Mar 25, 2018 08:45 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 786 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 42 na 43 ambazo zinasema:

وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَئِن جَاءَهُمْ نَذِيرٌ لَّيَكُونُنَّ أَهْدَىٰ مِنْ إِحْدَى الْأُمَمِ ۖ فَلَمَّا جَاءَهُمْ نَذِيرٌ مَّا زَادَهُمْ إِلَّا نُفُورًا

Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kuapa kwao, kwamba akiwajia mwonyaji bila ya shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote. Lakini alipo wajia mwonyaji hakuwazidishia ila kuikimbia hiyo Haki,

اسْتِكْبَارًا فِي الْأَرْضِ وَمَكْرَ السَّيِّئِ ۚ وَلَا يَحِيقُ الْمَكْرُ السَّيِّئُ إِلَّا بِأَهْلِهِ ۚ فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا سُنَّتَ الْأَوَّلِينَ ۚ فَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَحْوِيلًا

Kwa kutakabari kwao katika nchi, na kufanya vitimbi vya uovu. Na vitimbi viovu havimsibu ila mwenyewe aliye vifanya. Basi hawangojei ila desturi ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na watu wa zamani? Basi hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu. Wala hutapata mageuko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa tafsiri za kuaminika za Qur'ani, wakati washirikina wa Makka waliposikia kwamba Mayahudi waliwaua baadhi ya Mitume wao na hawakuwa tayari kuyakubali mafundisho waliyokuja nayo, wao walikula kiapo na kusema: ikiwa sisi tutajiwa na Mtume tutayakubali maneno yake, tutauitika wito wake na tutafuata uongofu atakaokuja nao kuliko umma nyengine zilizopita. Lakini wakati Nabii Muhammad SAW alipopewa Utume na kuwatangazia watu wa Makka wito wa Lailah illa Allah, wakubwa wa Makureishi walisimama kumpinga na kumkadhibisha. Watu hao hawakuonyesha kitu kingine zaidi ya chuki na kufanya kila aina ya hila na vitimbi ili kuwazuia watu wasisilimu na kuukubali Uislamu. Ni wazi kwamba wao walitaka wajiwe na Mtume ambaye atafanya yale yanayoendana na utashi na matakwa yao au kwa uchache hatozungumzia mambo yanayokinzana na matashi yao. Lakini kwa kuwa mafundisho ya Uislamu yalizungumzia usawa wa watu wote mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, hilo lilikuwa jambo zito mno na lisiloweza kuvumilika kwa viongozi na maashrafu wa Kikureishi. Mabwanyenye hao hawakuwa tayari kamwe wawe sawa na watumwa na wajakazi wao. Kwa sababu kwa mtazamo wa Uislamu muungwana aliye huru na mtumwa na mjakazi anayemilikiwa, wote wawili ni viumbe wa Mwenyezi Mungu na thamani ya watu mbele yake Yeye Mola ni taqwa, utakasifu na uchajiMungu wao; si kwa kuwa kwao watu huru au watumwa, wamiliki au wamilikiwa. Chanzo cha baadhi ya watu kuupiga vita Uislamu na dini nyingine za mbinguni ni kuamua kukabiliana na Mwenyezi Mungu. Mtu anayefadhilisha alitakalo yeye badala ya analolitaka Allah SW na akawa hayuko tayari kusalimu amri mbele ya maamrisho ya Mola huwa na hali ya kutakabari. Mtu mwenye kutakabari hufanya kila hila na vitimbi ili kuidhoofisha dini ya Mwenyezi Mungu na daima huwa anapanga na kutekeleza njama hii au ile. Bila shaka atakapo Yeye Mola njama za waistikbari hao haziwi na taathira yoyote na mwishowe huwarejea wenyewe. Hii ni kaida na kanuni ya Allah kuhusiana na jamii za wanadamu. Kanuni ambayo haibadiliki na inabaki kuwa utaratibu na desuri thabiti iliyowekwa na Yeye Mola ambayo inafanya kazi katika zama zote za historia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba si kila kiapo kinaweza kuaminika. Pengine si hasha watu wakala viapo vikubwa vikubwa lakini mwishowe wakavihalifu kwa kutenda kinyume na walivyoviapia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mwanadamu anahitaji maonyo ili asije akaghafilika na kujisahau; na au kama amejisahau basi aweze kuzinduka kwa kutoka kwenye usingizi wa mghafala. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kukufuru kwa watu wengi hakutokani na kutoijua haki, lakini chimbuko lake ni hulka zao za kutakabari kwa kutokuwa tayari kusalimu amri na kumtii Muumba wa ulimwengu. Kadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba ulimwengu unaendeshwa kulingana na kaida na kanuni maalumu zilizowekwa na Allah. Ni muhimu kuzijua kaida na kanuni hizo kwa ajili ya kufuzu na kuifikia saada.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 44 ambayo inasema:

أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَكَانُوا أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً ۚ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعْجِزَهُ مِن شَيْءٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ ۚ إِنَّهُ كَانَ عَلِيمًا قَدِيرً

Je! Hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hao walikuwa wana nguvu zaidi kuliko wao. Na hakuna kitu kiwezacho kumshinda Mwenyezi Mungu mbinguni wala ardhini. Hakika Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye uweza.

Aya hii inaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kwa kuwahutubu makafiri na wakanushaji wote wa haki ya kwamba: kama mtatembea katika ardhi mtajionea wenyewe vipi ulikuwa utaratibu na kanuni za Allah kwa kaumu zilizopita kabla yenu. Watu wa kaumu hizo, ambao walikuwa na nguvu na uwezo mkubwa zaidi kuliko nyinyi, waliangamizwa pia kwa sababu ya kusimama kwao kuipinga haki; na hakuna athari yoyote ya nguvu na uwezo wao iliyosalia. Hebu jiulizeni, Firauni, Namrudi pamoja na wasaidizi wao waliowazunguka ambao kuna wakati walikuwa nembo za nguvu na utajiri kwa kutawala sehemu kubwa ya maeneo ya dunia hii, kuna kipi kilichobakia leo hii katika athari zao?! Je, wao waliweza kuizuia irada ya Allah SW na kumfanya Yeye Mola asitekeleze alitakalo? Je, waliweza kuikwepa qudra na mamlaka ya Mola na kuziokoa nafsi zao? Bila shaka kuisoma na kuipitia historia iliyopita ya dunia, ya kaumu na mataifa, wafalme na majabari mbalimbali kunabainisha kwa uwazi kabisa jinsi kaida na kanuni ya Allah inavyofanya kazi, kwamba ukafiri na dhulma havidumu na wala havina mwisho mwema. Hivyo basi, tupate funzo na ibra kwa waliotangulia na kuujenga mustakabali wetu kwa namna sahihi ili tusije tukafikwa na mwisho mbaya. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Qur’ani inawataka Waislamu wafanye safari za kutembelea sehemu mbalimbali na kutalii historia ya maisha ya kaumu zilizopita. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, katika dini ya Uislamu imeusiwa kuzitunza athari na turathi za kale zilizoachwa na watu wa staarabu na tamaduni mbalimbali na kutalii mambo yanayozihusu kaumu zilizopita na kupata ibra na mazingatio kwa hatima iliyowafika watu wa kaumu hizo. Vilevile aya hii inatuelimisha kwamba tusipumbazwe na kutekwa na nguvu na utajiri na makeke na vishindo vya wenye kutakabari. Tuzingatie na kutafakari juu ya hatima na mwisho wao. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hii kuwa tusiingiwe na ghururi kwa sababu ya nguvu na uwezo tulionao kwa sababu kulikuwa na jamii na watu wenye nguvu na uwezo mkubwa kuliko sisi lakini walihilikishwa na kuangamizwa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 786 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kupata ibra na mazingatio kwa yaliyowafika wa kabla yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags

Maoni