Mar 25, 2018 08:51 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 787 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Darsa yetu ya leo itazungumzia aya ya 45 na ya mwisho ya sura yetu hii. Aya hiyo inasema:

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۖ فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِعِبَادِهِ بَصِيرًا

Na lau Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa waliyo yachuma, basi asingeli muacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja. Lakini Yeye anawachukulia mpaka ufike muda maalumu. Ukifika muda wao basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake baraabara.

Aya hii inaendeleza maudhui tuliyozungumzia kwenye aya tulizosoma katika darsa iliyopita kuhusu hila na vitimbi vya watu wenye kutakabari na mwisho mbaya watakaokuwa nao kwa kueleza kwamba: bila ya shaka Allah SW ana subira kubwa mno na kwa hivyo si kwamba kila mtu anapofanya dhambi au kuteleza humteremshia adhabu papo hapo. Afanyavyo Yeye Mola ni kuwapa fursa na muhula wanadamu wote maadamu wangaliko hai hapa duniani ili watubie madhambi yao na kuziepusha nafsi zao na adhabu. Lakini utakapofika muda wa kufikwa na mauti na kushuhudia ishara zake, hapo tena hakutakuwa na istighfari wala toba yoyote itakayokubaliwa. Aya hii wapenzi wasikilizaji ambayo kama tulivyotanguliza kueleza kuwa ndiyo aya ya mwisho ya Suratu-Fati'r inadhihirisha ihsani na wema mkubwa wa Allah kwa waja wake; nao ni kwamba, hata kama watafanya madhambi, Yeye Mola hawapatilizi na kuwaadhibu papo hapo, bali huwapa fursa na muhula wa kutubia na kujirekebisha makosa waliyofanya. Na laiti kama isingekuwa hivyo, mwanadamu asingekuwa na uhuru na hiari bali angelazimika kuacha kufanya dhambi bila ya yeye mwenyewe kupenda. Kwa mfano kama angeona kwa macho yake mtu anayesema uongo anapatilizwa papo hapo kwa kuzibwa kauli na kufanywa bubu, yeye pia ingembidi ajiepushe na kusema uongo bila ya kutaka. Kwa hivyo kuamuliwa malipo ya thawabu au adhabu yakalipwe huko akhera huwafanya wale wanaotaka kufanya mema wafanye hivyo kwa hiari yao, na wale wanaoamua kutenda maovu na mabaya wafanye hivyo pia kwa hiari yao; pasina yeyote kati yao kuhisi kama kuna nguvu inayomlazimisha kufanya alifanyalo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba moja ya sababu za kuakhirishwa utoaji adhabu kwa watu hapa duniani na kucheleweshwa hadi Siku ya Kiyama ni kutaka kizazi cha mwanadamu kiendelee kubaki. Kwani kama watu wangekuwa wanaadhibiwa papa hapa duniani, kizazi cha mwanadamu kingelitoweka juu ya uso wa sayari ya dunia na asingesalia yeyote miongoni mwao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa subira ya Allah SW ni kubwa mno. Yeye ni mwenye kughufiria na kusamehe na pia ni mwenye kuwapa muda na muhula waja wake. Kwa sababu hiyo hamwadhibu mtu papo hapo kwa amali zake mbaya anazofanya. Lakini humpa fursa hadi mwisho wa uhai wake ya kujirekebisha kwa kuuacha upotofu na kurejea kwenye njia ya uongofu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, isitupitikie kuwa muhula na fursa anayotupa Allah inatokana na Yeye kutokuwa na habari ya tunayoyafanya. La hasha! Yeye Mola anayaona na anayajua yote tuyafanyayo kwa siri na kwa dhahiri, makubwa na madogo bali hata tuyawazayo akilini mwetu na yanayotupitikia ndani ya nafsi zetu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 787 ya Qur'ani imefikia tamati. Darsa hii pia imehitimisha tarjumi na maelezo kwa ufupi ya sura ya 35 ya Fati'r. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kufaidika na kunufaika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba pia Mola atuwezeshe kutubia madhambi yetu kabla ya mwisho wa uhai wetu, atutakabalie amali zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags

Maoni