Sep 09, 2018 09:59 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (124)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo mpenzi msikilizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia suala la kulaani na kutoa laana ikiwa na maana ya kumtakia mtu mwingine afikwe na jambo baya. Tulisema kuwa, laana au kulaani ni apizo atoalo mtu kwa mtu mwingine ili afikwe na jambo baya. Tuulibainisha kwamba, kitendo hiki kimegawanyika katika sehemu mbili. Kwa maana kwamba, kulaani kinaweza kuwa ni kitendo hasi na wakati mwingine kikawa ni chanya na cha mahala pake. Hii ni kusema kuwa, kama laana itatolewa mahala pake panapostahiki huwa chimbuko la mtu kujikurubisha na Mwenyezi Mungu. Lakini kama kulaani na kutoa laana kutakuwa si pa mahala pake huwa na matokeo mabaya na humfanya mhusika kuwa mbali na rehema za Mwenyezi Mungu SWT. Tuliashiria nukta muhimu nayo ni kwamba, mtu anapaswa kuwa makini mno kabla ya kutoa laana kwani kama atamlaani mtu asiyestahiki basi laana hiyo humrejea mwenyewe. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 124 ya mfululizo huu kitazungumzia tabia ya ukorofi na kutoa visingizio. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.                                     

 

Kuna wakati mtu hufanya kosa, lakini atapozinduka na kufahamu kuwa, amekosoa huomba radhi na msamaha kwa kosa lake hilo. Katika mazingira kama haya, uwezekano wa yeye kukosea tena au kufanya kosa hilo hilo hupungua au kutokuweko kabisa. Lakini kuna wakati pia inashuhudiwa kwamba, baada ya mtu kukosea au hata kutenda dhambi na kosa lake kuonekana bayana, badala ya kuomba msamaha au kutubia dhambi yake, mhusika hutafuta visingizio na kukataa kubeba masuuliya na jukumu la kosa lenyewe.  

Kitendo hiki kwa kupita muda na kukaririwa, humgeuza mhusika na kumfanya kuwa mtu mkorofi na kaidi ambaye kumbadilisha tena huwa kibarua kigumu. Katika mazingira kama haya, tabia ya kutafuta visingizio baada ya kuufanya kosa na mhusika kuwa mkorofi kwa kukataa kukiri kosa, huwa ni jambo baya kuliko kitendo chenyewe. Hii ni kutokana na kuwa, hatua hiyo huondoa fursa ya mtu kujirekebisha na kusahihisha mwenendo na tabia yake mbaya na kumuandalia uwanja wa kuzama na kughiriki katika dhambi kubwa zaidi. Imam Ali AS amenukuliwa akibainisha hatima ya mtu mkaidi, mkorofi na mtafutaji visingizio baada ya kufanya kosa kwa kusema: Mtu ambaye atafanya ukorofi (na kutoa visingizio) na kisha akaendelea na mwenendo wake huo, fikra zake hupinduka na Mwenyezi Mungu hutia kutu moyo wake na hivyo mambo mabaya humzunguka na kumzingira.

 

Mtu ambaye ana tabia ya kutoa visingizio licha ya kuwa na elimu na ufahamu kamili juu ya ukweli, kimsingi huwa ni mkaidi na mkorofi na hukwepa kukubaki haki na ukweli. Tabia na mwenendo huu mbaya, baadhi ya wakati kutokana na kukakariwa, hudhihirika na kuwa sifa za wazi za mtu. Sifa ambayo humfanya na kumgeuza mtu kuwa muasi katika jamii anayoishi.

Katika kubainisha hilo, Imam Ali bin Abi Twalib AS anaitaja sifa ya ukorofi kuwa ni kipando cha uasi. Anasema:  Hakuna kipando cha uasi zaidi kama ukorofi na ukaidi.

Hadithi hii iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Ali AS inataka kuonyesha na kutueleza ukweli huu kwamba, ukorofi na kutoa visingizio, humpeka mhusika na kumfikisha mahala ambapo hakutarajia. Hata hivyo, wakati mwingine ukorofi na utoaji visingizio ni matunda ya lawama zisizo za mahala pake ambazo mtu hutwishwa na wengine. Kulaumu na kutoa lawama kupita kiasi, hususan kama hatua hiyo itaambatana na utumiaji mabavu au hilo kufanyika mbele za watu, humfanya mlaumiwa akumbwe na hali mbaya ya ukorofi na utoaji visingizio. Ni katika mazingira kama haya ambapo mlaumiwa akiwa na lengo la kuhalalisha vitendo vyake na kuonyesha kwamba, hakuwa katika makosa na kwamba, lawama za wengine hazikuwa za mahala pake, hung'ang'ania na kukamia maneno yake na kutaka kuendelea kushikamana na tabia yake hiyo.

Ndio maana Imam Ali AS anaeleza kuwa, moja ya sababu za ukorofi na utoaji visingizio ni mtu kuandamwa na lawama kupita kiasi. Anasema: Kuchupa mipaka katika kulaumu, huwasha moto wa ukorofi.

 

Wapenzi wasikilizaji matatizo mengi na masaibu ya kijamii ni matokeo ya mijadala, mivutano na ukorofi wa baadhi ya watu baina yao katika jamii. Kundi moja limefanya ukorofi na kundi la pili kutokana na ujahili na kujiona nalo limeamua kufuata njia hiyo hiyo na kwa msingi huo kuwasha moto wa mivutano na mapigano. Hii ni katika hali ambayo, lau watu wangeachana na tabia ya kutafuta na kutoa visingizio na kwa namna fulani wakashikamana kidogo na subira na ustahamilifu, basi wangeweza kuzuia mivutano na makelele mengi yanayoshuhudiwa hii leo katika jamii. Imam Ali AS anautaja ukorofi na utoaji visingizio kuwa ni chimbuko la kila shari. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Kitovu cha shari na ufisadi ni ukorofi na mijadala ya taasubi.

Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana Imam Ali AS anawaasa Waislamu na kuwataka wajiweke mbali na tabia ya ukorofi na utafutaji visingizio hasa baada ya kuwa mtu amefanya kosa na kosa lenyewe kufahamika na kueleweka wazi na bayana. Kusimama kidete na kung'ang'ania jambo la haki ni hatua ya kupendeza na ambayo imekokotezwa katika mafundisho ya Kiislamu. Lakini kinyume chake, yaani mtu kung'ang'ania jambo la batili na kutokubali kubadilisha msimamo wake, humfanya mhusika akumbwe na hatima mbaya. Tukirejea katika mafundisho ya Kiislamu tunaona kuwa, Lajuuj yaani mtu mkorofi si mwenye kufuata mantiki na wanajamii wanamuona mtu mkorofi na mwenye kutoa visingizio ili kuhalisha makosa yake kuwa ni mchache wa akili na asiyetumia bongo.

Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi chetu, sina budi kukomea hapa kwa leo, nikiwa na matumaini kwamba, mmenufaika na yale niliyokuandalieni kwa wiki hii.  Ninakuageni nikimuomba Allah atuepusha na ukorofi na tabia ya kutoa visingizio badala ya kuomba msamaha pale tunapokosea.

Basi hadi wakati huo ninakuegeni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh.

Tags

Maoni