Jul 27, 2018 07:33 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (120)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.  Kipindi chetu kilichopita kilijadili tabia mbaya ya kutoa matusi na lugha chafu.

 

Tulisema kuwa, tukirejea mafundisho ya Uislamu tunapata kuwa yanawataka wafuasi wa dini hii kutumia lugha nzuri wanapozungumza na watu wengine na kujiepusha na lugha chafu iliyoojaa kebehi na matusi. Tulikunukulieni hadithi kutoka kwa Imam Ja'far bin Muhammad al-Swadiq as inayosema: Kutukana ni kudhulumu na mwenye kudhulumu mafikio yake ni motoni. Mafundisho ya Kiislamu yanaonyesha kuwa, Mwenyezi Mungu atawaadhibu huko akhera kwa adhabu kali na inayoumiza watu wenye lugha chafu na wanaotoa matusi. Aidha tulieleza kwamba, tabia mbaya ya kutoa matusi na kutumia lugha chafu na mbaya kwa wengine mbali na kuwa na matokeo mabaya kwa mhusika hapa dunia, huwa na madhara makubwa na hatima mbaya zaidi Siku ya Kiyama. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 120 kitazungumzia suala la mzaha na utani. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

Moja ya sifa nzuri za muumini ni tabia njema na mwenendo mzuri. Mwenendo mzuri na kuamiliana vyema na watu kunajumuisha pia kufanya mzaha na utani na watu marafiki. Yunus Sheibani anasimulia kwamba, siku moja Imam Ja'far bin Muhammad al-Swadiq as aliniuliza: Mzaha na utani wako na watu wengine ukoje? Nikamwambia, ni kidogo na wa kiasi. Imam akaniambia: Kwa nini huna mzaha na utani na wengine? Utani na mzaha ni sehemu ya mwenendo mzuri na tabia njema.

 

Kwa mujibu wa mafundisho ya dini, waumini ni ndugu wa kidini hivyo wanapaswa kusaidiana katika dhiki na faraja. Kuna wakati kumfurahisha muumini katika mazingira magumu aliyonayo ni kitendo kinachopendeza zaidi kuliko kitu kingine. Imam Ali bin Abi Twalib as analitambua suala la kufanya utani na mzaha kuwa ni chimbuko la furaha na ukunjufu wa moyo katika moyo wa ndugu muumini. Imam Ali as anaashiria sira ya kivitendo ya Bwana Mtume saw na kusema: Kila mara Mtume saw alipokuwa akimuona mmoja wa masahaba zake ana ghamu na majonzi, alikuwa akimfurahisha kwa utani. Mafundisho ya kimaadili ya Uislamu yanamtaka muumini kuwa na uso wa bashasha na furaha anapokutana na ndugu yake muumini. Hii ni kusema kuwa, hata kama mtu ana matatizo yake, ghamu na mazonge anapaswa kujitahidi kuficha hali yake hiyo na asiidhihirishe kwa wenzake.

Miongoni mwa amali njema za kimaadili ambazo zimekokotezwa katika Uislamu ni kutia furaha katika moyo wa muumini. Imam Muhammad Baqir as amesema: Kwa hakika amali bora kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu mtukufu ni kuleta furaha katika moyo wa muumini.  Mtume saw anakitaja kitendo hicho kwamba, ni mithili ya kumrahisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Mbora huyo wa viumbe amenukuliwa akisema: Kila atayemfurahisha muumini, amenifurahisha mimi, na mwenye kunifurahisha mimi amemfurahisha Mwenyezi Mungu.

Inasimuliwa kwamba, mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Ummu Aiman alimwendea Bwana Mtume saw na kumwambia: "Mume wangu ana kazi na wewe". Mtume akamwambia, mumeo ndiye yule ambaye sehemu fulani ya jicho lake kuna weupe? Ummu Aiman akasema: Hapana! Sehemu ya jicho la mume wangu haina weupe. Mtume akasema: Basi mumeo ni yule ambaye macho yake yote mawili yana weupe? Mwanamke yule akajibu, hapana! Macho ya mume wangu hayana weupe. Mtume saw akacheka kwa upole na kusema: Je kuna mtu ambaye macho yake hayana weupe?

Hadithi ya Uongofu

 

Aidha katika kisa kingine mashuhuri, bibi kizee mmoja alikuja kwa Mtume saw. Mtume akamwambia, hakuna mzee ambaye atangia peponi. Bibi Kizee yule akalia. Mtume akamwambia, nakusudia kwamba, siku hiyo wewe hautakuwa mzee. Kwa maana kwamba, watu wote watakuwa vijana. Jambo hilo linaashiriwa na aya ya 35 na 36 za Surat al-Waqiah zinazosema:

"Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya, Na tutawafanya vijana."

Pamoja na hayo yote, Uislamu ni dini ya uwiano na kati na kati. Uislamu sio kama baadhi ya dini ambazo zimefungamana na mambo ya kidunia na kuacha mambo ya akhera na wala haikushikamana na mambo ya akhera tu na kuachana na mambo ya kidunia. Katika mzaha na utani pia, haipasi kufanya mzaha kupita kiasi na kufikia hatua ya kusema maneno mabaya na kumdhalilisha mtu.

Mtume saw anasema: Mimi ni mtu wa utani na mzaha; lakini wakati wa kutania sisemi isipokuwa maneno ya haki.

Endapo utani na mzaha utavuka mipaka huua moyo na hata kupelekea kutokea hasama na chuki ambazo hupelekea kuvurugika mahusiano mazuri yaliyokuwako. Imam Ja’afar bin Muhammad Swadiq as anasema kuwa: Mwenyezi Mungu anampenda mtu anayefanya mzaha na utani katika mkusanyiko wa watu kama jambo hilo halipelekei kutendeka dhambi.

Kwa hakika kama utani na mzaha utaondoka katika hali ya kati na kati na uwiano na kuvuka mipaka hupelekea udunishaji na maskhara na ni katika mazingira kama haya ambapo utani na mzaha hugeuka na kuwa ugomvi na uadui.

Imam Ja’afar bin Muhammad Swadiq as alimnasihi mmoja wa masahaba zake kwa kumwambia: Kama unataka urafiki na ndugu yako uwe msafi na usio na uchafu, basi usifanye utani, majadiliano, kujifakharisha na mivutano.

Hivyo basi ili mahusiano mema baina ya wanajamii yaweze kubakia na kudumu iwe ni baina ya marafiki wawili au ndugu wawili, kuna haja ya kujiweka mbali na aina yoyote ile ya uchupaji mipaka katika kufanya utani na mzaha. Aidha wakati mtu anafanya mzaha au utani na mwenzie anapaswa kuchunga namna ya kufanya utani na aina ya utani wenyewe ili asije akamdhalilisha mwenzake na kumdunisha.

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kisa kifupi kifuatacho:Abu Basir anasimulia kwa kusema kuwa:

Nilikuwa katika msikiti wa Kufa nikimfundisha Qur’ani mwanamke mmoja. Ghafla moja nikawa nimefanya naye mzaha na utani. Ukapita muda, kisha siku moja nikapata fursa ya kumtembelea Imam Muhammad Baqir (a.s) mjini Madina. Imam akanilaumu kwa kitendo changu kile. Niliona haya na kuinamisha kichwa changu chini. Imam Baqir (a.s) akasema: Fanya toba, na usifanye tena utani na mzaha na mwanamke ambaye si maharimu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu umefikia tamati kwa leo, basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni huku nikitaraji kwamba, mmenufaika na yale niliyokuandalieni kwa leo.

 

 

 

Maoni