Aug 21, 2018 02:53 UTC
  • Jumanne tarehe 21 Agosti, 2018

Leo ni tarehe 9 Dhulhija 1439 Hijria sawa na Agosti 21, 2018.

Leo ni siku ya Arafa tarehe 9 Dhil-Hija. Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na mlima wa Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, husimama katika uwanja wa Arafa na hadithi nyingine za Kiislamu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho. Hadithi zinasema kuwa Mwenyezi Mungu SW ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahala pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hija na ameweka meza na karamu yake pembeni ya mlima wa Jabalur Rahma. Ni vyema kukumbusha kuwa magharibi ya siku hii ya leo mahujaji wanaondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hija.

Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita, Muslim bin Aqil, binamu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS aliuawa shahidi mjini Kufa Iraq. Alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa na wacha Mungu katika zama zake. Alielekea mjini al-Kufa, Iraq akiwa na lengo la kwenda kutathmini ni kwa kiwango gani watu wa mji huo walikuwa wakimtii Imam Hussen, baada ya watu wa mji huo kumwandikia maelfu ya barua Imam huyo wakimtaka aende mjini humo na kwamba wako tayari kumuunga mkono katika harakati yake dhidi utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya. Watu wa Kufa walimsaliti Muslim bin Aqil baada ya kuhadaika kwa hila na uongo wa Ubeidullah bin Ziyad, mtawala wa wakati huo wa Kufa na wakamuacha Muslim bin Aqiil peke yake.

Haram ya Muslim bin Aqiil, Kufa Iraq

Siku kama ya leo yaani tarehe 30 Mordad katika kalenda ya mwaka wa Kiirani ni siku ya kumuenzi na kumkumbuka Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu. Baba yake Allamah Majlisi alipata elimu kwa msomi mkubwa wa Kiislamu Sheikh Bahai. Umahiri wa Sheikh Majlisi ulianza kuonekana akiwa bado kijana na alipata ijaza au ruhusa ya kunukuu hadithi kutoka kwa msomi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu Mulla Sadra akiwa na umri wa miaka 14 tu. Allamah Majlisi ameandika vitabu vingi wakati wa uhai wake ambavyo hii leo ni marejeo ya Waislamu. Katika kipindi cha uhai wake Allamah Muhammad Baqir Majlisi alifanya hima kubwa kuhakikisha kuwa Swala za Ijumaa na jamaa zinatekelezwa. Vilevile alifanya juhudi za kuasisi shule za masomo ya kidini na kueneza hadithi za Mtume wa Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Idadi ya vitabu vilivyoandika na Allamah Muhammad Baqir Majlisi imetajwa kuwa zaidi ya 600 na umashuhuri zaidi ni kile kinachojulikana kwa jina la Biharul Anwar. Vitabu vingine mashuhuri vya msomi huyo ni Hayatul Quluub, Ainul Hayat na Zadul Maad.

Allamah Muhammad Baqir Majlisi

Miaka 891 iliyopita, aliaga dunia Fadhl bin Hassan Tabarsi anayejulikana kwa lakabu la Aminul Islam, alimu, mpokeaji wa hadithi na mfasiri mkubwa wa Kiislamu. Fadhl bin Hassan Tabarsi alikuwa mwanazuoni mkubwa na alikuwa akiheshimiwa na makundi mengi ya Kiislamu. Sheikh Tabarsi pia alikua miongoni mwa makadhi waadilifu katika zama zake. Kitabu muhimu zaidi cha msomi huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani ya Majmaul Bayan yenye juzuu kumi. Vilevile ameandika tafsiri nyingine ya Qur'ani aliyoipa jina la Jawamiul Jamii.

Tafsiri ya Majmau'l Bayaan

Tarehe 21 Agosti mwaka 1965 yaani katika siku kama hii ya leo miaka 53 iliyopita Wamarekani wenye asili ya Afrika katika mji wa Alabama walifanya maandamano wakitaka kutekelezwa sheria ya haki ya kupiga kura. Maandamano hayo yalizidisha harakati ya vuguvugu la kupigania haki za kijamii za Wamarekani weusi. Harakati hiyo ilianza mwaka 1955 kwa lengo la kupigania usawa kati ya Wamarekani weusi na wazungu na ilimalizika mwaka 1968 baada ya kupasishwa sheria ya haki za kiraia.

Harakati ya kupigania haki za kiraia Marekani

Siku kama ya leo tarehe 21 Agosti miaka 59 iliyopita, iliasisiwa The Central Treaty Organization ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Cento na kuchukua nafasi ya mkataba wa Baghdad. Taasisi hiyo iliundwa na Iran, Uturuki, Pakistan na Uingereza mjini Ankara, Uturuki. Japokuwa Marekani haikuwa mwanachama rasmi wa Taasisi ya Cento na ilishiriki kwenye vikao vya jumuiya hiyo kama mtazamaji tu, lakini ilikuwa na nafasi kuu katika maamuzi yote ya taasisi hiyo. The Central Treaty Organization ilivunjika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kujiondoa nchi hiyo katika mkataba huo mwaka 1979.

Mkataba wa The Central Treaty Organization

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, inayosadifiana na 21 Agosti 1969, Masjidul Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu, kilichomwa moto na Wazayuni. Katika tukio hilo, eneo hilo takatifu na la kihistoria liliharibiwa vibaya sana. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Utawala huo wa Kizayuni ulitayarisha mahakama ya kimaonyesho tu mjini Tel Aviv, na kuchukua uamuzi wa kumuachilia huru mtuhumiwa huyo kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili. Baada ya kutokea kitendo hicho, nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC. 

Msikiti wa al Aqsa ulichomwa moto na Wazayuni wa Israel

Na miaka 504 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea mapigano ya kihistoria ya Chaldoran kati ya Iran na dola la Othmania katika eneo la bonde lililoko kati ya Tabriz na Khoui, kaskazini magharibi mwa Iran. Mapigano hayo yalikuwa kati ya wapiganaji wa Shah Ismail Safawi na vikosi vya Sultan Salim Othmani.

Mapigano ya kihistoria ya Chaldoran

 

Tags

Maoni