Aug 10, 2018 08:13 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (122)

Ni wasaa na wakati mwingine mpenzi msikilizaji wa kujiunga nami Salum Bendera katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kwa wale wafuatialiaji wa kipindi hiki wanakumbuka kwamba, wiki iliyopita tulijadili moja ya sifa mbaya ya kimaadili nayo ni ya kujikomba na kujipendekeza kwa wengine.

 

Tulisema kuwa, kujikomba na kujipendekeza ni katika dhambi za ulimi. Mtu mwenye kujikomba si tu kwamba, huwa amekumbwa na tabia hii mbaya ya kimaadili bali hutumbukia katika tabia nyingine mbaya kama za kusema uongo, ria na kujionyesha na kujikweza ambazo zote hizi ni katika sifa na tabia mbaya za kimaadili. Tulibainisha jinsi Imam Ali as alivyoeleza kuwa, moja ya vigezo vya urafiki wa kweli baina ya marafiki wawili ni kujiepusha na kujikomba na kujipendekeza.

Kwa maana kwamba, rafiki wa kweli ni yule ambaye hajikombi na kujipendekeza kwa ajili ya maslahi yake. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 122 ya mfululizo huu kitazungumzia tabia nyingine mbaya na isiyofaa nayo ni “kusema sana”. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Wapenzi wasikilizaji, vipindi vyetu kadhaa vilivyopita vya mfululizo huu tulizungumzia madhara ya kutumia vibaya ulimi ambao ni moja ya neema kubwa na muhimu za Allah kwa kiumbe mwanadamu. Hapana shaka kuwa, endapo ulimi utatumiwa vyema utakuwa wenzo wa mwanadamu kukwea kidaraja na kuboresha mahusiano yake na wengine katika jamii anayoishi. Kutokana na kuwa, ulimi unaweza kuwa chimbuko la dhambi nyingi, mwanadamu anapaswa kuwa makini na kuchunga mno ulimi wake na anapaswa kujikumbusha kila siku juu ya umuhimu wa kuchunga na kuudhibiti ulimi wake. Kwani kiungo hiki kama kitatumiwa vyema kinaweza kumfikisha mwanadamu katika kilele cha saada na ufanisi, kama ambavyo endapo kitatumiwa vibaya kitamfikisha mja katika hatua mbaya ya uovo, madhila na hatimaye kuharibikiwa hatima yake.

"Kunyamaza ni hekima na ujamali"

 

Kuhusiana na jambo hilo Imam Sajjad as anasema:  Kila asubuhi ulimi wa mtu huwa mwangalizi wa viungo vingine vyote vya mwili wake na kusema: Mkoje? Mmeamkaje? Viungo hivyo hujibu kwa kusema, tuko salama kwa sharti kwamba, utuache na usitufuatefuate. Kisha viungo hivyo vinauapisha ulimi na kuuambia, usiseme maneno mahala si pake na hivyo kuvitia viungo vingine katika mashaka na taabu. Viungo hivyo vinaendelea kusema:  Hapana shaka kuwa, kwa sababu yako wewe ulimi, sisi tunapata ujira na thawabu na ni kwa sababu yako wewe tunahukumiwa.

Wapenzi wasikilizaji miongoni mwa mambo yenye madhara yanayotokana na ulimi ni kusema maneno yasiyo na faida ambayo hayana sudi na faida kwa dunia wala akhera.

Hata kama kuzungumza sana au kusema maneno yasiyo na faida duniani na akhera kisheria si haramu, lakini kimaadili ni jambo baya na lisilopendeza. Hii ni kutokana na kuwa, hatua hiyo huwa ni kupoteza wakati bure bilashi na hivyo kuufanya umri wa mtu ambao ni rasilimali muhimu hapa duniani kupotea bure.

 Kuzungumza sana hufikia katika hatua ya hatari na mbaya pale inapotokea kwanza, mtu anayezunguma sana anasema uongo, anasengenya au kutoa tuhuma na mambo mengine mfano wa hayo ambayo kimsingi ni haramu katika Uislamu. Imam Ali bin Abi Twalib as amesema: Jiepushe na kusema sana, kwani kila mwenye maneno mengi, dhambi zake huongezeka.

Katika hadithi nyingine imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume saw ya kwamba amesema: Mwenyezi Mungu atauadhibu ulimi kwa adhabu ambayo hajakiadhibu kiungo kingine chochote. Ulimi utalalamika na kusema: Ewe Mola wangu! Unaniadhibu kwa adhabu ambayo hujakiadhibu kiungo kingine chochote? Mwenyezi Mungu atajibu kwa kusema: Ndio! Maneno yalitokea kwako na yakaenea na kuwafikia watu wa mashariki na magharibi mwa dunia na kwa maneno yako hayo, damu ikamwagwa kwa njia ya haramu, mali ikaporwa… ninaapa kwa izza, utukufu na adhama yangu kwamba, kwa hakika ninakuadhibu kwa adhabu ambayo sikiadhibu kiungo kingine chochte kwa adhabu hii.

"Kusema sana ni ishara ya udhaifu wa akili"

 

Kikawaida kuzungumza sana ni katika madhara ya ulimi ambayo hayazingatiwi sana na watu. Kwani wakati mwingine upweke wa mtu, kuchoka au fikra zake zisizofaa huwa chimbuko la kusema sana. Hata hivyo katika vitabu vya Kiislamu, kuzungumza sana kumewekwa katika orodha ya ujinga, ukosefu wa akili na kutokuwa na hekima.

Mfano wa wazi ni hadithi ya Imam Ali as ambaye amenukuliwa akisema: Wakati akili inapokamilika, maneno hupungua.

Hadithi hii inatufunza kwamba, mtu mwenye akili timamu kikawaida si mwenye kuzungumza sana na ikitokea mtu anazungumza sana basi fahamu kwamba, akili yake iko pungufu. Kwa msingi huo basi, kuna uhusiano wa pande mbili kama ulivyo mzani baina ya uhakika wa akili na maneno kama vile mzani wa kupimia uzito na kama akili itakuwa nyingi maneno hupungua na kama maneno yatakuwa mengi basi akili hupungua.

Wapenzi wasikilizaji mwanadamu ana jukumu na masuuliya mkaba na amali na matendo yake yote. Ndio maana tunapaswa kuwa makini juu ya maneno tunayoyazungumza kwani kila neno linalotoka katika vinywa vyetu huandikwa katika kitabu cha amali zetu. Aya ya 18 ya Surat Qaaf inabainisha hilo kwa kusema: Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari

Hadithi ya Uongofu

Inanukuliwa kwamba, Bwana mmoja alikwenda kwa Bwana Mtume saw na akawa akiongea sana. Mtume saw akiwa na lengo la kuzuia kitendo chake hicho alimuuliza: Ulimi wako una milango mingapi? Bwana yule akasema, una milango miwili, mlango wa kwanza ni midomo na mlango wa pili ni meno. Mtume akasema, je milango hii haina uwezo wa kuzuia kwa kiwango fulani hii hali yako ya kuzungumza sana? Kisha mbora huyo wa viumbe akasema: Zingatieni kwamba, hakuna mtu hapa duniani ambaye amepatiwa kitu kwa ajili ya akhera yake ambacho kina madhara kuliko ulimi, na ulimi huo ni ule ulioachwa na kutelekezwa ambao unazungumza sana na kusema maneno yasiyo na maana.

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kunukuu hadithi kutoka kwa Imam Ali bin Abi Twalib as ambaye amesema: Neno litakuwa katika udhibiti wako madhali bado hujalitamka kwa ulimi, lakini ukishalisema, utakuwa katika minyororo ya matokeo yake mabaya. Filihali, uchunge na kuuhifadhi ulimi wako kama dhahabu na fedha zako. Jizuie kusema kila usichokijua. Mwenyezi Mungu amewajibisha mambo kwa viungo ambayo atayauliza Siku ya Kiyama…Kila mwenye kusema sana, makosda yake nayo hukithiri na kila ambaye yuko hivi haya na soni yake hupungua, basi hofu ya kujitenga na dhambi nayo hupunngua na hivyo moyo wake hufa. Na kila ambaye moyo wake umekufa ataingia katika moto wa Jahanamu.

Wassalaamu Alayakum Warahmatullahi Wabarakkaatuh….

 

Tags

Maoni