Sep 09, 2018 10:16 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (126)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia suala la elimu bila amali yaani kutoifanyia kazi elimu. Tulisema kuwa, kuwa na elimu ni jambo muhimu lakini kuifanyia kazi elimuu hiyo ni jambo lenye umuhimu maradufu. Hii ni kutokana na kuwa, mtu ambaye hanufaiki na elimu yake ni mithili ya punda aliyebeba mzigo ambaye hana anachofahamu ghairi ya uzito wa mzigo huo. Moja ya hadithi tulizokunukulieni na ambayo inabainisha umuhimu wa kuifanyia kazi elimu ni ile iliyonakiliwa kutoka kwa Bwana Mtume SAW katika kukemea wasomi na wajuzi ambao hawanufaiki na elimu yao anasema: Kila ambaye elimu yake itaongezeka, lakini hidaya yake isiongezeke, elimu yake haina kitu kingine ghairi ya kumuweka mbali na Mwenyezi Mungu. Aidha tulibainisha kwamba, elimu ni sababu ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, lakini kama elimu hiyo isipofanyiwa kazi huwa mzigo kwa mtu na badala ya kumfikisha mja katika kilele, humporomosha mwanadamu huyo na kumfikisha katika madhila.  Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 126 ya mfululizo huu kitajadili na kuzungumzia suala la kutunza na kufichua siri. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa dakika hizi chache. Karibuni.

 

Moja ya sifa za Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo ni kutunza na kuhifadhi siri. Elimu isiyo na kikomo ya Mola jalali imeenea na kuvizunguka vitu vyote na Mwenyezi Mungu ana habari ya kila kitu, lakini utunzaji na ufichaji siri wake hauna mithili na haiwezekani kuutolea wasifu. Mtu muumini pia ambaye ni mja wa Allah na mwakilishi wa Allah katika ardhi, anapaswa kuwa kama Muumba wake yaani awe ni mwenye kulinda na kuhifadhi siri na afunike aibu na mapungufu ya watu wengine. Kwa maana kwamba, asitoboe na kufichua siri za watu na aibu zao.

Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as) amenukuliwa akisema katika hadithi moja kuhusiana na maudhui hii kwamba: Muumini hawezi kuwa muumini wa kweli mpaka atakapokuwa na sifa tatu:  Suna kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Suna kutoka kwa Mtume na Suna kutoka kwa Walii wa Mwenyezi Mungu. Amma Suna ya Mwenyezi Mungu ni kuhifadhi na kutunza siri. Suna ya Mtume ni kuwalegezea watu mambo na amma kuhusu Suna ya Imam (walii) ni kuwa na subira mbele ya mitihani na matatizo. (Uyuun Akhbar al-Ridha).   

Kuhusiana na suala la kutunza na kuhifadhi siri kuna hadithi na riwaya nyingi zinazotilia mkazo jambo hilo. Sisitizo la kulinda siri ni kubwa kiasi kwamba, Imam Ja'far bin Muhammad al-Swadiq AS analitaja jambo hilo kuwa lina umuhimu kama damu inavyozunguka katika mishipa ya mwanadamu. Anasema kuwa:  Siri yako ni sehemu ya damu yako, hivyo basi damu hiyo haipaswi kuzunguka katika mishipa isiyokuwa ya kwako.  (Mizan al-Hikmah Jz 2). Kwa maana kwamba, kama ambavyo mzunguko wa damu katika mishipa huwa sababu ya kupatikana uhai, kuondoka damu hiyo katika mishipa hukwamisha uhai wa mtu na yumkini akapoteza maisha, vivyo hivyo siri za mtu pia kama zitatoka katika asasi ya mtu na kuwa kwa watu wengine, maisha ya kawaida ya mtu huyo hutetereka na heshima yake kuwa hatarini.

 

Wapenzi wasikilizaji kuna haja ya kuzingatia nukta hii kwamba, mtu ambaye hawezi kujilinda mwenyewe, bila shaka hawezi kutunza na kuhifadhi siri za watu wengine.

Mkabala na hilo, watu nao hawatakuwa ni wenye kufunika na kuficha siri zake. Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as) akiwa na lengo la kuwazindua watu wasio na uwezo wa kuficha na kulinda siri zao amesema katika maneno yenye hekima kubwa kwamba: Mwaminifu hakufanyii hiana (usaliti), wewe ndiye ambaye amempatia mtenda hiana amana yako (yaani siri yako).

Kwa msingi huo basi, katika fikra na mafundisho ya Uislamu, siri za watu ni mithili yaa amani na kuifichua au kuitoboa siri hiyo ni kufanya hiana katika amana. Kwa maana kwamba, mtu anapokwambia siri yake ni kana kwamba, amekupatia amana umhifadhie. Imam Ali bin Abi Twalib AS anafafanua nukta hii kwa kusema: Siri uliyoambiwa, usiifichue, kwani kufichua siri ni (kutenda) hiana. Aidha mbora wa viumbe Bwana Mtume SAW amenukuliwa akisema kuwa, wakati mtu anapozungumza na mtu mwingine kisha akawa ni mwenye kuangalia huku na kule ili mtu mwingine (wasiokuwa wao wawili) asije akasikia, basi maneno hayo ni mithili ya amana.

Kupitia hadithi hiyo tunafahamu kwamba, maneno hayo aliyeambiwa hapaswi kuyasema sehemu nyingine yaani kwa watu wengine.

Nukta nyingine muhimu ni hii kwamba: Mtu ambaye anafichua siri za watu, Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu na hivyo hufichua siri zake kwa watu wengine.

Katika kubainisha zaidi nukta hii, Imam Ali bin Abi Twalib as anasema: Kila ambaye ataondoa pazia la siri la ndugu yake Mwislamu, Mwenyezi Mungu hufichua aibu na siri zake.

Kwa msingi huo na kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, kwa vyovyote vile hakuna mtu mwenye haki ya kufichua siri za watu wengine.

 

Inasimuliwa kwamba, Bwana mmoja mwenye heshima zake alikuwa akimuandikia barua mmoja wa marafiki, mwandani na swahibu wake. Lakini kulikuwa na mtu aliyekaa kando na ubavuni mwake ambaye alikuwa akichungulia na kusoma kila alichokuwa akikiandika Bwana yule. Bwana aliyekuwa akiandika barua kwa swahibu wake akalifahamu hilo na ikamuia vigumu kuendelea kuandika barua ile hasa kwa kuzingatia kwamba, kuna mambo ya siri ambayo alitaka kumueleza mwanadani wake katika barua hiyo. Akaamua kuandika hivi: Swahiba wangu, laiti kando yangu asingekuwa amekaa mtu ambaye anasoma maandiko yangu haya, basi ningekueleza siri zangu zote." Bwana yule aliyekuwa akichungulia na kusoma kwa kuibia barua ile akasema: Wallahi, naapa mimi sijasoma barua yako. Bwana muandikkaji wa barua akahamaki na kusema: Ewe mjinga! Kama ungekuwa husomi ninayoyaandika, basi umejuaje kama nimekutaja katika barua hii?

Wapenzi wasikilizaji, muumini kwa kulinda siri zake anakuwa amehifadhi nafasi yake. Hii ni kutokana na kuwa, kufichuliwa baadhi ya siri miongoni mwa siri za maisha binafsi ya mtu, wakati mwingine huwa chimbuko la husuda, chuki, adawa na hata ushindani usio salama.  Tunakamilisha kipindi chetu cha juma hilo kwa hadithi kutoka kwa Imam Ali bin Abi Twalib as ambaye amenukuliwa akisema: Siri yako ni chimbuko la ukunjufu wa moyo na furaha yako, kwa sharti kwamba, uifiche siri hiyo, na kama utaifuchua (utamwambia mtu), itakuwa chimbuko la kuangamia kwako.

Muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umefikia tamati kwa leo, tukutane tena wiki ijayo siku na wakati kama wa leo.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Tags

Maoni