Jul 11, 2018 13:04 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (118)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia moja ya tabia mbaya za kimaadili nayo ni uzuaji na usingiziaji au utungaji uwongo.

Tulisema kuwa, uzushi ni kumzulia mtu uwongo na kumnasibisha na mambo mabaya ambayo kimsingi hana. Tulieleza kwamba, Mafundisho ya Uislamu ambayo yanawataka wanadamu waishi kwa amani, usalama, huba na mapenzi yanayoambatana na ushirikiano na kuoneana huruma, yamekemea kwa nguvu zake zote tabia hii mbaya na kuwataka watu wajitenge nayo hasa kutokana na kutokuwa na majaaliwa na hatima njema. Aidha tulibainisha kwamba, Katika mafundisho ya Kiislamu, mtu mwenye tabia ya kuwazulia watu mambo anahesabiwa kuwa mtu mbaya zaidi ambaye Siku ya Kiama atakumbwa na adhabu kali zaidi katika moto wa jahanamu. Moja ya misdaqi na mifano ya wazi ya uzuaji ni kuwaudhi waumini ambapo aya ya 58 ya Surat al-Ah'zab inasema:

Na wale wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilio dhaahiri.

Mtume saw akiwa na lengo la kuwafanya Waislamu wajiweke mbali na dhambi ya kuwazulia watu anasema kuwa: Kila ambaye atamzulia muumini mwanamume au mwanamke au amnasibishe na kitu ambacho yuko mbali nacho, Mwenyezi Mungu atambakisha mtu huyo Siku ya Kiama katika moto wa Jahanamu mpaka atakaposafishwa na dhambi hiyo. Wapenzi wasikilizaji, udaku na umbea ni tabia nyingine mbaya na dhambi inayotokana na kutumia vibaya ulimi. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 118 ya mfululizo huu kitazungumzia tabia hii mbaya ya kimaadili na kubainisha baadhi ya nukta muhimu zilizobainishwa na mafundisho ya Uislamu kuhusiana na suala hili. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Udaku au umbea ni kuchukua maneno ya huku na kuyapeleka kule. Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, umbe maana yake ni mtu kuchukua maneno aliyosemwa mtu fulani na kuyapeleka kwa aliyesemwa. Kwa mfano mtu akaenda kwa fulani na kumueleza kwamba, unajua fulani amesema hivi na hivi kukuhusu. Tabia hii inajulikana kama umbea na mwenye kufanya kitendo hicho anajulikana kama mbea au mdaku. Katika jamii yoyote mtu mwenye tabia ya umbea huchukiwa, hutengwa na hata wakati mwingine hupigwa kwa kuonekana kuwa ni chanzo cha migogoro na huku viongozi wa dini wakimwona mtu wa aina hiyo kuwa ni mtenda dhambi.

Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: Watu wabaya kabisa miongoni mwenu ni wale wanaochukua maneno ya huku na kuyapeleka kule na kuleta utengano baina ya marafiki na wanachunguza aibu na mapungufu ya watu wasafi. Aidha Bwana Mtume SAW amenukuliwa katika hadithi yenye madhumuni kama hiyo akisema kwamba: Je mnataka nikujulisheni watu washari na wabaya kabisa? Hadhirina wakasema: Ndio ewe Mtume wa Allah! Kisha mbora huyo wa viumbe akasema: Ni wale ambao ni wambea na wadaku, ambao wanazusha mifarakano na utengano baina ya marafiki na wanatafuta aibu za watu wasio na hatia na wasafi na kuwakwamisha.

Wapenzi wasikilizaji kupitia hadithi hizo mbili tunafahamu kwamba, umbea na kuchukua maneno ya huku na kuyapeleka kule ni katika tabia mbaya kabisa za kimaadili na humfanya mhusika kuwa mtu mbaya kabisa miongoni mwa watu hasa kutokana na kuzusha mifarakano baina ya watu na hata kupeekea marafiki wawili kutengana.

Mtume wa Allah Muhammad al Mustafa SAW anasema katika hadithi nyingine kuhusiana na maudhui hii kwamba, maadui wenu wakubwa kabisa mbele ya Allah ni wale wanaochukua maneno ya huku na kuyapeleka kule, wanaoisambaratisha jamii iliyokuwa imeshikamana na kazi yao ni kuzusha mifarakano baina ya jumuiya na kutafuta aibu za watu wasafi na wema.

Kwa mtazamo wa Uislamu, ulimi ni moja ya nyenzo ambazo mwanadamu anapaswa kuzichunga kwa umakini mkubwa; kwani dhambi nyingi chimbuko lake ni ulimi ambapo uli huwa wenzo wa kufanya dhambi hizo kama kusengenya, kusema uongo, kuwazulia watu, kutukana na kutoa maneno machafu na kadhalika. Aidha mafundisho ya Uislamu yanaeleza wazi kwamba, dhambi nyingi kubwa hufanywa na ulimi. Umbea na kuchukua maneno ya huku na kuyapeleka kule nao umo katika orodha ya matendo machafu yanayofanywa kwa njia ya ulimi ambayo yanahesabiwa kuwa ni katika madhambi makubwa.

Katika suala la umbea mhusika huteda dhambi mbili. Mosi hufanya khiyana na usaliti wa amana kwa kutoa habari za watu na pili huwa amesengenya wakati anapowasilisha maneno aliyoyasikia mahala kwa anakuwa amefichua siri za watu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana tabia ya umbea na udaku inachukiwa na Mwenyezi Mungu.

Imam Ali AS anampongeza mtu aliyejiweka mbali na tabia hii pale anaposema: Hongera kwako wewe ambaye umjitenga mbali na udaku na umbea ambao unapanda chuki katika moyo na unamuweka mbali mtu na Mola Muumba.

Qur’ani Tukufu inawaonya na kuwatahadharisha wale wanaochukua maneno ya huku na kuyapeleka kule kwamba, amali hiyo ni katika matendo mabaya ambayo matokeo yake ni kumbukwa na dhambi hapa duniani na kesho akhera.

 kwamba, Bwana mmoja alimwambia Imam Ali bin Hussein Sajjad (as) kwamba: Fulani anakusema vibaya wewe na kukutaja kuwa ni mpotoshaji na mwenye kuleta bidaa na uzushi.

Imam Sajjad AS akamwambia Bwana yule, hukuwa na haki ya kukaa pamoja naye, kwani umenifikishia maneno aliyoyasema kunihusu mimi. Aidha hukunitendea haki kwani umenifikishia kitu kutoka kwa ndugu yangu ambacho sikuwa na habari nacho!…jiepushe na kusengenya, kwani hiyo ni mboga ya mbwa wa motoni; na tambua kwamba, mtu ambaye anataja aibu na mapungufu ya watu wengine inaonyesha kwamba, anazitafuta aibu hizo kwa wengine kwa kiwango kile kile ambacho anazo yeye

 

Tags

Maoni