Sep 05, 2018 02:29 UTC
  • Jumatano, Septemba 5, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 24 Mfunguo Tatu Dhuhlija 1439 Hijria sawa na Septemba 5, 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1430 kwa mujibu wa riwaya mashuhuri ya kihistoria Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na binti yake mtukufu Bibi Fatima (AS), mkwewe Ali bin Abi Twalib (AS) na wajukuu wake wawili Imam Hassan na Hussain (AS) waliondoka mjini Madina kwenda kufanya mdahalo na viongozi wa Wakristo wa eneo la Najran. Tukio hilo linaelezwa na Mwenyezi Mungu SW katika aya za 60 na 61 za sura ya Aal Imran inayosema: "Hii ni Haki kutoka kwa Mola wako Mlezi, basi usiwe miongoni mwa wanaofanya shaka. Na watakaokuhoji katika haya baada ya kukufikia ilimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, kisha tuombe kwa enyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo." Wakati viongozi wa Najran walipoona Mtume amekuja katika mdahalo huo akiwa na watu wanne tu wa Nyumba yake tukufu walipingwa na mshangao na kuelewa kwamba, dua ya mtukufu huyo ya laana kwa atakayesema urongo itakubaliwa. Katika hali hiyo askofu wa Najran alisema: "Ninaziona nyuso ambazo iwapo zitamuomba Mwenyezi Mungu aung'oe mlima mkubwa zaidi mahala pake basi dua yao itajibiwa papo hapo. Kwa msingi huo si sahihi kufanya mdahalo na watu hawa watakatifu kwani yumkini kizazi chetu chote kikaangamia." Baada ya hapo askofu huyo wa Najran alimuomba Mtume (SAW) kufanya suluhu na kusamehe. Tukio hilo la kihistoria lilidhihirisha haki na ukweli wa dini tukufu ya Kiislamu na utukufu na nafasi aali ya Ahlubait wa Mtume Muhammad (SAW). 

Siku kama hii ya leo miaka 161 Auguste Comte mwanafalsafa na mwanahisabati wa Kifaransa alifariki dunia. Comte alizaliwa mwaka 1798. Alishirikiana kwa muda fulani huko Paris na Henri de Saint Simon, mwanafalsafa mashuhuri wa zama hizo na baadaye Comte alianza kufundisha. Auguste Comte alikuwa mwasisi wa mfumo wa elimu jamii. Comte ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha The Positive Philosophy of Auguste Comte.

Auguste Comte

Miaka 131 iliyopita mwafaka na tarehe 5 mwezi Septemba mwaka 1887, mto mkubwa wa Huang He huko China ulianza kufurika maji. Mafuriko hayo makubwa yalisababishwa na kujaa maji katika mto huo kwa zaidi ya mwezi mmoja. Zaidi ya watu laki tisa walipoteza maisha katika mafuriko hayo na taathira zake mbaya. Aidha miji kadhaa, mamia ya vijiji na mashamba mengi yaliharibiwa baada ya kukumbwa na mafuriko ya mto Huang He huko China.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita Ayatullah Ali Quddusi Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mapinduzi ya Kislamu nchini Iran aliuawa shahidi katika mlipuko wa bomu uliotekelezwa na kundi la kigaidi la MKO. Shahidi Quddusi alipata elimu kwa wasomi kama Ayatullah Burujerdi, Allama Tabatabai na Imam Ruhullah Khomeini MA na kufikia daraja ya Ijtihad. Shahidi Quddusi alishiriki vilivyo katika masuala ya kidini na mfano wa wazi wa mchango wake ni kuasisi shule ya mafunzo ya kidini ya Haqqani. Mwaka 1341 Hijria Shamsia alisimama kupambana na utawala dhalimu wa Shah na akatiwa jela kwa kipindi fulani. Ayatullah Quddusi alisabilia miaka ya mwishoni mwa umri wake kwa juhudi za kuimarisha mfumo mchanga wakati huo wa Kiislamu hapa nchini na hatimaye aliuawa shahidi na magaidi wa kundi la MKO katika siku kama hii ya leo.

yatullah Ali Quddusi

Siku kama yaleo miaka 25 iliyopita inayosadifiana na tarehe 5 Septemba 1993, moja kati ya misikiti mikubwa katika ulimwengu wa Kiislamu ulifunguliwa rasmi huko Casablanca nchini Morocco. Msikiti huo umejengwa mwa mtindo wa kisasa na una minara inayoakisi usanifu majengo wa hali ya juu wa Kiislamu. Eneo la uwanja wa msikiti huo lina uwezo wa kuchukua waumini 75,000. Eneo la ndani la msikiti huo limepambwa kiufundi. Pembeni ya msikiti huo kumejengwa maktaba moja kubwa na Chuo Kikuu cha Kidini. Msikiti huo unahesabiwa kuwa moja kati ya misikiti mikubwa na mizuri katika ulimwengu wa Kiislamu.

Msikiti wa Casablanca.

 

Tags

Maoni