Sep 07, 2018 02:20 UTC
  • Ijumaa tarehe 7 Septemba 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 26 Dhulhija 1439 Hijria sawa na tarehe 7 Septemba 2018.

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita alifariki dunia dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji.

Jenerali Mobutu Sese Seko

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo, Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani alifariki dunia. Alimu huyo ni mjukuu wa Mirza Muhammad Hassan Ashtiyani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Tumbaku nchini Iran. Alizaliwa mjini Tehran na baada ya kukamilisha masomo ya awali alielekea katika mji wa Najaf huko Iraq na kupata elimu kwa maulama mashuhuri wa zama hizo kama Ayatullah Mirza Naini na Sayyid Abul Hassan Isfahani. Ayatullah Muhammad Baqir Ashtiyani ameacha athari nyingi za vitabu zenye thamani kubwa katika nyanja mbalimbali.

Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita kulitokea Harakati ya Wanamasumbwi nchini Uchina. Wanamasumbwi lilikuwa jina walilopewa wanajeshi wa China waliosimama kupambana na ubeberu wa nchi za kigeni hususan za Magharibi ulioambatana na harakati za wamishonari wa Kikristo ndani ya China. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na wanamasumbwi hao ni kuteka balozi za nchi za Magharibi katika mji wa Beijing na kupambana vikali na shughuli za wahubiri wa Kikristo kutoka Ulaya. Hata hivyo Harakati ya Wanamasumbwi wa Kichina ilikandamizwa na majeshi ya Ulaya, Marekani na Japan na serikali ya China ikalazimika kulipa gharama kubwa kwa nchi hizo.

Majeshi ya nchi 8 yalishirikiana kukabiliana na Harakati ya Wanamasumbwi nchini Uchina.

Siku kama ya leo miaka 196 iliyopita, nchi ya Brazil ilipata uhuru wake toka kwa mkoloni Mreno. Ureno ilianza kuikoloni Brazil mwaka 1494, na mbali na kuwatumikisha watu wa jamii ya wekundu wa nchi hiyo, ilichukua mamilioni ya Waafrika kwa ajili ya kuwatumikisha kama watumwa katika shughuli za kilimo nchini humo.

Bendera ya Brazil.

Na siku kama ya leo miaka 880 iliyopita alizaliwa huko katikati mwa Iraq Abul-Fadhail Amedi fakihi na mwanafasihi wa Kiislamu. Baada ya kusoma elimu za fiqhi, usul fiqhi, fasihi na hisabati katika mji wa Baghdad aliondokea kuwa mahiri katika elimu hizo. Abul Fadhail Amedi ameqndika mashairi matamu na ya kuvutia. Amedi aliaga dunia katika eneo alikozaliwa akiwa na umri wa miaka 49.

 

Tags

Maoni