Sep 09, 2018 11:12 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (62)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 62.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba tunapoyachunguza matukio yaliyojiri katika Ulimwengu wa Kiislamu katika vipindi tofauti vya umri wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC tutabaini kuwa, moja ya sababu kuu za kutofanikiwa jumuiya hiyo kimalengo ni nchi wanachama kujali zaidi maslahi yao binafsi kuliko maslahi ya pamoja na ya jumuiya.  Sababu nyingine iliyoikwamisha Jumuiya ya Nchi za Kiislamu na kuifanya ishindwe kufikia malengo yake kikamilifu ni kuwepo misuguano na mivutano kati ya malengo hayo na hatua za jumuiya hiyo mkabala na malengo na hatua za jumuiya zingine za kieneo na kimataifa. Japokuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ilijaribu katika misingi na hati yake kujenga uhusiano na maelewano na jumuiya nyingine za kieneo na kimataifa, lakini kivitendo na katika utekelezaji kumejitokeza misuguano na migongano kati ya maslahi ya OIC na jumuiya zingine za kieneo na kimataifa; misuguano ambayo imezorotesha harakati ya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu na kuifanya ipige hatua kwa mwendo wa kujikongoja na kusuasua katika kufikia malengo yake au hata kuathiriwa kwa kiwango cha kupindukia na jumuiya hizo. Kusema hivi hakumaanishi kwamba sababu ya hali hiyo itakuwa lazima imetokana na migongano ya malengo na utendaji wa OIC na ule wa jumuiya zingine za kieneo na kimataifa hususan Umoja wa Mataifa, kwa sababu Jumuiya ya Nchi za Kiislamu imekuwa ikisisitiza kila mara katika maazimio yake juu ya ulazima wa kushirikiana, kustawisha na kuimarisha uhusiano wake na Umoja wa Mataifa.

Mkutano wa "Wahda" mjini Tehran Iran

 

Kwa kutoa mfano, katika kikao cha 16 cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa OIC lilipitishwa azimio kwa madhumuni ya kustawisha uhusiano na jumuiya zingine za kieneo na kimataifa. Hata katika baadhi ya kadhia, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu imeidhinisha na kuafiki maamuzi yaliyopitishwa na Umoja wa Mataifa kinyume na maslahi yake makuu na kutilia mkazo kutekelezwa maamuzi hayo. Mfano wa suala hilo ni hatua ya kuunga mkono msimamo uliochukuliwa na Umoja wa Mataifa wakati Iraq ilipoivamia kijeshi Kuwait ambapo Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ilisisitizia ulazima wa kushirikiana na Umoja wa Mataifa.  Sababu ya kuchukua misimamo ya aina hiyo ambayo iliandamwa na lawama na ukosoaji mkubwa pia ni kwamba katika hati ya misingi na malengo ya OIC kuna mambo yaliyoainishwa ndani yake ambayo yanaendana na kuwiyana kikamilifu na misingi na hati ya Umoja wa Mataifa: mfano wake ni kupambana na ukoloni na ubaguzi wa rangi na kuleta amani na uadilifu. Kwa hivyo kinachokusudiwa hasa ni misuguano, migongano au misokotano inayojitokeza kwenye malengo na maslahi ya baadhi ya jumuiya za kieneo na kimataifa na OIC na kuwa na taathira hasi ya kudhoofisha nafasi na maamuzi yanayopitishwa na jumuiya hiyo ya nchi za Kiislamu. Na mfano wa asasi hizo ni Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Kwa kutilia maanani kwamba sehemu kubwa ya wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu inaundwa na nchi za Kiarabu, katika baadhi ya masuala misimamo ambayo OIC imekuwa ikichukua imekuwa zaidi na sura ya Uarabu kuliko ya Uislamu na jambo hili kwa kiwango kikubwa limekuwa likitokana na ushawishi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) katika jumuiya hiyo ya nchi za Kiislamu. Kwa mfano wakati ulipopendekezwa mpango wa Fas kwa ajili ya amani kati ya Wapalestina na Israel, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu iliathiriwa na misimamo ya Arab League kiasi kwamba licha ya kuwepo baadhi ya misingi iliyokubaliwa na nchi zote wanachama wa OIC kuhusiana na Israel, mpango huo ulipitishwa kwa mashinikizo ya Saudi Arabia na nchi nyingine za Kiarabu. Mpango wa mapatano wa Fas ulikuwa umeshaidhinishwa hapo awali katika kikao cha kumi na mbili cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Hali hiyo ilishuhudiwa pia katika uungaji mkono usio wa moja kwa moja wa OIC kwa Iraq katika vita ilivyoanzisha dhidi ya Iran.

 

Sababu nyingine ambayo imeifanya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu isifanikiwe kufikia malengo yake ni kukosekana msukumo na dhamana ya utekelezaji wa maamuzi yanayopitishwa na jumuiya hiyo. Kubaki bila utekelezwaji maamuzi yanayopitishwa na OIC si tu yanaitia dosari itibari ya maamuzi hayo yaliyopitishwa na nchi wanachama lakini pia kunashusha hadhi ya jumuiya hiyo kimataifa. Kwa hivyo kushindwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu kujiwekea taratibu za utekelezaji kwa ajili ya kufuatilia kwa njia ya kudumu maamuzi yaliyopitishwa kumeigeuza jumuiya hiyo kuwa asasi ambayo maamuzi yake ni ya kiwango cha ushauri tu ambao inautoa kwa nchi wanachama na wigo wa ushawishi wake ni wa kiwango na mpaka maalumu. Kwa sababu ya kukosekana hakikisho la utekelezaji, nchi na jumuiya zingine zimekuwa haziyapi umuhimu tena wala itibari na uzito yanaostahiki maamuzi yanayopitishwa na OIC katika hali ambayo kutokana na kuwa na suhula nyingi za kiuchumi, kisiasa na kijeshi, nchi wanachama zinao uwezo wa kuhakikisha maamuzi zinayopitisha yanatekelezwa na hivyo kuongeza kiwango cha itibari na hadhi ya jumuiya katika uga wa kimataifa. Inavyoonyesha, kuwepo hitilafu za ndani baina ya nchi wanachama wa OIC ndiko kunakosababisha maamuzi yanayopitishwa na jumuiya hiyo yasiwe na nguvu na dhamana ya utekelezaji.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa kwa kuangazia utendaji wa iliyokuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ambayo sasa ni Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC katika vipindi tofauti tutabaini kwamba sababu tatu tulizozitaja, yaani kufadhilisha na kuweka mbele maslahi ya kitaifa badala ya maslahi ya pamoja ya jumuiya, misuguano na uingilianaji wa maslahi na misimamo ya OIC na jumuiya zingine za kieneo na kukosekana dhamana na hakikisho la utekelezaji ndiyo mambo muhimu zaidi yaliyokwamisha utendaji wa jumuiya hiyo ya nchi za Kiislamu katika awamu mbalimbali; na bila kutatuliwa matatizo hayo hadhi na itibari ya OIC itaendelea kuwa na doa; na dhana ya kupatikana umoja na mshikamano wa Kiislamu itabaki kuwa ndoto.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 62 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Inshallah katika mfululizo ujao wa 63 tutakuja kuzungumzia kipindi kilichojulikana kama zama za Mwamko wa Kiislamu na kutathmini utendaji wa OIC katika kipindi hicho. Basi hadi wiki ijayo, katika siku na saa kama ya leo nakuageni na kukutakieni kila la kheri maishani.

Tags

Maoni