Sep 09, 2018 11:18 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (64)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 64.

Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa Yemen na Bahrain zilikuwa nchi nyingine ambazo ziliathiriwa na wimbi la Mwamko wa Kiislamu. Tukaashiria kwamba maandamano ya upinzani yalianza katikati ya Januari mwaka 2011 katika miji mingi ya kaskazini na kusini mwa Yemen. Malalamiko ya waandamanaji, kwanza yalihusu upinzani wao kwa mipango ya serikali ya kuibadilisha katiba, kukosekana ajira, hali mbaya ya uchumi na ufisadi uliokithiri. Lakini matakwa na madai yao yalibadilika ghafla yakawa ni kumtaka aliyekuwa rais wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh ajiuzulu.

Kama tujuavyo, kwa upande wa Yemen mapigano na machafuko yangali yanaendelea kushuhudia mipando na mishuko mingi, lakini kwa hivi sasa hatamu za madaraka ziko mikononi mwa jeshi la taifa na vikosi vya kujitolea vya harakati ya wananchi ya Ansarullah; na hujuma na mashambulio ya kijeshi yanayoendelea kufanywa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kwa zaidi ya miaka mitatu sasa kwa madhumuni ya kuisambaratisha harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wa Riyadh, Abd Rabbuh Mansour Hadi, hadi sasa hayajaweza kubadilisha mlingano wa nguvu za madaraka nchini humo.

Nchini Bahrain pia malalamiko ya umma yalianza tarehe 14 Februari mwaka 2011. Kwa sehemu kubwa, maandamano nchini humo yalifanyika kwa njia ya amani na lengo la maandamano na mikusanyiko hiyo, mwanzo wake lilikuwa ni kupigania uhuru zaidi wa kisiasa na kutaka kuheshimiwa haki za binadamu; na kimsingi waandamanaji hawakuwa na dhamira ya kuuandama moja kwa moja utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa. Lakini kutokana na hatua kali na kandamizi za askari polisi, waandamanaji wakataka kuhitimishwa enzi za utawala wa kifalme nchini Bahrain. Makabiliano ya wananchi na utawala wa Bahrain nayo pia yamekuwa na mipando na mishuko mingi, lakini hadi sasa madaraka yangali mikononi mwa utawala na ukoo wa Aal Khalifa.

 

Matukio yaliyojiri na yanayoendelea kujiri katika nchi za Syria, Yemen na Bahrain ni moja ya vielelezo na mifano hai ya mpasuko na hali ya utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Hivi sasa mlingano wa kisiasa katika nchi hizo umetatizika na kuwa tata mno, na kutokana na wimbi la uhasama mkubwa uliozuka baina ya nchi za Kiislamu, nchi za Magharibi na maadui walioapa kuuangamiza Uislamu na Waislamu wanalitumia kikamilifu kwa maslahi yao wimbi hilo la uhasama na mapigano yanayoendelea. Bila ya shaka yoyote itatupasa tuseme kuwa mikono michafu ya utawala wa Kizayuni wa Israel imeingia kwenye mengi ya matukio hayo; na kama ilivyokwisha thibitika na kubainika, viongozi wa makundi yanayoonekana kidhahiri kuwa ya Kiislamu, hususan makundi ya kigaidi na ukufurishaji likiwemo la Daesh (ISIS), kwa kutojielewa au kwa uelewa kamili wanatumiwa na mashirika ya ujasusi ya Marekani na Israel, yaani CIA na Mossad.

Kwa masikitiko, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ambayo nayo pia ingeweza kuingilia kati katika kadhia hizo kwa mtazamo wa insafu na uadilifu kamili na kwa kutegemea nguvu na uwezo wa nchi wanachama, bado haijaweza kuchukua nafasi inayostahiki na kutoa mchango chanya katika uwanja huo; lakini hata katika baadhi ya kesi imekuwa ikichukua misimamo isiyo ya busara na hivyo kushadidisha hasama, chuki na uadui uliopo. Kwa kuzingatia umuhimu wa matukio yanayojiri katika nchi hizo tatu, kipindi hiki na vinavyofuatia vitajaribu kuzungumzia baadhi ya matukio hayo machungu ambayo ni nadra kuwahi kushuhudiwa katika historia ya uhusiano ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu.

Kongamano wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran, Iran

 

Kwa upande wa kadhia ya Syria, wakati mapigano yaliyokuwa yakiendelea nchini humo yalipokuwa yameshtadi na kufikia kilele, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, ambayo ilikuwa na uwezo wa kuchukua nafasi ya msuluhishi asiyependelea upande wowote na kupendekeza njia ya kimantiki ya utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo, kwa ombi lililowasilishwa na Saudi Arabia, ilikubali kuitisha kikao cha dharura cha viongozi wa nchi wanachama wa OIC ambacho kilifanyika mwezi Agosti 2012 mjini Makka. Kikao hicho kilifanyika katika hali ambayo mlolongo wa vikao vya waungaji mkono wa wapinzani wa serikali ya Syria vilivyofanyika katika miji ya Istanbul, Uturuki, Tunis, Tunisia na barani Ulaya vilikuwa vimegonga mwamba; navyo vikao vya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu vilimalizika bila ya kupatikana tija, na juhudi zilizofanywa na hayati Kofi Annan, mjumbe wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Syria zilikuwa nazo pia zimegonga mwamba. Katika kikao hicho cha Makka, rais wa wakati huo wa Iran alisisitiza na kutilia mkazo udharura wa kuchukuliwa hatua mbili kwa pamoja, ambazo ni kuleta mageuzi na marekebisho nchini Syria na wakati huohuo kukabiliana na uingiliaji wa madola ajinabi. Alisema: "Inapasa tuzingatie kwa makini maudhui zote hizi mbili; yaani udharura usio na shaka wa kufanyika mageuzi na kudhaminiwa haki za msingi za watu wa mataifa yetu na vilevile kukabiliana kishujaa na kwa hekima na umakini na njama na mipango wanayotaka kututwisha maadui. Na katika kufanya hivyo, si uwepo wa adui, mipango na ulazimishaji wake utufanye tuache kudhamini kikamilifu haki za msingi za wananchi wetu, wala kushughulika kwetu na marekebisho kusitughafilishe na adui na njama zake. Mawili haya ni hakika moja na jukumu la aina moja, na yanategemeana katika ufanikishaji wao." Hata hivyo licha ya msimamo na pendekezo hilo la kimantiki lililotolewa na Iran katika kikao hicho, kwa mashauriano na mashinikizo yaliyotolewa na Saudia, uanachama wa Syria katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ulisimamishwa rasmi.

Msimamo huo wa OIC si tu haukuhitimisha mgogoro wa Syria, lakini ulikuwa sababu pia ya kushadidi na kuwa tata zaidi mgogoro huo. Msimamo huo ndicho kitu kilichokuwa kikitakiwa na maadui wa nchi za Kiislamu kwa ajili ya kufanikisha malengo yao katika eneo la Mashariki ya Kati na kushadidisha hitilafu ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu. Kwani mara tu baada ya kumalizika kikao cha OIC, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alitangaza katika mkutano na waandishi wa habari kuwa Washington inakaribisha hatua ya kusimamishwa uanachama wa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki kwa leo umemalizika, hivyo sina budi kuishia hapa nikitumai kuwa mumenufaika na yale miliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Katika sehemu ya 65 ya mfululizo huu tutakuja kuzungumzia matukio ya Yemen na Bahrain na taathira zake katika kuleta utengano na mpasuko kati ya nchi za Kiislamu. Basi hadi wiki ijayo, katika siku na saa kama ya leo nakuageni nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags

Maoni