Sep 03, 2018 07:55 UTC
  • Wanasayansi Wairani wabuni njia ya kutibu saratani ya kongosho

Makala hii huangaiza mafanikio ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani.

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Shiraz ,Iran kwa kutumia teknolojia ya nano, wamefanikiwa kutengeneza dawa ya walio na saratani ya kongosho ambayo matumizi yake hayana madhara kwa mwili.

Saratani ya Kongosho ni sababu kuu ya nne ya vifo vinavyotokana na saratani na matibabu yake hutegemea upasuaji, tiba ya kemikali (chemotherapy) au tiba ya mionzi (Radiotherapy). Matibabu kwa kutumia mbinu hizo wakati mwingi huwa hayana mafanikiko na kwa msingi huo watafiti wanatafuta njia mbadala za matibabu kama vile kutumia dawa maalumu ambazo zinatumia njia erevu kufikisha dawa katika uvimbe wa saratani pasina kuathiri viungo vingine vya mwili.

Kwa mujibu wa mmoja wa watafiti katika mradi huo, dawa inayojulikana kama Erlotinib leo ni kati ya dawa maarufu za kutibu saratani ya Kongosho. Pamoja na faida nyingi za dawa hii ya Erlotinib, lakini haijaweza kufanya kazi katika miili ya baadhi ya wagonjwa. Mbali na hayo baadhi ya wagonjwa wamepata madhara mengine katika mwili kutokana na kutumia dawa kama vile ya matatizo ya tumbo, ngozi na macho.

Katika mradi wa wanasayansi Wairani wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Shiraz, chembe za nano zilizoundwa kwa proteini zimetumika kusheheni dawa ya Erlotinib katika eneo lenye uvumbe wa saratani. Albumin ni aina ya protini ambayo imetumiwa na watafiti wa mradi huu kuwezesha chembe za nano kubeba dawa ya Erlotinib. Na kutokana na kuwa haina mada ya sumu, imebainika kuwa bora kuliko mbinu zingine mshabaha. Matokeo ya utafiti huo wa Wairani yamechapishwa katika jarida la International Journal of Pharmaceutics toleo 3.649.

Matuta barabarani kuzalisha umeme

Katika mafanikio mengine, hivi karibuni wanasayansi Wairani katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Amir Kabir hapa Tehran wamefanikiwa kuunda matuta barabarani yanayojulikana kama HEGSB ambayo yana uwezo wa kuzalisha nishati. Kwa kawaida matuta barabarani hutumika kwa ajili ya kuzuia kasi ya magari katika maeneo hatari barabarani na hivyo kuimarisha usalama kwa watumizi. Matuta barabaani yenye kuzalisha nishati yanaweza kutumika kukidhi baadhi ya mahitaji ya umeme ya maeneo kama vile vijwanja vya ndege, bandari, mataa ya barabarani na hata umeme ziadia huweza kuingia katika gridi ya kitaifa.

Kimsingi wataalamu wameweza kuzalisha nishati kupitia matuta barabarani kwa kutegemea miale ya jua na pia kwa kutegemea nishati inayotokana na kupita magari au vyombo vya kusafiria vinavyotumia barabara.

Mkutano wa Drone wafanyika Tanzania

Mkutano wa kimataifa wa kutumia ubunifu wa ramani mtandaoni kwa kutumia picha zilizopigwa na ndege zisizokuwa na rubani au drones, umefanyika  jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, ukiwaleta pamoja wadau zaidi ya 1000 kutoka nchi mbalimbali duniani.  

Mkutano huo unaojulikana kama FOSS4G 2018, umejumuisha wataalamu wa ramani mtandaoni, wawakilishi wa serikali mbalimbali, sekta binafsi, vyuo, vijana, na taasisi zisizokuwa za kiserikali.

Mkutano huo ulioandaliwa na FOSS4G, Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa na wadau wengine, unatoa fursa kwa washiriki  kubadilishana mawazo kuhusu umuhimu na faida ya kutumia teknolojia kuleta maendeleo na kuboresha kanzi data. Miongoni mwa washiriki ni Khadija Abdullah Ali  alimaarufu kama Malkia wa Drone kutoka Zanzibar. Yeye ni mtaalamu wa kutengeneza ramani kwa kutumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani au Drones na anasema kuna muhimu kutumia teknolojia hizo kwa ajili ya kuleta maendeleo katika jamii. Kwa mujibu wa waandaji wa mkutano huo kanzi data ni tatizo kubwa katika  nchi nyingi barani Afrika na duniani kote, hivyo uwezo wa kupata taarifa za msingi utasaidia kupima maendeleo kwa siku zijazo.

Hii ni mara ya pili kwa mkutano huu wa kimataifa kufanyika barani Afrika. Mara ya kwanza ulifanyika nchini Afrika Kusini mwaka 2016, na mwaka huu Tanzania.

Roboti za kuchunguza mabomba

Nchini China hivi sasa roboti zinatumika kuchunguza mabomba yaliyo chini ya ardhi katika miji mikubwa ili kuweza kubaini iwapo kuna dosari katika mtandao wa mabomba.

Katika mji wa Hefei, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Anhui, kuna roboti yenye miguu sita ambayo imeundwa na shirika la Wuhan Easy Sight Technology ambayo inatumika kuchunguza mambomba yaliyo chini ya ardhi.  Roboti hiyo yenye Kamera inaweza kufanya kazi kwa muda wa hadi masaa matano mfululizo katika masafa ya hadi mita 1000 ya bomba lililo chini ya ardhi.

Roboti hiyo ilianza kutumika kwa mara ya kwanza mwezi Julai katika wilaya ya Shushan na inatazamiwa kufanya ukaguzi katika mtandao wa mambo ya chini ya ardhi yenye urefu wa kilomita 150.

Roboti hiyo inaweza kubaini iwapo bomba linavuja, limeharibika au limezibwa. Wataalamu wanasema kamera iliyo katika roboti hiyo ina uwezo wa kutuma picha za hali ya juu na hivyo kurahisisha kazi  ya ukarabati. Kutokana na ustawi wa kasi wa miji, kumeibuka changamoto ya kusimamia mabomba yaliyo chini ya ardhi hasa mabomba ya maji taka na ya maji ya kawaida. Faida ya roboti hiyo ni kuwa kinyume na wanadamu inaweza kuingia katika mabomba madogo, haithiriwi na hewa chafu na yenye sumu katika mabomba ya maji taka na pia hakuna haja ya kuchimba na kuvuruga mtiririko wa magari barabarani wakati wa kutafuta matatizo katika bomba.

Kenya mwenyeji wa mkutano wa Einstein Ajaye

Kenya itakuwa mwenyeji wa Jukwaa la Kimataifa la Einstein Ajaye au Next Einstein Forum (NEF) ambalo limepangwa kufanyika mjini Nairobi Machi 2020.

NEF ni jukwaa ambalo huandaliwa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi za Hisabati (AIMS) kwa ushirikiano na  Taasisi ya Robert Bosch Stiftung ya Ulaya ambayo hujihusisha na ustawi wa sayansi kijamii na kimaumbile. Waziri wa Elimu wa Kenya Bi. Amina Mohammad ametia saini mapatano ya kikao hicho kwa niaba ya serikali ya Kenya huku mkuu wa AIMS na mwenyekiti wa NEF Thierry Comhahoun akiyatia saini kwa niaba ya NEF.

Amina amepongeza hatua ya kufanyika Jukwaa la Kimataifa la Einstein Ajaye nchini Kenya kwani hivi sasa nchi hiyo iko mbioni kuimarisha masomo ya sayansi katika sekta zote za elimu.

Amesema serikali ya Kenya sasa imeanzisha mpango maalumu wa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati, maarufu kama STEM katika majimbo yote 47 ya nchi hiyo. Amesema serikali ya Kenya inaamini kuwa masomo hayo yatawezesha nchi hiyo kustawi kiviwanda.

 

 

 

 

 

Tags

Maoni