Jul 21, 2018 11:08 UTC
  • Watafiti wa Kenya, Tanzania, Uhispania kuboresha mihogo

Wakaazi wa Afrika Mashariki wataweza kupata mihogo bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa kutokana na ushirikiano wa watafiti wa Kenya, Tanzania na Uhispania. Hayo ni kati ya yaliyomo katika makala yetu ya leo ya sayansi na teknolojia.

Katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia, hivi karibuni tulishuhudia mafanikio makubwa ya Wanasayansi walio katika mashirika ambayo msingi wake ni elimu au knowledge-based  ambao wamefanikiwa kutengeneza dawa ya kuzuia mwili kukataa figo iliyopandikizwa. Mkuu wa mradi huo, Sirous Zeinali amesema dawa hiyo inafanyiwa majaribio katika maabara na iko katika mkondo wa kupata kibali cha kufanyiwa majaribio katika mwili wa mwanadamu. Nchini Iran hivi sasa uzalishaji wa dawa erevu za kibioteknolojia umeshuhudia ustawi mzuri. Dawa hiyo ambayo wanasayansi Wairani wameitengeneza, ikianza kuuzwa, itakuwa inagharimu asilimia 40 chini ya bei ya dawa inayoshabihiana na iliyotengenezwa katika nchi za kigeni. Iran imekuwa ikitumia mamilioni ya dola kuagizia dawa kama hizo kutoka nje ya nchi na hivyo kutengenezwa dawa hiyo ndani ya nchi kutaiokolea nchi hii kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.

 

Hivi karibuni watafiti Wairani walifanikiwa kuunda aina mpya ya chombo cha electroencephalography kwa kifupi EEG. Electroencephalography ni njia  ya utafiti wa ubongo kwa kurekodi uwezo wake wa umeme.

Shahbazi Askari wa shirika ambalo limeunda chombo hicho anasema chombo walichounda kinaweza kulinganishwa vizuri na mshabaha wake wa kigeni na pia kiwango chake cha kelele kiko chini sana. Mbali na hayo, shirika husika la Iran pia limeweza kuunda programu ya kompyuta ambayo inafanya utumizi wa chombo hicho kuwa rahisi zaidi. Halikadhalika kwa kuzingatia teknolojia ya juu iliyotumika kuuunda chombo hichi cha EEG nchini Iran, bei yake ni nafuu sana ikilinganishwa na mshabaha wake wa kigeni.

Chombo cha EEG

Kwa mtazamo wa viwango, chombo hicho kipya cha EEG kimeidhinishwa na Wizara ya Afya ya Iran na kimeweza pia kupata cheti cha kiwango cha kimataifa cha ISO, CE 13485 na pia cheti cha ubora cha Canada kinachojulikana kama Health Canada.

Katika mafanikio mengine, kwa mara ya kwanza mtafiti Muirani ametunukiwa zawadi ya kifahari ya  hidrolojia  katika Jumuiya ya Jiolojia ya Marekani. Mtafiti huyo kwa jina la Amir Aghakouchak amevumbua vianzo vya maji chini ya ardhi katika Jangwa la Lut nchini Iran ambalo ni eneo lenye joto jingi zaidi duniani.

Aghakouchak ambaye ni mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha California ni kati ya watafiti maarufu zaidi duniani katika uga wa sayansi za hidrolojia. Kwa kifupi hidrolojia ni tawi la sayansi inayohusu maji na harakati zake ardhini.

Utafiti uliofanywa na Aghakouchak umechapishwa katika majarida yenye itibari duniani na yeye binafasi anasema amevumbua kiwango kikubwa cha maji katika kina cha Jangwa la Lut. Amesema yeye akiwa na timu yake ya utafiti wametembelea jangwa hilo mara kadhaa kwa ajili ya utafiti. Anasema wamefikia natija kuwa kuna hifadhi ya maji chini ya ardhi katika baadhi ya maeneo ya Jangwa la Lut lakini hawajaweza kubaini kikamilifu wingi wa maji hayo. Aghakouchak anasema Jangwa la Lut ni kati ya maeneo ya kipekee duniani kwani kwa mtazamo wa kihidrolojia, jangwa hilo limetambuliwa kama eneo lenye joto jingi zaidi duniani.

Huku akiashiria kuwa dunia inashuhudia ongezeko la matumizi ya maji, mtafiti huyo anasema hatua zinapaswa kuchukuliwa kukidhi mahitaji ya maji ya watu kwa kuwekeza katika teknolojia mpya na pia kuboresha njia za kubana matumizi.

Hebu tafakari kuhusu nguo ambayo ina uwezo wa kupunguza au kuongeza joto mwilini kwa kutegemea hali ya hewa. Naam hilo litawezekana kufuatia utafiti unaoendelea katika Kituo cha Nano Teknolojia na Vitu Erevu nchini Ureno- CeNTI. Kituo hicho hivi karibuni kilitangaza kuunda kapsuli za nano ambazo zikitumika katika vitambaa zinaweza kuufanya mwili wa mwenye kuvivaa kuhisi joto au baridi kwa kutegemea hali ya hewa. Kapsuli hizo ndogo za nano teknolojia  zina uwezo wa kuvutia au kuachilia joto. Kapsuli hizo za nano ni nyembamba mara elfu kadhaa kuliko unywele wa mwanadamu na zimetengenezwa kwa wanga na mada inayoshabihiana na nta.

Mtafiti mkuu katika mradi huo ni Bi. Carla Silva ambaye anafanya tafiti mbali mbali kuhusu kuyafanya mavazi yawe na manufaa kamili kwa mwili wa mwanadamu pasina kuwa na madhara au kero. Dkt Silva amekuwa akifanya utafiti kwa muda wa miaka17 sasa katika Chuo Kikuu cha Minho ambapo utaalamu wake ni kemia ya vitambaa na anasema teknolojia mpya sasa inatumika kutengeneza nguo erevu.

Na wakaazi wa Afrika Mashariki wataweza kupata mihogo bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa kutokana na ushirikiano wa watafiti wa Kenya, Tanzania na Uhispania. Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Teknolojia na Kilimo (JKUAT) nchini Kenya pamoja na Kituo cha Utafiti wa Mazao ya Kilimo cha Mikocheni nchini Tanzania wakishirikiana na Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Kilimo ya Basque nchini Uhispania  wanachunguza njia za kuzalisha mihogo ambayo itaweza kustahamili mabadiliko ya tabianchi. Kwa kifupi tabianchi ni jumla ya halihewa zote zinazoweza kutokea mahali pamoja duniani katika kipindi kisichopungua miaka 30.

Mihogo iliyokaangwa

Mabadiliko ya tabianchi hutokea kieneo au hata duniani kote kila baada ya muda fulani. Mabadiliko hayo yanaweza kusababishwa na mabadiliko ya kiasi cha nuru ya jua inayofika duniani pamoja na mabadiliko katika angahewa ya dunia. Mabadiliko ya tabianchi yaliyojadiliwa sana tangu mwishoni mwa karne ya 20 yanahusu kuongezeka kwa gesi joto kutokana na shughuli za binadamu ambazo ni haribifu kwa mazingira. Hali hiyo hupelekea kuongezeka joto duniani, mafuriko, kiangazi n.k.

Sasa tukirejea katika mada yetu ya utafiti wa mihogo, watafiti hao wa Kenya, Tanzania na Uhispania wanalenga kuzindua mihogo ambayo itaweza kupambana na magonjwa ya mimea na pia kuweza kustahamili hali mbali mbali za hewa kama vile, joto, baridi na kiangazi.

Kiongozi wa timu ya watafiti hao ni Profesa Elijah Ateka wa Kitivo cha Kilimo cha JKUAT na anasema wanachunguza anuai za mihogo ambayo inaweza kukuzwa katika wakati wa kiangazi.  Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO na ni sehemu ya malengo ya Umoja wa Mataifa wa maendeleo endelvu kwa lengo la kuangamiza umasikini na njaa.

Mihogo imetambuliwa kama chanzo muhimu cha chakula kinachotegemewa na zaidi ya asilimia 20 ya watu wanaoishi Afrika, Asia na Amerika ya Kusini. Zao la mhogo  ni muhimu hasa kwa nchi za Afrika kwa sababu hufanya vizuri hata katika maeneo ambayo mchanga wake hauna rotuba ya kutosha na pia katika maeneo yenye mvua duni. Kwa kuwa mhongo unaweza kuvunwa wakati unapohitajika umetambuliwa kama chanzo cha kuimarisha usalama wa chakula.

 

Tags

Maoni