا رَبَّنَا أَخْرِجْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا غَيْرَ الَّذِي كُنَّا نَعْمَلُ ۚ أَوَلَمْ نُعَمِّرْكُم مَّا يَتَذَكَّرُ فِيهِ مَن تَذَكَّرَ وَجَاءَكُمُ النَّذِيرُ ۖ فَذُوقُوا فَمَا لِلظَّالِمِينَ مِن نَّصِيرٍ

Na humo watapiga makelele: Mola wetu Mlezi! Tutoe tufanye mema sio yale tuliyo kuwa tukiyafanya. Kwani hatukukupeni umri wa kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka? Na akakujieni Mwonyaji? Basi onjeni! Kwani walio dhulumu hawana wa kuwanusuru. 

إِنَّ اللَّـهَ عَالِمُ غَيْبِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ

Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa siri za mbinguni na ardhini. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani. 

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia malipo makubwa ya thawabu watakayopata waumini na watenda mema. Aya hizi tulizosoma zinaanza kwa kutaja adhabu kali ya Moto watakayopata makafiri na wakanushaji wa haki. Katika utamaduni na misamiati ya dini, madhumuni ya kafiri ni yule mtu ambaye haki ameitambua kisha akaikanusha; au alikuwa na fursa na uwezo wa kuitambua haki, lakini hakuitumia fursa hiyo kufanya hivyo. Kwa maneno mengine ni kwamba, maana ya ukafiri ni kufunika na kuiziba haki kunakofanywa kwa sababu ya inadi, ubishi na ukaidi au kwa ajili ya kutaka mambo ya kimaada na kukidhi shahawa na matamanio ya nafsi. Ni wazi kwamba mtu anayeikana haki kwa sababu ya manufaa ya binafsi au ya kundi fulani, huwa ameifanyia dhulma nafsi yake na jamii yake, hivyo anastahili kupatwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Sababu ni kwamba Yeye Mola Muumba hakutuumba sisi ili tufanye lolote lile tupendalo na tutakalo. Lakini ametuumba na kututaka tufuate njia ya maisha aliyotuainishia. Hapana shaka kuwa kuikengeuka njia hiyo kutamuelekeza mtu mwenye hilaki na maangamizi. Lakini ili kutimiza dhima kwa wakanushaji wa haki, aya hizi zinasema: Wao wasidhani kuwa, kwa kila wanalolifanya watalipwa kwa kuadhibiwa papa hapa duniani. Kwa sababu kiasili, Mwenyezi Mungu SW ameifanya dunia kuwa uwanja wa amali; kwa hivyo mwanadamu yuko huru hapa kuchagua na kuamua kwa hiyari yake kufanya matendo mema au mabaya. Lakini hakuna wema ufanywao utakaopita vivi hivi, wala dhambi itendwayo itakayoachwa au kusahaulika. Bali hata hapa duniani pia, mwanadamu huonjeshwa baadhi ya wakati mchonyoto wa adhabu kwa maovu anayoyafanya. Lakini malipo hasa na kamili ya adhabu, yako Siku ya Kiyama ambayo haina mpaka wa mahala wala zama, na kila mtu atalipwa thawabu au ikabu kulingana na mema aliyofanya na athari yake, au mabaya aliyotenda na madhara yake. Watenda jinai kama Hitler, Genghis Khan pamoja na watawala madikteta wengineo, ambao kila mmoja katika zama zake amesababisha vifo vya mamia, maelfu bali hata mamilioni ya watu; hata kama wangekamatwa hapa duniani wakashtakiwa na kuhukumiwa wasingeweza kunyongwa zaidi ya mara moja tu.  Lakini aya ya 36 ya sura hii ya Fatir inasema, hakutokuwa na kifo huko akhera; na kila mtu atakuwa adhabuni tu kulingana na maovu aliyoyafanya, hata kama adhabu hiyo itachukua muda wa maelfu ya miaka, Allah atulinde na adhabu yake hiyo isiyoweza kuvumilika.

Wasikilizaji wapenzi wa darsa ya Qur'ani inatupasa tujue kwamba kigezo cha utoaji adhabu wa Allah ni elimu yake mutlaqi na uadilifu wake usio na doa. Kwa hivyo adhabu watakayopewa wafanya maovu haitokuwa kubwa zaidi ya mabaya waliyofanya, wala ndogo kuliko maovu waliyotenda. Watapewa adhabu iliyo haki yao na kwa kiwango wanachostahiki. Kwa hivyo kuhusu kiwango na ukubwa wa adhabu ambayo mtu muovu anastahiki kupewa, hilo linaainishwa kwenye mizani ya elimu mutlaki ya Allah Jalla wa A'laa. Sababu ni kuwa Yeye ni mjuzi wa mambo yote ya mwanadamu na ulimwengu kwa jumla. Anayajua ya dhahiri na ya batini mwa nafsi za watu. Kisha aya zinaashiria ombi la watu waovu la kutaka warejeshwe tena duniani ili wakatende mambo mema kufidia mabaya waliyokuwa wakiyafanya; yawe ni yale waliyoyafanya ilhali wakielewa fika kama ni mabaya au yale waliyokuwa wakidhani kuwa ni mambo mema lakini sasa imewabainikia kwamba yalikuwa maovu. Lakini jawabu watakayopata kutoka kwa Mwenyezi Mungu na walinzi wa Motoni ni ya kuulizwa: je, ule umri wa kuishi mliokuwa mmepewa duniani ulikuwa hautoshi kwa nyinyi kuijua haki na batili na kufanya amali zenu kwa kufuata mizani hiyo? Je, kule duniani Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu hawakukupeni ukumbusho na indhari, kwamba njia mliyochagua kuifuata mwisho wake itakuingizeni Motoni? Na kuna dhamana na uhakika gani kwamba ikiwa mtarejeshwa tena duniani hamtorudia tena kuyafanya yaleyale mliyokuwa mkiyatenda? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ukafiri ni aina mojawapo ya ukanushaji wa neema; kama ambavyo kuzikufuru neema nako pia kunampeleka mtu kwenye ukafiri. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, madhalimu, madikteta, watenda jinai na majabari wote wa dunia iko siku watakuwa wanyonge, hawana hawanani, wenye kutaradhia kwa Mola na kuonyesha majuto kwa dhulma na maovu waliyofanya duniani; lakini majuto yao hayo hayatowafalia kitu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, baada ya kutimiza kikamilifu dhima kwa mhalifu haitupasi tena kumkubalia ombi lake la kufutiwa au kupunguziwa adhabu. La kufanya ni kumpa adhabu anayostahiki, na kwa msingi wa uadilifu. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa, umri na uhai tuliopewa si wa kuutumia kwa anasa, starehe, na mambo ya upuuzi. Ni wa kuutumia kwa kuufanyia kazi ukumbusho tunaopewa kwa kufanya mema na kuyaepuka maovu; vinginevyo, kadiri umri wa mtu unavyokuwa mrefu na akautumia kwa yasiyomridhisha Mola, ndivyo adhabu atakayopata itakavyokuwa kubwa pia. Vilevile aya tulizosoma zinatuonyesha kuwa, kutoutumia ipasavyo umri na neema zake ni kuitendea dhulma mtu nafsi yake; kama ambavyo kuyadharau maonyo na indhari za Mitume na mawalii wa Allah ni kujidhulumu mtu mwenyewe na kuwafanyia dhulma wao pia. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, katika misamiati ya dini kabla dhulma kuwa na maana ya kuwadhulumu wengine, kujidhulumu mtu kwa kuviharibu na kuvitumia vibaya vipawa na atiya alizojaaliwa na Mola, hiyo yenyewe pia ni dhulma. Sababu ni kuwa, chochote kile tulichonacho ni amana tuliyopewa na Mola, si milki yetu sisi. Miili hii tuliyonayo, si mali yetu ya kuwa na uhuru wa kuitumia vyovyote vile tutakavyo au tupendavyo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 784 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata, na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags

Maoni