Jun 30, 2018 09:05 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (59)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 59.

Katika mifululizo kadhaa iliyopita ya kipindi hiki, mbali na kuzungumzia chimbuko na malengo ya kuasisiwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), ikiwa ni moja ya vielelezo na nembo za kupatikana sauti moja na muelekeo mmoja katika Ulimwenngu wa Kiislamu, tumechambua vipindi na awamu nne tofauti za kihistoria za umri na harakati za jumuiya hiyo, ambapo katika awamu ya kwanza utambulisho wa OIC ulijengeka juu ya msingi wa kuundwa kwake wa malengo matukufu ya Palestina na kuleta aina fulani ya umoja na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu; lakini pia katika awamu ya pili, yaani kipindi cha hadi ulipofanyika mkutano wa tatu wa OIC mwaka 1997 hapa mjini Tehran, hali fulani ya muelekeo na sauti moja ilipatikana katika jumuiya hiyo ya nchi za Kiislamu. Katika marhala na awamu ya tatu ya umri wa OIC ambayo ilianzia katika mkutano wa Tehran yaani mwaka 1997 hadi lilipoibuka vuguvugu la umma la wananchi Waislamu katika nchi nyingi za Kiarabu mnamo mwaka 2011 hadi 2012 muelekeo wa pamoja kati ya nchi za Kiislamu ulifufuka na kuhuishwa tena. Kabla ya kuingia katika awamu ya nne ya umri wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, katika kipindi chetu cha leo tunataka kufanya tathmini jumla ya kiwango cha mafanikio iliyopata OIC katika kufikia malengo iliyojiwekea, na kisha baada ya hapo tutaijadili awamu ya nne ya umri wa jumuiya hiyo.

 

Kama tunataka kufanya tathmini kuhusu kiwango cha mafanikio ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu au ile iliyokuwa ikijulikana kama Jumuiya ya Nchi za Kiislamu katika kufikia malengo yake, inapasa kwanza tujiulize suali hili; ni ipi hasa mizani na kipimo cha kutumia ili kujua mafanikio ya jumuiya au taasisi fulani? Kwa maneno mengine ni kuwa, utendaji wa jumuiya yoyote ile inapasa utathminiwe kwa kutumia kigezo gani ili kuweza kubaini kama imepata au haijapata mafanikio yoyote? Moja ya vipimo muhimu vya kutumia kutathmini utendaji wa jumuiya fulani ni ufanisi wake; na kwa muktadha huo jumuiya ya kimataifa itatathminiwa kwamba ni asasi iliyofanikiwa kama itaweza kuthibitisha kuwa utendaji wake katika uga wa kimataifa umekuwa na faida na ufanisi na kuathiri mwenendo wa matukio ya kimataifa katika kufikia malengo yake. Kuna wale wanaoamini kwamba ufanisi wa jumuiya yoyote ya kimataifa unategemea uwezo wa jumuiya hiyo katika kushughulikia na kudhibiti migogoro inayoathiri utendaji wake. Kuna wengine pia wanaoitakidi kuwa ufanisi na mafanikio ya jumuiya yoyote ya kimataifa yanapimwa kwa kuangalia uwezo au mafanikio ya nchi wanachama katika kutatua masuala na matatizo yao kulingana na kiwango cha utekelezaji wa maamuzi ya jumuiya yao.

Kama tutataka kutumia mtazamo wa pili kutathmini utendaji wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu inapasa tuseme kuwa, kwa kuzingatia malengo na misingi iliyobainishwa kwenye hati ya kuasisiwa kwake, mafanikio ya OIC katika kipindi cha hadi lilipoanza vuguvu la Mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu mnamo mwaka 2011 yalikuwa ya kiwango cha wastani au cha kati na kati. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika kipindi hicho OIC haikuweza kufikia kikamilifu malengo iliyojiwekea, lakini pia si insafu kudai kwamba jumuiya hiyo haikupata mafanikio yoyote kiutendaji; kwa sababu laiti kama OIC isingelikuwepo, bila shaka hali ya umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu ingelikuwa mbaya zaidi. Kwa hivyo tathmini jumla inaonyesha kuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu imeweza kwa kiwango fulani kuleta hali ya muelekeo wa pamoja baina ya nchi wanachama. Ili kufafanua na kuthibitisha dai hilo inatosha kuyatupia jicho tena malengo na misingi ya hati ya OIC. Ndani ya hati hiyo yametajwa malengo kadhaa ikiwemo kustawisha umoja baina ya nchi za Kiislamu, kung’oa mizizi ya ukoloni, kupambana na ubaguzi wa rangi, kutoa msukumo kwa mapambano ya wananchi wa mataifa ya Waislamu ya kulinda heshima yao ya kiutu, kujitawala kwao na haki zao za kitaifa. Kwa hivyo ili kupima kiwango cha mafanikio ni aula kuangalia natija na matokeo ya hatua za kivitendo zilizochukuliwa na OIC na kulinganisha na malengo iliyojiwekewa.

 

Moja ya nukta muhimu na yenye kutiliwa mkazo katika misingi na malengo yaliyotajwa kwenye hati ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ni kulinda amani na usalama wa nchi wanachama. Kwa hivyo ni mahali pake kujiuliza, kama jumuiya ya OIC imeweza kutetea na kulinda usalama wa wanachama wake? Na kama imeweza kufanya hivyo, ni kwa kiwango gani? Ili kulitolea jawabu suali hili inafaa tuzitathmini hatua zilizochukuliwa na OIC katika uwanja huo. Uhakiki uliofanywa unaonyesha kuwa, kwa mtazamo jumla, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu imechukua hatua za aina mbili katika suala la kulinda na kuimarisha usalama wa pamoja wa nchi wanachana. Aina ya kwanza ya hatua hizo ni ya msimamo uliochukuliwa na OIC kuonyesha mshikamano wake na nchi wanachama na wakati huohuo kulaani hatua hatarishi zilizochukuliwa na nchi ajinabi dhidi ya amani na usalama wa nchi wanachama wa jumuia hiyo. Kutangazwa mshikamano na uungaji mkono wa jumuia ya OIC kwa wananchi wa Lebanon wakati Israel ilipoivamia nchi hiyo mwaka 1982; kuunga mkono juhudi za serikali ya Lebanon za kurejesha mamlaka ya kujitawala na udhibiti wa maeneo yote ya ardhi ya nchi hiyo katika matukio ya mwaka 1997 na 1999; kutangaza mshikamano na wananchi wa Somalia wakati nchi hiyo ilipovamiwa na Ethiopia mwaka 1984; na hatimaye kuonyesha kwamba OIC iko pamoja na wananchi wa Azerbaijan pale nchi hiyo ilipovamiwa na Armenia mwaka 1993 ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na jumuiya hiyo ya nchi za Kiislamu katika uwanja huo.

Aina ya pili ya hatua zilizochukuliwa na jumuiya za nchi za Kiislamu ni ya kutotosheka na kutoa uungaji mkono wa maneno matupu, lakini kwa kwenda mbali zaidi na kuchukua hatua za kivitendo pia katika kuziunga mkono nchi wanachama. Mfano wa hatua hizo ni kwamba mara baada ya Shirikisho la Kisovieti la Urusi ya zamani kuishambulia na kuivamia ardhi ya Afghanistan, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ilifanya kikao cha dharura katika ngazi ya mawaziri ya mambo ya nje mjini Islamabad, Pakistan na kuchukua hatua maalumu dhidi ya serikali ghasibu iliyotwaa madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi na vile vile dhidi ya serikali ya Urusi iliyoiunga mkono serikali hiyo. Jumuiya ya nchi za Kiislamu ilisimamisha uwanachama wa Afghanistan katika jumuiya hiyo na vile vile ikasusia michezo ya Olimpiki iliyofanyika mwaka 1980 mjini Moscow.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki kwa leo umemalizika, hivyo sina budi kuishia hapa nikiwa na matumaini kwamba mtajiunga nami tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki. Basi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.

Tags

Maoni