Aug 21, 2018 12:59 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (123)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo mpenzi msikilizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia suala na "kusema sana". Tulisema kuwa, kutokana na kuwa ulimi unaweza kuwa chimbuko la dhambi nyingi, mwanadamu anapaswa kuwa makini na kuchunga mno ulimi wake kwani kiungo hiki kama kitatumiwa vyema kinaweza kumfikisha mwanadamu katika kilele cha saada na ufanisi, kama ambavyo endapo kitatumiwa vibaya kitamfikisha mja katika hatua mbaya ya uovo, madhila na hatimaye kuharibikiwa hatima yake. Wapenzi wasikilizaji miongoni mwa mambo yenye madhara yanayotokana na ulimi ni kusema maneno yasiyo na faida ambayo hayana sudi na faida kwa dunia wala akhera. Kadhalika tuliona jinsi hadithi nyingi zinavyoeleza kwamba, kuzungumza sana ni ishara ya upungufu wa akili. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 123 kitazungumzia suala la kulaani na kutoa kutoa laana. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa pamoja nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo.

 

Laana au kulaani ni apizo atoalo mtu kwa mtu mwingine ili afikwe na jambo baya. Kulaani au kutoa laana ni katika amali na matendo ya ulimi. Kitendo hiki kimegawanyika katika sehemu mbili. Kwa maana kwamba, kulaani kinaweza kuwa kitendo hasi na wakati mwingine kikawa ni chanya na cha mahala pake. Hii ni kusema kuwa, kama laana itatolewa mahala pake panapostahiki huwa chimbuko la mtu kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Lakini kama kulaani na kutoa laana kutakuwa si pa mahala pake huwa na matokeo mabaya na humfanya mhusika kuwa mbali na rehema za Mwenyezi Mungu SWT.

Dini ya Uislamu imejengeka juu ya msingi wa huba na upendo. Hata hivyo suala la kufanya urafiki na marafiki na kufanya uadui na maadui nao ni katika msingi jumla katika tamaduni zote na katika dini mbalimbali. Ukweli ni kuwa, huba na kupenda mambo mazuri na kuchukia mambo mabaya ni mambo ambayo yapo katika dhati na maumbile ya mwanadamu. Kwa maana kwamba, katika hali ya kawaida mwanadamu hupenda mambo mazuri na kuchukia mambo mabaya. Kwa mfano mwanadamu anapenda wema na kuchukia ubaya, anapenda uukweli na kuchukia uongo, anapenda ukarimu na kuchukia uchoyo, anapenda uadilifu na kuchukia dhulma na kadhalika. Hii ni fitra na maumbile ya mwanadamu. Uislamu nao ukiwa ni dini ya fitra na maumbile umesisitiza juu ya urafiki na uadui. Mwislamu anapaswa kuonyesha mapenzi na chuki yake mbele ya haki na batili, uadilifu na dhulma, kheri na shari na kadhalika.  Kwa hakika kulaani ni radiamali ya kihisia kwa ajili ya kuonyesha ghadhabu, chuki na uadui kwa dhulma au ukiukaji wa ahadi wa madhalimu!

Qur'ani Tukufu

 

Mwenyezi Mungu anaashiria matokeo mabaya ya kuvunja ahadi katika aya ya 13 ya Surat al-Maidah:

Basi kwa sababu ya kuvunja agano lao tuliwalaani, na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu.

Aidha tunasoma katika Ziyarah Ashura au ziyara ya Imam Hussein AS mjukuuu wa Bwana Mtume saw aliyeuawa shahidi na jeshi la Yazid bin Muawaiya katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria kwamba:

فَلَعَنَ اللَّهُ اُمَّةً اَسَّسَتْ اَساسَ الظُّلْمِ وَ الْجَوْرِ عَلَیْکُمْ اَهْلَ الْبَیْتِ

"Mwenyezi Mungu aulaani umma ambao uliasisi dhulma na uonevu kwenu nyinyi watu wa Nyumba ya Mtume saw".

 

Baadhi ya watu ambao kidhahiri ni waumini hughadhibika wanapopatwa na ugumu kidogo au mashinikizo na hivyo hutoa maneno mabaya na hata laana na kuona kama dunia imewageukia au kama watu waliolaaniwa na kutokuwa na bahati. Kwa vyovyote itakavyokuwa kitendo cha kulaani si katika matendo stahiki kwa waja wema na wastahiki wa Mwenyezi Mungu. Kwa maana kwamba, waja wema ni wale ambao hushikamana na subira na uvumilivu kutokana na mitihani au masaibu yaliyowakumba na katu si wenye kutoa maneno mabaya na laana. Mtume saw anasema kuhusiana na hilo kwamba: Muumini si mwenye kutoa laana.

Hivyo basi waumini wanapaswa kuwa na insafu. Endapo kumetokea dhulma na uonevu katika hatua ya awali ni kuomba dua za kheri na kisha kufanya kila liwezekanalo kuwapa mwongozo watu waliopotea. Baada ya hatua hiyo kama bado wataendelea kung'ang'ania vitendo vyao vya kufanya dhulma na ushari basi hapo inawezekana kuwatolea laana na kuwaombea wafikwe na mabaya. Kwa msingi huo basi, kutoa laana ni jambo lililokemewa katika Uislamu ukitoa katika baadhi ya sehemu, Waislamu wametakiwa kujiweka mbali na tabia ya kuwalaani watu wengine na kuwaombea wafikwe na ubaya.

 

Imam Muhammad Baqir AS amenukuliwa akisema: Mtu ambaye anamlaani mwenzake, ikiwa mtu yule hastahiki laana, laana ile hurejea kwa aliyeitoa. Hivyo jiepuusheni kumlaani Muumini, ili isije laana hiyo ikakupateni wenyewe.

Kadhalika Imam Ja'afar bin Muhammad al-Swadiq as amenukuliwa akisema kuwa:  Mwenyezi Mungu amesema, naapa kwa utukufu wangu kwamba, sitakabali dua ya aliyedhulumiwa kuhusiana na dhulma aliyotendewa endapo yeye mwenyewe amemfanyia mtu mwingine dhulma kama hiyo hiyo.

 

Hivyo basi kupitia hadithi tulizokunukulieni inafahamika wazi kwamba, mtu anapaswa kuwa makini kabla ya kutoa laana na kabla ya kulaani awe na uhakika kwamba, mtu anayetaka kumlaani anastahiki laanna za Allah. Kwani kama hastahiki na amemlaani basi hilo ni jambo lisilofaa na laana hizo zitamrejea mwenyewe.

Aidha Imam Muhammad Baqir AS amenukuliwa akisema katika hadithi nyingine kwamba: Laana inapotokana katika kinywa cha mtu, huanza kuzunguka baina ya mtoa laana na mtu aliyelaaniwa. Kama aliyelaaniwa anastahiki laana hiyo basi humfikia, lakini kama hastahiki laana hiyo hurejea kwa mwenyewe (kwa aliyeitoa).

Kwa msingi huo basi, laana ina athari zake. Kama laana itakuwa sio ya haki na si ya mahala pake humrejea aliyeitoa. Ndio maana hadithi nyingi zinakataza kuwalaani waumini kwani laana hiyo huwarejea walioitoa.

Kulaani kwa hakika ni aina fulani ya kulipiza kisasi kwa mtu aliyekudhulumu. Katika mafundisho na utamaduni wa Kiislamu kusamehe ni jambo linalopendekezwa zaidi kuliko kulipiza kisasi. Waumini wanausiwa watangulize msamaha kwa yule aliyewatendea ubaya na kuwadhulumu, badala ya kutaka kulipiza kisasi licha ya kuwa huenda kulipiza kisasi ikawa ni haki yao kisheria.   Kwa msingi huo basi si laiki na haifai kwa Muumini kumlaani Muumini mwenziwe na kumtakia jambo baya. Katika baadhi ya riwaya, tabia ya mtu kumlaani muumini mwenzie inatajwa kuwa miongoni mwa sifa mbaya kabisa za kimaadili na ndio maana imekokotezwa na kuusiwa mno katika Uislamu kwamba, waumini wanapaswa kujiepesha na tabia hii mbaya ya kimaadili.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo.

Hadi tutakapokutana tena wakati mwingine, kwaherini…

 

Maoni