Mar 25, 2018 08:40 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 785 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 39 ambayo inasema:

هُوَ الَّذِي جَعَلَكُمْ خَلَائِفَ فِي الْأَرْضِ ۚ فَمَن كَفَرَ فَعَلَيْهِ كُفْرُهُ ۖ وَلَا يَزِيدُ الْكَافِرِينَ كُفْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ إِلَّا مَقْتًا ۖ وَلَا يَزِيدُ الْكَافِرِينَ كُفْرُهُمْ إِلَّا خَسَارًا

Yeye ndiye aliye kufanyeni makhalifa katika ardhi. Na anaye kufuru, basi kufuru yake ni juu yake; na kufuru za makafiri haziwazidishii kwa Mola wao Mlezi ila kuchukiwa. Wala kufuru za makafiri haziwazidishii ila khasara.

Aya hii kwanza inatilia mkazo suala la ukhalifa na unaibu wa mwanadamu katika ardhi; suala ambalo wafasiri wa Qur'ani wamelitolea rai mbili tofauti: moja ni ukhalifa wa kiumbe huyo kama mwakilishi wa Allah duniani; na nyingine ni unaibu na ukhalifa wa kaumu moja mpya kurithi kaumu zilizotangulia. Katika hali zote hizo mbili aya inabainisha ihsani na fadhila za Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu za kumuidhinishia kuzitumia na kufaidika nazo neema na atiya za maumbile pamoja na kutiishiwa sayari hii ya dunia. Inavyohukumu akili timamu, ni mtu kumjua na kumshukuru mtoaji wa neema hizo, lakini kwa masikitiko ni kwamba, wanadamu wengi hawamjui mtoaji huyo na wanazikanusha neema alizowapa. Ukanushaji huo wa neema unaishia kwenye kumkana na kumkufuru Yeye Allah mwenyewe, hata hivyo madhara yake yanawarejea makafiri wenyewe. Sababu ni kwamba Mwenyezi Mungu SW si mhitaji wa shukurani za waja, kama ambavyo si mhitaji pia hata wa asili ya kuwepo kwao. Wakati wao walipokuwa hawapo, Mwenyezi Mungu alikuwepo, na wakati wao watakapotoweka, Allah SW ataendelea kuwepo. Kwa hivyo kukufuru na kuamini kwa watu hakumletei hata chembe ya faida au hasara Yeye Muumba wa ulimwengu; na kama ni faida na hasara, basi zitawarejea wao watu wenyewe. Na bila ya shaka ni jambo lililo wazi kwamba watu washukurivu na wenye kuamini watapata fadhila na rehma maalumu za Allah duniani na akhera; na wale makafiri watapatwa na ghadhabu na adhabu ya Mola kutokana na maovu waliyoyafanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kama ambavyo sisi ni warithi na makhalifa wa kaumu za kabla yetu, iko siku sisi pia tutaondoka na zitakuja na kuishi kaumu za watu wengine badala yetu; kwa hivyo tusiingiwe na ghururi kwa sababu ya tulivyonavyo wala kuzikufuru neema tulizopewa na Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa athari na matokeo hatari za kukufuru hayana mpaka bali huendelea kupanuka na kuenea. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba ukafiri huwa sababu ya kufanya madhambi aina nyingi na kumsukuma mtu kwenye lindi la maporomoko na maangamizi.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya aya 40 ambayo inasema:

قُلْ أَرَأَيْتُمْ شُرَكَاءَكُمُ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَرُونِي مَاذَا خَلَقُوا مِنَ الْأَرْضِ أَمْ لَهُمْ شِرْكٌ فِي السَّمَاوَاتِ أَمْ آتَيْنَاهُمْ كِتَابًا فَهُمْ عَلَىٰ بَيِّنَتٍ مِّنْهُ ۚ بَلْ إِن يَعِدُ الظَّالِمُونَ بَعْضُهُم بَعْضًا إِلَّا غُرُورًا

Sema: Mnawaona hawa miungu wenu wa kishirikina mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu! Nionyesheni wameumba sehemu gani katika ardhi? Au wana ushirika wowote katika mbingu? Au tumewapa Kitabu nao kwa hicho wakawa na hoja zilizo wazi? Lakini madhaalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu tu.

Aya hii inaibomoa misingi ya shirki kwa sura ya kuwahoji na kuwauliza masuali washirikina na kumtaka Bwana Mtume SAW awaambie watu hao watoe hoja ya kimantiki au ya kimapokezi ya kutetea kumshirikisha kwao Mwenyezi Mungu. Masuali yenyewe ni je, wale wanaowaitakidi kuwa washirika wa Mwenyezi Mungu katika kuendesha ulimwengu wamewahi kuumba kitu chochote kile mbinguni au ardhini? Bila shaka jibu ni hapana. Kama ni hivyo inakuwaje mnawafanya wao washirika wa Mungu ambaye ndiye muumbaji wa ulimwengu wote na vyote vilivyomo ndani yake?! Hivi kwa mtazamo wa kiakili, mtu au kitu kisicho na uwezo wa kuumba kinastahiki kweli kuwa mola na muabudiwa? Baada ya kubainika sasa kwamba hakuna hoja yoyote ya kiakili ya kutetea shirki, hebu waulize, katika vitabu vya mbinguni ambavyo Mwenyezi Mungu amewateremshia Mitume wake, je humo pia ameamuru au amejuzisha kuabudiwa miungu na maabudu bandia? Ni wazi kwamba hakuna hoja yoyote ya kimantiki au ya kimapokeo ya kuthibitisha jambo hilo isipokuwa ni fikra potofu na za kikhurafa ndizo zilizokupeni nyinyi matumaini ya kupata shufaa na uombezi wa washirika wenu hao, hivyo mkaamua kuwaabudu. Ni matamanio hewa na yasiyo na msingi ndiyo yaliyokuhadaeni na kukuwekeni mbali na njia sahihi ya kumwabudu Mungu wa haki. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mojawapo ya njia za kuwalingania watu Uislamu ni kuziamsha dhamiri zao kwa njia ya kuwatupia masuali. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa ukafiri na shirki havina mantiki wala mashiko yoyote ya hoja ya kiakili. Ni vitu vilivyojengeka kutokana na fikra potofu zinazomhadaa na kumpoteza mtu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kufru na shirki ni dhulma kwa mtu na utu wake; na madhara yake yanamrudia mtu mwenyewe.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 41 ambayo inasema:

إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا ۚ وَلَئِن زَالَتَا إِنْ أَمْسَكَهُمَا مِنْ أَحَدٍ مِّن بَعْدِهِ ۚ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anaye zuilia mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka hapana yeyote wa kuzizuia isipo kuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole Mwenye kusamehe.

Baada ya aya iliyotangulia kuzungumzia uumbaji wa mbingu na ardhi na viumbe wa ardhini, aya hii inaashiria tadbiri na uendeshaji wa mfumo mzima wa mbingu na ardhi ambao nao pia uko kwenye mamlaka ya Allah pekee, na hakuna kiumbe chochote ambacho ni mshirika wa Mola Muumba katika jambo hilo. Kwa kuwa washirikina walikuwa wakikubali kwamba Mwenyezi Mungu SW ndiye muumbaji wa kila kitu lakini wakawa wanaitakidi pia kuwa miungu yao bandia ni washirika wa Allah katika tadbiri na uendeshaji wa ulimwengu na majaaliwa ya maisha yao, aya hii ya 41 inasema: kama ambavyo hakuna yeyote aliye mshirika wa Allah katika uumbaji; katika uendeshaji wa masuala yote ya ulimwengu pia Yeye Mola hana mshirika. Kuuhifadhi mfumo mzima wa uumbaji na kuufanya uendelee kudumu nako pia kuko kwenye mamlaka ya Yeye Allah SW peke yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba hali ya mbingu na ardhi na utuliaji na ueleaji wa kila moja kati ya sayari ya dunia, jua pamoja na nyota katika mzingo na njia yake maalumu, yote hayo yanafanyika kwa irada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; na kudumu kwa kila kimoja hata kwa sekunde na nukta moja kunategemea qudra yake Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa nidhamu inayotawala katika mfumo wa ulimwengu wa maumbile inatokana na irada na ratiba iliyokwisha pangwa tokea hapo kabla na Allah SW; si kitu cha sadfa kilichotokea bila kukusudiwa mpaka kikafikia hatua na hali tunayoishuhudia. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Mwenyezi Mungu ni Muumba na pia wa Muendeshaji wa mambo. Kuwepo na kuendelea kubaki vitu vyote kuko kwenye mamlaka yake; na viumbe havitotoweka bila ya kutaka Yeye Mola. Vilevile aya inatutaka tujue kwamba lau kama si subira na usamehevu wa Allah ulimwengu huu wa maumbile ungewaangukia na kuwaporomokea waovu na madhalimu. Na ikiwa tunaona madhalimu wanapewa muhula bila kuadhibiwa ni kutokana na subira ya Mola; si kwa kutoweza kuwaadhibu na kuwaangamiza. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 785 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na kila aina ya shirki, kubwa na ndogo, ya dhahiri na iliyojificha. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags

Maoni