Sep 09, 2018 08:14 UTC
  • Jumapili, Septemba 9, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 28 Mfunguo Tatu, Dhul-Hijjah 1439 Hijiria, sawa na tarehe tisa Septemba mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1446 iliyopita vilianza vita maarufu kwa jina la Vita vya Miaka Saba kati ya madola mawili yaliyokuwa na nguvu kubwa wakati huo ya Iran na Roma, baada ya mfalme Justinian wa Roma kuanzisha mashambulizi yaliyokuwa na lengo la kulikalia kwa mabavu eneo la magharibi mwa Iran. Baada ya miaka saba ya vita mfalme wa Iran Anushirvan alimshinda mfalme Justinian wa Roma na hivyo mfalme huyo akalazimika kujiuzulu. Baada ya kujiuzulu mfalme Justinian mfalme Tiberius alishika mamlaka ya utawala wa Roma. Vita hivyo vilimalizika mwaka 579 baada ya Waroma kukubali kuilipa Iran gharama inayofikia sarafu za dhahabu elfu 45.

Vita vya miaka saba kati ya madola mawili yaliyokuwa na nguvu ya Iran na Roma

Siku kama ya leo miaka 1376 iliyopita, sawa na tarehe 28 Dhul-Hijjah mwaka 63 Hijiria, yaani miaka miwili baada ya harakati na mapambano ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) yaani Imam Hussein bin Ali (AS) katika ardhi ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria, kulijiri tukio la Harrah. Mwaka huo watu wa mji mtukufu wa Madina waliokuwa wamechoshwa na dhulma na ukatili wa mtawala Yazid bin Muawiya, walimfukuza gavana wake mjini humo Marwan bin Hakam. Baada ya tukio hilo Yazid alituma jeshi likiongozwa na mtumishi wake mmwaga damu na mtenda dhulma Muslim bin Uqbah katika mji mtakatifu wa Madina na kuliamuru kufanya mauaji makubwa mjini humo na kupora mali. Mauaji kama hayo hayakuwahi kushuhudiwa katika historia ya zama za awali za Uislamu na wanahistoria wamesema kuwa Waislamu zaidi ya elfu kumi wakiwemo maswahaba wa Mtume, waliuawa katika shambulizi hilo. Vitabu vya historia pia vinasema utawala wa Yazid bin Muawiya ulihalalisha mji wa Madina kwa askari wake kwa muda wa siku tatu na kwamba wasichana na wanawake wa maswahaba walinajisiwa katika tukio hilo.

Vita ya Harrah

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, alizaliwa Leo Tolstoy, mwandishi na mwanafasihi raia wa Russia. Awali Tolstoy alijiunga na jeshi la Qaukasia na ni katika kipindi hicho ndipo alipoandika kitabu chake cha kwanza alichokipa jina la "Childhood". Mwandishi huyo wa Russia baadaye alijiengua jeshini na kutumia muda wake wote kwa ajili ya kusoma na kuandika. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwandishi Leo Tolstoy ni "Vita na Amani", "Waqazaki" na "Hadji Murad." Tolstoy alifariki dunia mwaka 1910.

Leo Tolstoy

Siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, alifariki dunia Hadi Sabzavari au Hajj Mulla Hadi Sabzavari, mmoja wa maulama na wanafalsafa wakubwa wa karne ya 13 Hijiria. Mulla Hadi Sabzavari alizaliwa mwaka 1212 Hijiria ambapo umri wake ulijaa baraka, huku mwishoni mwa maisha yake akijawa na izza ya nafsi, zuhdi na ucha-Mungu. Athari za Mulla Hadi Sabzavari zinaonyesha kwamba, alimu huyo mkubwa wa Waislamu mbali na kwamba alikuwa mmoja wa wanafalsafa wakubwa, pia alitabahari katika uwanja wa elimu ya sheria za Kiislamu (fiq'hi), tafsiri ya Qur'an, mantiki, hisabati, fasihi na elimu ya tiba. Aidha Mulla Hadi Sabzavari mbali na kufikia daraja za juu za kielimu, alikuwa pia malenga. Katika uwanja huo, alikuwa akisoma mashairi ambayo yalifungamana na nukta za kifalsafa na elimu ya irfani. Allamah Iqbal Lahore, malenga na mwanafalsafa mkubwa wa Pakistan, alimzungumzia Mulla Hadi Sabzavari kuwa, mwanafikra mkubwa wa Iran ambaye falsafa yake alijifunza kupitia dini ya Kiislamu. Miongoni mwa athari za mwazuoni huyo ni pamoja na 'Mandhumah' katika uwanja wa elimu ya mantiki, 'Asraarul-Hikami' na 'al-Jabru wal-Ikhtiyaar.'

Hajj Mulla Hadi Sabzavari

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita yaani tarehe 9 Septemba 1945, kulitiwa saini mkataba wa kusalimu amri vikosi vya Japan vilivyokuwa vimeidhibiti na kuikalia kwa mabavu China. Kwa mujibu wa mkataba huo askari milioni moja wa Japan waliweka chini silaha zao kwa amri ya Hirohito mfalme wa wakati huo wa Japan. Kwa utaratibu huo vita vya kihistoria kati ya China na Japan vikafikia tamati.

Mkataba wa kusalimu amri vikosi vya Japan

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, Korea Kaskazini ilijitangazia uhuru, kufuatia kujiri Vita vya Pili vya Dunia na kugawanywa eneo la Korea. Katika historia ya Rasi ya Korea, ardhi ya Korea Kaskazini na kwa mara kadhaa ilikaliwa kwa mabavu na mataifa mbalimbali ya kigeni. Mwaka 1905 na baada ya kushindwa nchi za China na Urusi ya zamani, Japan iliidhibiti Rasi ya Korea na licha ya mapambano kadhaa ya Wakorea kutaka kujiokoa na uvamizi huo, bado rasi hiyo iliendelea kudhibitiwa na nchi hiyo hadi mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Kutokana na pendekezo la kongamano la Yalta na Potsdam la mwaka 1945, Korea Kaskazini ilidhibitiwa na Urusi ya zamani, huku Korea Kusini nayo ikidhibitiwa na Marekani. Na hatimaye katika siku kama ya leo ikiwa ni muda wa chini ya mwezi mmoja umepita baada ya Korea Kusini kutangaza uhuru, nayo Korea Kaskazini ikajitangazia uhuru.

Bendera ya Korea Kaskazini

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita yaani tarehe 18 Shahrivar 1348 Hijria Shamsia, alifariki dunia Jalal Aal Ahmad, mwandishi na mkosoaji wa Kiirani. Aal Ahmad alizaliwa mwaka 1302 Hijria Shamsia jijini Tehran. Mwaka 1325, Jalal al Ahmad alitunukiwa shahada ya fasihi ya Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika uwanja wa siasa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na akaanza kuandika katika magazeti. Alijishughulisha na kuandika makala na ukosoaji na hadithi fupi fupi. Jalal Aal Ahmad alikuwa hodari katika kuandika visa.

Jalal Aal Ahmad.

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, aliaga dunia Mao Tse Tung (Mao Zedong) kiongozi wa Uchina. Tse Tung alizaliwa mwaka 1893 na mwaka 1921 aliunda chama cha Kikomonisti cha Uchina baada ya kuungwa mkono na wafuasi wa fikra zake. Mao alikuwa akisisitiza juu ya kuwatetea na kuwalinda wanavijiji na kwa sababu hiyo alipata uungaji mkono mkubwa wa wanavijiji wa Uchina.

Mao Tse Tung

 

Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, nchi ya Tajikistan ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Umoja wa Kisovieti.  Katika karne ya 6BC Miladia, Tajikistan ilikuwa sehemu ya utawala wa Hakhamaneshian wa Iran na katika karne ya 9 Miladia ikakombolewa na Waislamu. Kijiografia Tajikistan ipo katikati mwa Asia ikiwa na ukubwa wa kilomita mraba 143,000 na inapakana na nchi za China, Uzbekistan, Afghanistan na Kyrgyzstan na mji mkuu wake ni Dushanbe. Sarafu ya nchi hiyo ni Somoni huku lugha ya taifa ikiwa ni Kitajiki.

Bendera ya Tajikistan

 

 

Tags

Maoni