Sep 04, 2018 05:41 UTC
  • Jumanne tarehe 4 Septemba 2018

Leo ni Jumanne tarehe 23 Dhulhija 1439 Hijria inayosadifiana na Septemba 4, 2018.

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, maandamano ya kwanza ya mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa Shah yalifanyika hapa nchini. Maandamano hayo yalifanyika baada ya Swala ya Idi na yalianzia katika vituo au nukta nne tafauti mjini Tehran na yakapata idadi kubwa zaidi ya watu kadiri muda ulivyosonga mbele. Waandamanaji hao ambao walikuwa wamebeba mabango pamoja na picha kubwa za Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, walisikika wakipiga nara za kutaka uhuru, kujitawala na kuundwa mfumo wa utawala wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu.

Maandamano ya kwanza ya mamilioni ya Wairani dhidi ya utawala wa Shah

Tarehe 4 Septemba miaka 110 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Richard Wright. Baada ya mashaka makubwa maishani, Richard Nathaniel Wright alianza kazi ya uandishi akiwa na umri wa miaka 30. Baadhi ya vitabu vyake vinaakisi sehemu ya maisha ya kifukara na ya kuchosha ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. Ameandika vitabu vingi kama Black Boy, Native Son, Uncle Tom's Children na The Outsider.

Richard Wright

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, mota ya kwanza ya umeme ilitengenezwa. Mvumbuzi na mtengenezaji wa mota hiyo alikuwa Thomas Edison mtaalamu na mtafiti wa Kimarekani. Kwa kutumia mota hiyo ya umeme, Edison alianzisha kiwanda cha umeme katika mji wa New York na wakati huo huo akawa amefanikiwa kudhamini sehemu ya mahitaji ya mwanga katika mji huo. Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kwamba, mwaka 1879, Edison alifanikiwa kuvumbua balbu.

Thomas Edison

Na Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sheikh Abbas Qummi, aalim na mpokeaji hadithi mtajika wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria katika mji mtakatifu wa Qum huko kusini mwa Tehran. Sheikh Abbas Qummi alianza kusoma elimu ya dini akiwa huko huko Qum na baadaye alielekea katika chuo kikuu cha kidini katika mji wa Najaf nchini Iraq ili kukamilisha masomo yake. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Sheikh Abbas Qummi alipata elimu kutoka kwa maulamaa watajika wa hauza hiyo ya kielimu. Sheikh Abbas Qummi alirejea Iran baada ya muda ambapo alitumia muda wake wote kuandika vitabu na kufuatilia masuala ya kidini. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwanazuoni huyo ni Mafatiihul Jinan na Manazilul Akherah.

Ayatullah Sheikh Abbas Qummi

 

Tags

Maoni