Aug 04, 2018 12:42 UTC
  • Watafiti Wairani wabuni njia mpya ya kutibu saratani

Karibuni katika makala hii ambayo huangazia mafanikio katika uga wa sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani.

Hivi karibuni wanasayansi Wairani walifanikiwa kubuni njia mpya ya kutibu ugonjwa wa saratani. Watafiti Wairani katika Kitivo cha Teknolojia Mpya za Kitiba katika Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba Iran wamefanikiwa kuibua harakati katika  seli za kinga na kubuni mbinu mpya ya kutibu saratani ya Neuroblastoma. Kwa kifupi saratani ya Neuroblastoma  ni aina moja ya kawaida ya uvimbe ambao hutokea miongoni mwa watoto. Watafiti Wairani wamefanikiwa kuibua harakati katika seli seli salama za kinga ambazo zimekabiliana na seli za saratani na kufanikiwa kuziangamiza kwa kiasi kikubwa.

Watafiti wa mradi huu wanasema seli ambazo dhati yake na kuhami ni seli za kinga ambazo huwa mstari wa mbele katika kukabiliana na hujuma ya seli za saratani. Baadhi ya wakati seli za saratani hufanikiwa kukwepa seli hizi kinga na hata kuzifanya zisiweze kufanya kazi na hivyo kupelekea seli hizo za saratani kuenea. Ndani ya mwili kuna seli mbali mbali ambazo kwa kutumia mbinu ya exosomal hupata uwezo wa kuwasiliana. Kwa mujibu wa mbinu mpya ya wanasayansi Wairani walioifanyia majaribio, kupitia Exosomal, seli za kinga zenye uwezo wa kuangamiza  seli mbaya huwasiliana na seli za saratani ya Neuroblastoma na kuuweza kuziondoa. Uchunguzi huo umebaini kuwa seli za kinga zikiwa katika harakati zinaweza kutumia uwezo mkubwa zilizonao na kuangamiza seli za saratani za Neuroblastoma.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangazwa kuwa nchi ya kiongozi miongoni mwa mataifa ya Kiislamu duniani katika uga wa uzalishaji wa sayansi.

Hayo yamedokezwa na mkuu wa Kituo cha Marejeo ya Sayansi katika Ulimwengu wa Kiislamu (ISC) Dkt. Mohammad Javad Dehqani.

Dehqani amesema kwa mujibu wa data ya Taasisi ya Taarifa za Kisayansi (ISI), Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya kwanza miongoni mwa nchi za Kiislamu katika uzalishaji wa sayansi. Amesema Iran imeweza kuchangia asilimia 22 ya uzalishaji wa kisayansi katika nchi za Kiislamu. Hivi karibuni aidha, mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Iran Murtadha Barari alisema Iran inashika nafasi ya kwanza miongoni mwa nchi za eneo la Asia Magharibi katika uga wa sayansi za anga za mbali.

Wanafunzi Wairani wamefanikiwa kupata medali 40 katika Mashindano ya Kimataifa ya Hisabati (WMI) na hivyo kushika nafasi ya pili katika mashindano hayo ambayo yalifanyika kuanzia 12 hadi 16 Julai katika Chuo Kikuu cha Yonsei mjini Seoul, Korea Kusini.

Wanafunzi 54 wa kike na kiume kutoka Iran walishiriki katika mashindano  hayo ya hisabati ambapo walipata medali 8 za dhahabu, 18 za fedha, 17 za shaba na diploma 14 za kifahari. Mashindano hayo yam waka 2018 yalikuwa na washiriki kutoka nchi 20 za maeneo yote ya dunia.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mashindano ya Kimataifa ya Hisabati (WMI), mashindano hayo hufanyika kwa lengo la kustawisha hesabati na kuwawezesha wanafunzi kubadilishana mawazo na pia kuchangia maelewano baina ya tamaduni. Mashindano ya Kimataifa ya Hisabati (WMI) yalianzishwa mwaka 2013 na hujumuisha wanafunzi kutoka shule za  chekechea hadi shule za upili au sekondari.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanzimia kuimarisha uhusiano wake wa biashara ya kiteknelojia na bara la Afrika.

Idara ya Uhusiano wa Kimataifa katika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya Sayansi na Teknolojia imetangaza mpango wa kutuma ujumbe  Afrika Mashariki kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa Iran na  nchi za eneo hilo katika uga wa sayansi na teknolojia.

Kwa mujibu wa taarifa, ujumbe huo utajumuisha wawakilishi wa mashirika yenye msingi wa elimu yaani knowledge-based, mashirika ya kiteknolojia ambayo yanajisghulisha na teknolojia za kilimo, afya, viwanda, ujenzi, uchimbaji madini n.k. Ujumbe huo unatazamiwa kuzitembelea nchi za Kenya, Uganda na Ethiopia.

Watafiti Wairani katika Chuo Kikuu cha Ferdowsi katika mji wa Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran wamefanikiwa kuvumbua spishi mpya za viumbe  wa baharini katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.

Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Ferdowsi cha Mashhad, uvumbuzi huo ni sehemu ya utafiti uliofanywa na Fatima Nazari, mwanafunzi wa chuo kikuu hicho katika taaluma ya biosystematiki ya wanyama. Utafiti wa Bi. Nazari umefanywa chini ya usimamizi wa Dkt. Omid Mirshamsi na kwa ushauri wa Dkt. Pedro Martinez Arbizu wa Jumba la Makumbusho la Naturemuseum Senckenberg  ambalo limejikita katika historia ya maumbile huko Frankfurt am Main, Ujerumani.

Utafiti huo umepelekea kuvumbuliwa spishi mpya za familia ya Canuellidae Lang. Spishi hizo tatu mpya zimepewa majina ya Brinaola haliensis, Canuella persica na Scottolana gomezi. Makala kuhusu utafiti huo umechapishwa katika jarida la Zootaxav Julai 2018.

Na wiki hii Maonyesho ya 24 ya Kimataifa ya Teknolojia ya Mawasiliano, Kompyuta na Biashara ya Intaneti ya Iran yameanza Jumamosi mjini Tehran na kuhudhuriwa na makampuni kutoka nchi 20 duniani.

Sherehe za ufunguzi wa maonyesho hayo zimehudhuriwa na Sorena Sattari, Naibu Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia na Mohammad Jawad Azari Jahromi, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Mawasiliano.

Maonyesho ya mwaka huu ya ELECOMP, ambayo ndiyo makubwa zaidi ya Iran yanayoonyesha bidhaa na huduma za  teknolojia ya mawasiliano, yanafanyika kuanzia Julai 28 hadi 31. Kuna mashirika 400 ya startup, mashirika 24 ya kiserikali na kwa mara ya kwanza zaidi ya mashirika 30 ya Kiirani yanayojihusisha na utengenezaji michezo ya kompyuta.

Maonyesho ya ELECOMP yalifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1995 na yamekuwa yakiimarika kila mwaka jambo ambalo linaashiria ustawi wa kasi wa Iran katika sekta za sayansi na teknolojia.

Wiki hii wanasayansi Wairani walitangaza kuunda na kuzindia mfumo ambao unaweza kuimarisha uwezo na utendajikazi wa mabati ya kunasia mwanga wa jua (solar panel) kwa kutumia teknolojia ya maji ya nano.

Bi. Reyaneh Loni, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Mohaghegh Ardabili (UMA) amesema bati ya kunasa mwanga wa jua lenye kipokezi chenye muundo wa bomba kilitumika kama chanzo cha joto katika utafiti huo.

Amesema mbinu hiyo aliyovumbua inapunguza kupotea nishati ya jua inapokusanywa  na hivyo kuimarisha utendaji kazi wa mabati ya kunasa mwanga wa jua.

Kwa mujibu wa Loni, maji ya nano yanaweza kuhamisha nishati ya kujia pasina kuwepo israfu kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuhamisha umeme.

Katika miaka ya hivi karibuni Iran imeimarisha jitihada zake za kuzalisha nishati jadidika badala ya kutegemea vyanzo vya nishati vya fosili kama vile mafuta ambayvo ni haribifu kwa mazingira.

Hivi sasa Iran inajenga vituo vitatu vikubwa vya nishati ya jua na kimoja kiko katika mkoa wa Ardabil kaskazini magharibi mwa Iran. Chuo  Kikuu cha Mohaghegh Ardabili (UMA) kiko katika mkoa huo.

 

 

 

 

 

 

 

 

Tags

Maoni