Jun 30, 2018 09:12 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (60)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 60.

Kwa wale wasikilizaji wetu wanaofuatilia kwa karibu kipindi chetu hiki, bila shaka mngali mnakumbuka kuwa mazungumzo yetu katika mfululizo uliopita wa 59 yaliishia pale tulipoashiria aina ya pili ya hatua zilizochukuliwa na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, ambayo ni ya kutotosheka na kutoa uungaji mkono wa maneno matupu, lakini kwa kwenda mbali zaidi na kuchukua hatua za kivitendo katika kuziunga mkono nchi wanachama. Tukasema kuwa mfano wa hatua hizo ni kwamba mara baada ya Shirikisho la Kisovieti la Urusi ya zamani kuishambulia na kuivamia ardhi ya Afghanistan, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ilifanya kikao cha dharura katika ngazi ya mawaziri ya mambo ya nje mjini Islamabad, Pakistan na kuchukua hatua maalumu dhidi ya serikali ghasibu iliyotwaa madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi na vile vile dhidi ya serikali ya Urusi iliyoiunga mkono serikali hiyo. Jumuiya ya nchi za Kiislamu ilisimamisha uwanachama wa Afghanistan katika jumuiya hiyo na vile vile ikasusia michezo ya Olimpiki iliyofanyika mwaka 1980 mjini Moscow.

 Hatua nyengine iliyochukuliwa na OIC ilikuwa ni ya kuyaunga mkono makundi ya Mujahidina ya Afghanistan katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi katika ardhi ya nchi hiyo kiasi kwamba msimamo wa OIC ulikuwa moja ya sababu zilizoyafanya majeshi ya Shirikisho la Kisovieti yaondoke katika ardhi ya Afghanistan. Maudhui nyengine ni kuhusiana na kadhia ya Palestina. Kama tulivyotangulia kuashiria katika vipindi vilivyopita, kwamba Palestina ni moja ya ajenda kuu ambazo OIC imekuwa ikizifanyia kazi; na katika kipindi cha miaka yote ya shughuli zake imekuwa kila mara ikiunga mkono mapambano ya watu wa Palestina, japokuwa kumekuwepo na hali ya kupwa na kujaa katika wimbi hilo la uungaji mkono, ambapo baadhi ya wakati OIC imekuwa ikilegeza msimamo katika kutetea na kuunga mkono “Jihadi” ya watu wa Palestina. Kuanzishwa Mfuko wa Quds katika kikao cha saba cha mawaziri wa mambo ya nje, kuundwa kamati ya Quds mwaka 1975 na kuasisiwa ofisi ya Kiislamu ya kuisusia Israel ni miongoni mwa hatua za kivitendo zilizochukuliwa na OIC kuhusiana na kadhia hiyo.

 

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu haina rekodi nzuri katika suala la kulinda usalama wa pamoja wa nchi wanachama; kwa sababu katika kadhia nyingi, hatua zilizochukuliwa na OIC zilikuwa zaidi ni za kudhibiti tu hali ya mambo, na si kutatua tatizo lililopo. Kwa maneno mengine ni kuwa, pamoja na athari chanya za hatua zilizochukuliwa na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, lakini inapasa tuseme kuwa kuna tofauti kubwa kati ya hatua zilizochukuliwa na malengo yaliyoainishwa kwenye hati ya kuasisiwa jumuiya hiyo. Moja ya misingi mikuu ya hati ya OIC umetajwa kuwa ni “kutatua kwa njia za amani” hitilafu baina ya wanachama wa jumuiya hiyo. Kwa hivyo katika kutathmini kiwango cha mafanikio iliyopata Jumuiya ya Nchi za Kiislamu inatakiwa tulipatie jibu suali hili, kwamba ni kwa kiwango gani OIC imeweza kuzuia kutokea mizozo baina ya nchi za Kiislamu; na kwa upande wa masuala na matatizo yaliyopo, imewezaje kuyatatua kwa njia kama za upatanishi, mazungumzo au utoaji hukumu baina ya pande husika? Kwa kuyaangalia matukio yaliyojiri katika Ulimwengu wa Kiislamu itatupasa tuseme kuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu haijapata mafanikio yoyote katika uwanja huo; na hata katika baadhi ya matukio imechukua hatua za kushadidisha na kukoleza moto wa migogoro, vita na umwagaji damu baina ya nchi za Kiislamu. Kwa mfano katika vita vya Iran na Iraq, utendaji wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu haukuwa wa haki, na kutokana na sauti ya juu ziliyokuwa nayo nchi za Kiarabu mgogoro wa vita hivyo ulishtadi zaidi.

Lakini pia katika mzozo uliojitokeza mwaka 1989 kati ya Mauritania na Senegal, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ilizitaka pande mbili zihitimishe uadui na uhasama baina yao; lakini kivitendo haikutoa pendekezo lolote la hatua za kuchukuliwa kwa ajili ya kutatua mgogoro kati ya nchi hizo mbili; na kimsingi ilichofanya ni kuuachia uwanja na kibarua Umoja wa Afrika cha kufanya kazi ya upatanishi katika mzozo huo. Lakini mbali na yote hayo, jumuiya ya OIC haikuweza kuzuia uvamizi uliofanywa na Iraq mwaka 1990 dhidi ya ardhi ya Kuwait; na baada ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Kuwait, ilitosheka tu na kutoa wito kwa Iraq wa kuitaka iondoke katika ardhi ya nchi hiyo. Lakini pia wakati katika Umoja wa Mataifa ulipopitishwa kwa kauli moja uamuzi wa kuchukua msimamo dhidi ya Iraq, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu iliunga mkono uamuzi huo wala haikuweza kuwa na sauti katika kadhia hiyo.

 

Katika suala la kutafuta suluhu na maridhiano ya mgogoro wa Afghanistan pia, maamuzi yaliyopitishwa na OIC hayakudumu kwa muda mrefu; na moto wa vita na mapigano kati ya makundi ya mujahidina ukaripuka tena; na juhudi zilizofanywa kwa ajili ya kuhitimisha mapigano hayo hazikuwa na tija yoyote. Kwa hivyo kwa ujumla tunaweza kusema kuwa rekodi ya utendaji wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu katika kutatua kwa njia za amani mizozo na hitilafu ni dhaifu zaidi kulinganisha na suala la kulinda usalama wa pamoja wa nchi wanachama.

Katika kuyafanyia majumuisho mazungumzo yetu ya leo tunaweza kusema kuwa utendaji wa OIC unaonyesha kwamba katika kipindi chote cha tangu kuasisiwa kwake, jumuiya hiyo haijaweza kufanikisha kikamilifu malengo na misingi ambayo nchi wanachama zilikuwa zimejipangia kwa mujibu wa hati ya OIC. Kwa muktadha huo rekodi iliyojiwekea si ya mafanikio makubwa, lakini pia haitakuwa insafu kama tutafumbia macho au kudogosha jitihada ilizofanya OIC katika kupoza moto wa baadhi ya migogoro na baadhi ya hatua chanya ilizochukua kwa madhumuni ya kufikia malengo iliyojiwekea. Lakini suali linalojitokeza hapa kwa sasa ni, kwa nini nchi za Kiislamu, ambazo zina masuala ya kiitikadi na maslahi mengi ya pamoja, ambapo kipindi kimoja cha historia ya matukio ya kimataifa, masuala hayo ya pamoja yalizipa msukumo wa kuunda jumuiya kwa ajili ya kufuatilia na kuyafikia malengo hayo ya pamoja, katika muda wote wa miongo kadhaa ya utendaji wake haijaweza kuleta umoja na mshikamano unaotakiwa? Katika sehemu ijayo ya 61 ya kipindi hiki tutajaribu kufanya uhakiki na upembuzi ili kuweza kutambua chimbuko la udhaifu wa kutopatikana mafanikio yaliyokusudiwa kutokana na utendaji wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu. Na kutokana na natija tutakayofikia katika uhakiki huo tutaweza kupata taswira ya kutathmini utendaji wa OIC katika awamu ya nne inayofuatia. Hadi wakati huo inshallah, nakuageni kwa kukutakieni kila la heri maishani.

Tags

Maoni