Jul 07, 2018 14:18 UTC
  • Timu ya Iran yatia fora katika mashindano ya roboti duniani

Makala hii huangazia baadhi ya mafanikio muhimu ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani na kati ya mengine leo tutaangazia mafanikio ya timu ya wanafunzi Wairani katika mashindano ya roboti duniani.

Katika uga wa teknolojia, hivi karibuni wanasayansi Wairani walifanikiwa kupata zawadi au tuzo mbili muhimu za kimataifa.

Profesa Davood Younesian Mhadhiri katika Kitivo cha Uhandisi wa Reli katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran alitunukiwa Tuzo ya Mwaka 2017 ya  Kimataifa ya Taasisi ya Kimataifa ya Wahandisi wa Kimekaniki wa Reli. Alipata tuzo hiyo kutokana na ubunifu wake wa kuunda mfumo wa kudhibiti mtikisiko wa mabehewa ya mizigo yenye kusheheni bidhaa za maji. Makala kuhusu uvumbuzi huo ilichapishwa katika jarida lenye itibari la kimataifa la Rail and Rapid Transit mwaka 2016. Taasisi ya Kimataifa ya Wahandisi wa Kimekaniki (IMechE) ambayo iliasisiwa mwaka 1847 ina makao yake makuu Uingereza, na ni kati ya taasisi muhimu kongwe na zenye itibari kubwa zaidi ya uhandisi duniani.

Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran

Katika mafanikio mengine Mtafiti Muirani, Mahdi Sarai Tabrizi, ametunukiwa zawadi ya kimataifa ya mtaalamu bora kijana katika uga wa kubana matumizi ya maji ya kilimo. Sarai Tabrizi ni Naibu Profesa wa Chuo cha Uhandisi wa Maji Katika Kitengo cha Sayansi na Utafiti cha Chuo Kikuu cha Azad Islami mjini Tehran. Ametunukiwa  zawadi hiyo na Tume ya Kimataifa ya Unyunyizaji  Maji ICID. Katika mradi wake huo, amefanya utafiti kwa muda wa karibu miaka minne ambapo amekuwa akitathmini kiwango cha maji yanayohitajika katika ukuzaji mazao ya kilimo. Matokeo ya utafiti huo yanaweza kutumika katika maeneo makavu na kuokoa asilimia 10 ya maji yanayotumika hivi sasa.

 

Wiki hii shirika moja la utafiti nchini Iran lilitangaza kutumia teknolojia ya nano kutengeneza sakafu ambazo zina uwezo mkubwa wa kustahamili msongamano mkubwa wa watu na mizigo katika viwanja vya ndege na bandari.

Msimamizi wa mradi huo Dkt. Saeed Bozorgmehr amesema utengenezaji wa sakafu kama hizo umetegemea utumizi wa mada za nano teknolojia ikiwemo mada inayojulikana kama SiO2.

Bozorgmehr amesema tayari idadi kubwa ya nchi jirani zikiwemo Iraq, Afghanistan na Pakistan zimeshaanza kununua bidhaa hizo lakini amesema kwa sasa hawauzi bidhaa hiyo nje kutokana na kutokuwa na uwezo  wa kuisafirisha masafa marefu.

Nano

 

Wiki hii Iran ilizindua upya kiwanda cha uzalishaji gesi aina ya UF6 kwa mujibu wa amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu kuimarisha uwezo wa nchi katika kurutubisha madini ya urani.

Gesi za urani za hexafluoride au UF6 hutumika katika mashinepewa wakati wa kurutubisha madini ya urani yanayotumika katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia. Kiwanda cha kuunda UF6 ni sehemu kubwa ya Kituo cha Kubadilisha Urani (UFC) cha mjini Isfahan katikati mwa Iran.

Keki ya njano, ambayo ni mali ghafi ya utengenezaji fueli ya nyuklia iliondolewa katika kituo cha UFC miaka kadhaa iliyopita.

Kuzindiluwa tenda kiwanda hicho ni sehemu ya amri ya  Kiongozi Muadhamu aliyotoa kwa Shirika la Atomiki la Iran mwezi Juni. Ayatullah Khamenei aliweka wazi hilo katika hotuba aliyotoa siku ya Jumatatu katika kumbukumbu ya mwaka wa 29 tangu alipoaga dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini (MA), na kutangaza pia kwamba: "Shirika la Nishati ya Atomiki lina wajibu wa kuchukua hatua haraka za utangulizi na za maandalizi yanayohitajika kwa ajili ya kufikia kiwango cha SWU 190,000 , ambapo kwa sasa lifanyike hilo kulingana na makubaliano ya JCPOA."

Mitambo ya Iran ya gesi za urani za hexafluoride au UF6 hutumika katika mashinepewa

Kutangulia kuchukua hatua za kivitendo na za kuleta mlingano kulikofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa nyuklia kumeonyesha kuwa kujitoa Marekani kwenye makubaliano ya JCPOA hakuwezi kuliyumbisha taifa hili na kulifanya liliridhie mashinikizo na vikwazo, sambamba na kukubali kupunguza kiwango cha shughuli zake za nyuklia ambazo ni muhimu kwa mustakabali wa nchi hii hasa katika uga wa sayansi na teknolojia.

Lugha za Afrika zinatazamiwa kuwa na nafasi rasmi katika utafiti wa kisayansi baada ya kuanzishwa kituo ambacho kinahimiza na kukubali utafiti ulioandikwa kwa lugha za Kiafrika kama vile Kiswahili, Kiakan, Kizulu, Kihausa n.k.

Tovuti ya AfricArXiv inachapisha Makala ambazo zimeandikwa na watafiti Waafrika au zile zinazohusiana na bara la Afrika.

Tovuti hiyo inajiunga na tovuti zinginezo ambazo zinajaribu kuhakikisha kuwa Wanasayansi Waafrika hawabaki nyuma katika uchapishaji makala zao. Makala ambazo zitawekwa katika tovuti hiyo kwanza zitapitiwa na wataalamu au watafiti wengine ambao watatoa maoni yao kabla ya makala kuchapishwa rasmi.

Tovuti hiyo itapokea Makala kwa lugha za Kiingereza na Kifaransa lakini Makala zilizoandikwa kwa lugha za Kiafrika zitahimizwa zaidi.

Kuna takribani lugha 2,000 barani Afrika lakini zimekuwa zikipuuzwa katika elimu na badala yake lugha za Wakoloni zimekuwa zikifadhilishwa. Hii ni pamoja na kuwa utafiti umebaini kuwa masomo kwa lugha ya mama si tu kuwa hupunguza gharama lakini pia huimarisha uwezo wa kustawi kiakili na ubora wa masomo katika shule za msingi hadi vyuo vikuu.

Waanzilishi wenza wa  tovuti ya AfricaArXiv, Justin Ahinon wa Chuo cha Kitaifa cha Takwimu cha Benin na Jo Havemann wa Shirika la Access 2 Prespective la Ujerumani wanasema fikra ya kuanzisha tovuti hiyo ilitokana na jumbe za Twitter katika kongamano la Kisayansi mwezi Aprili. Wanasema tovuti ya AfricArXiv inawalenga wasomi wa vyuo vikuu katika nyanja mbali mbali kama vile usanifu majengo, fizikia,sayansi za tiba na hisabati. Watumizi wa tovuti hiyo hawatatozwa ada ili kuhimiza watafiti wengi kushiriki.

 

Na Timu za roboti za Iran zimepata mafanikio makubwa katika Mashindano ya Kimataifa ya Robotiki yaliyofanyika siku chache zilizopita huko Montreal nchini Canada.

Mashindano hayo yalimalizika Juni 22 na timu za Iran zilirejea nyumbani zikiwa na medali tatu za dhahabu, tatu za fedha na moja ya shaba.

Timu ya Roboti ya MRL kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad mjini Qazvin ilishiriki katika mashindano hayo pamoja na timu zingine mbili za Iran na kuchukua nafasi ya kwanza katika kategoria tatu za ‘Zoezi la Uokoaji’, ‘Kuhamisha Vitu kwa Kutumia Roboti ya Uokoaji’, na ‘Mashindano ya Kiufundi ya Roboti ya Humanoid-Inayoshabihiana na Mwanadamu-‘

Mashindano ya soka ya roboti

Aidha wanachuo kutoka vyuo vikuu vya Iran walishika nafasi ya pili katika kategoria tatu za ‘roboti za humanoid zenye kimo cha watoto’, roboti za humanoid zenye kimo cha mabarobaro’ na ‘roboti za uokoaji’.

Aidha timu ya Iran ilimaliza ya tatu katika kategoria ya ‘’roboti za kiviwanda. Nchi zingine ambazo zilishiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Ujerumani, Marekani, Ureno, Austria, China, Brazil, Uholanzi,  Uturuki, Mexico, Japan, Canada na Singapore. Mashindano ya Kimatiafa ya RoboCup mwaka ujao yamepangwa kufanyika nchini Australia.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kati ya nchi ambazo hushinda medali nyingi katika mashindano ya kimatiafa ya RoboCup.

Baada ya kurejea nyumbani wanachuo Wairani walioshinda medali katika mashindano hayo ya RoboCup huko Monreal walizutunuku medali hizo kwa Jumba la Makumbusho la Astan Quds Razawi katika Haram Takatifu ya Imam Ridha AS mjini Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran.

 

 

 

 

 

Tags

Maoni