Jul 26, 2018 14:32 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (119)

Assalamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia moja ya tabia mbaya za kimaadili ambayo ni udaku na kuchukua maneno ya huku na kuyapeleka kule.

 

Tulieleza katika kipindi chetu hicho kilichopita kwamba, katika jamii yoyote mtu mwenye tabia ya umbea huchukiwa, hutengwa na hata wakati mwingine hupigwa kwa kuonekana kuwa ni chanzo cha migogoro na huku viongozi wa dini wakimwona mtu wa aina hiyo kuwa ni mtenda dhambi.  Tulinukuu hadithi kutoka kwa Imam Ali bin Abi Twalib AS ambaye amesema kuwa: Watu wabaya kabisa miongoni mwenu ni wale wanaochukua maneno ya huku na kuyapeleka kule na kuleta utengano baina ya marafiki na wanachunguza aibu na mapungufu ya watu wasafi. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 119 ya mfululizo huu kitazungumzia tabia nyingine ambayo nayo dhambi yake inatokana na ulimi na ambayo ni kutoa matusi na maneno machafu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

Moja ya dhambi za ulimi ni kutukana na kutoa lugha chafu jambo ambalo limekemewa mno katika hadithi na mafundisho ya Uislamu. Kutukana na kutoa matusi au kutumia lugha chafu ni katika tabia mbaya mno ambazo hupelekea kutokea vinyongo na uadui na wakati huo huo kuondoa mfungamano wa kihuba na kupendana baina ya wanadamu. Tukirejea mafundisho ya Uislamu tunapata kuwa yanawataka wafuasi wa dini hii kutumia lugha nzuri wanapozungumza na watu na kujiepusha na lugha chafu iliyoojaa kebehi na matusi. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Matusi na lugha chafu hushusha daraja na hadhi ya mtu na huondoa udugu na urafiki.

Ukweli wa mambo ni kuwa, moja ya ujazi na neema zenye thamani kubwa ambazo Mwenyezi Mungu amemtunuku mwanadamu ni ulimi. Lakini hata hivyo kama zilivyo neema nyingine, ulimi pia unaweza kutumiwa katika njia zisizo sahihi. Kwa maana kwamba, mtu anaweza kumtaja na kumdhukuru Allah kwa ulimi, akazungumza maneno matamu na ya kuvutia. Aidha mwanadamu kwa kutumia neema ya ulimi anaweza kuwaudhi watu wengine kwa kusema uongo, akasengenya, akatoa tuhuma na hata kuwatusi wengine na kuwashambulia kwa maneno machafu na yasiyofaa. Matumizi ya ulimi katika mambo yasiyofaa ni mengi mno kiasi kwamba, zimetajwa dhambi hadi 70 zinazotokana na kutumia vibaya ulimi. Moja ya dhambi hizo ni kutukana na kutoa matusi.

Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani

Kutusi au kutukana ni kutoa maneno machafu, kusema matusi, chamba au kushambulia kwa maneno na lugha chafu kitendo ambacho ni kibaya katika jamii yoyote ile. Kwa maana kwamba, kitendo hicho ni cha kuchukiza na huwa na matokeo mabaya. Katika istilahi kutusi kunaelezwa kuwa ni kutoa maneno machafu na mabaya ambayo hupelekea kumdhalilisha au kumuuudhi mtu mwingine au kuondoa heshima yake. Imam Ja'far Muhammad al-Swadiq as anasema: Kutukana ni kudhulumu na mwenye kudhulumu mafikio yake ni motoni. Mafundisho ya Kiislamu yanaonyesha kuwa, Mwenyezi Mungu atawaadhibu huko akhera kwa adhabu kali na inayoumiza watu wenye lugha chafu na wanaotoa matusi. Aidha baadhi ya riwaya zinaonyesha kuwa, kuna watu wa aina tatu ambao adhabu yao itapelekea kuongezeka adhabu ya watu wa motoni. Mmoja wa watu hao ni yule ambaye hapa duniani alikuwa akitoa matusi na lugha chafu kwa ajili ya kujiburudisha na kujifurahisha.

Mafundisho ya Uislamu yanabainisha kwamba, lugha chafu na matusi humuweka mbali mtu na Uislamu na wakati huo huo kumkurubisha na nifaki na ukafiri. Hadithi ifuatayo ya Bwana Mtume saw inathibitisha hilo ambapo mbora huyo wa viumbe amenukuliwa akisema: Matusi na lugha chafu si katika sifa za Uislamu." Hadithi hii inaonyesha kuwa, kutusi na kutoa maneno machafu ni jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na mafundisho ya Uislamu.

Aidha amenukuliwa katika hadithi nyingine akisema kuwa, kutusi na kutoa lugha chafu ni matawi mawili miongoni mwa matawi ya nifaki na kauleni yaani undumakuwili.

Watalaamu wa elimu za kimaadili wanaamini kuwa, chimbuko la matusi na mtu kuwa ni mtumiaji wa lugha chafu ni kuwa kwake na hali ya kuelekea upande wa upotofu wa mambo na kukengeka njia ya kiutu na kibinadamu. Ukweli ni kuwa, madhali mwanadamu hajajiweka mbali na utu na ubinadamu wake basi hujiepusha na matusi, lugha chafu na maneno yasiyofaa. Lakini pindi tu anapokengeuka na kuwa mbali na utu na ubinadamu wake na akaelekea upande wa mambo mabaya na machafu, basi kutoa lugha chafu, matusi na maneno yasiyofaa kwake hugeuka na kuwa jambo la kawaida kabisa.

Hadithi ya Uongofu

Tabia mbaya ya kutoa matusi na kutumia lugha chafu na mbaya kwa wengine mbali na kuwa na matokeo mabaya kwa mhusika hapa dunia, huwa na madhara makubwa na hatima mbaya zaidi Siku ya Kiyama. Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema: Mwenyezi Mungu ameharamisha pepo kwa kila mwenye kutoa matusi, asiye na heshima wala haya ambayehana woga wa kile anachokisema na hata kile anachoambiwa.

Aidha mbora huyo wa viumbe anasema katika hadithi nyingine kwamba:  Mtoa matusi ni haramu kwake kuingia peponi.

Kutukana na kutoa matusi au kutumia lugha chafu na mbaya huleta uadui, chuki na vinyongo na hivyo kuchukua nafasi ya upendo na utafiki. Wakati mwingine kutokana na neno moja baya na chafu, urafiki wa miaka mingi wa marafiki wawili au hata udugu wa ndugu wawili hukatika na kusambaratika milele. Inasimuliwa kwamba, siku moja Bwana Mtume saw alimuusia bwana mmoja kutoka kabila la Bani Tamim akimwambia: Usiwatusi na kuwatolea lugha chafu watu kwani hilo litapelekea wakufanyie uadui na uhasama.

Aidha imekuja katika wasia wa Kiongozi wa Wachamungu Ali bin Abi Twalib as: Msitumie matusi na lugha chafu katika maneno yenu, kwani matusi na lugha chafu ni mambo yasiyofaa kwetu na kwa wafuasi wetu; na mtu mwenye tabia ya kutoa matusihastahiki kufanywa rafiki.

Tabia hii kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu mbali na kuwa na matokeo mabaya katika mahusiano na hata mhusika kukumbwa na adhabu ya moto wa jahanamu baada ya kuharamishiwa pepo, hapa dunia pia haina hatima na matokeo mazuri. Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, tabia ya kutusia na kuwashambulia wengine kwa lugha chafu huondoa baraka katika maisha ya mtu. Imam Ja'far bin Muhammad al-Swadiq anasema: Mwenye kumtusi nduguye muumini, Mwenyezi Mungu humuondolea baraka katika riziki yake na kumtelekeza na hivyo maisha yake kukumbwa na dhiki.

Uislamu umebainisha pia njia za kuamiliana na watu wenye tabia ya kuwatusi wengine. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 63 ya Surat al-Furqan:

Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama!

Hivyo basi kwa mujibu wa aya hii, waumini wana jukumu la kuwajibu kwa wema na lugha nzuri wale wanaowatolea maneno machafu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo.

 

Maoni