Sep 09, 2018 11:20 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (65)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 65.

Katika vipindi kadhaa vilivyopita tulitupia jicho matukio na mabadiliko ya kisiasa ya kimapinduzi yaliyojulikana kama Mwamko wa Kiislamu, yaliyojiri katika nchi za Tunisia, Misri, Libya na Syria na tukaeleza kuhusiana na mgogoro wa Libya kwamba majeshi ya madola ajinabi yalikuwa na nafasi kubwa na ya wazi zaidi katika matukio ya nchi hiyo ya Kiislamu; na kwamba uingiliaji huo ulifikia upeo wake wa juu kabisa katika mgogoro wa Syria. Tukautathmini pia msimamo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuhusiana na matukio hayo na tukafikia hitimisho kwamba kwa masikitiko, jumuiya hiyo, ambayo ilikuwa na uwezo wa kuingilia kati katika kadhia hizo kwa sura ya kiinsafu na uadilifu kamili na kwa kutegemea nguvu na uwezo wa nchi wanachama, haijaweza kuchukua nafasi inayostahiki na kutoa mchango chanya katika uwanja huo; lakini hata katika baadhi ya kesi imechukua misimamo isiyo ya busara na hivyo kushadidisha hasama, chuki na uadui uliopo. Mfano wa wazi kabisa wa hatua hiyo ni kusimamishwa uanachama wa Syria katika OIC kupitia kikao cha dharura cha viongozi wa nchi wanachama kilichofanyika mjini Makka kwa ombi la Saudi Arabia. Katika kipindi chetu cha leo tutaendelea kuzungumzia matukio ya Yemen na jinsi mgogoro wa nchi hiyo ulivyochangia kuleta umoja na mshikamano au mpasuko na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Matukio ya kisiasa ya Yemen, kuanzia wakati Yemen mbili zilipoungana mwaka 1990 hadi sasa yanaweza kugawanywa katika awamu au vipindi vitatu. Kipindi cha kwanza ni cha utawala wa Ali Abdullah Saleh; kipindi cha pili ni cha mpito cha utawala wa Abd Rabbuh Mansour Hadi; na kipindi cha tatu ni cha utawala wa harakati ya Wahouthi ya Ansarullah. Baada ya Yemen mbili kuungana, harakati zote za kidini na wanaharakati wa kisiasa pamoja na asasi za kijamii, ambazo zilifanya jitihada na kuendesha harakati za mapambano kwa muda wa miaka mingi kwa matumaini ya kuleta mageuzi na marekebisho katika muundo wa utawala, zilijenga matumaini kwa ahadi nzuri zilizotolewa na mtawala dikteta wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh za kutatua migogoro ya kisiasa na kiuchumi na vilevile kutoa uhuru uliodhaminiwa ndani ya katiba ya nchi hiyo. Matumaini ya jumuiya, asasi na wanaharakati hao yalikuwa ni kwamba, matakwa yao ya kisiasa, kiuchumi na kijamii waliyoyatarajia kuyapata ndani ya jamii ya Yemen yatathibiti; lakini baada ya muda kupita, udhaifu wa serikali wa kushindwa kutatua migogoro ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ulidhihirika. Kiwango kikubwa cha watu wasio na ajira miongoni mwa tabaka la vijana katika jamii, mivutano, migogoro kadha wa kadha ya ndani, malalamiko na manung’uniko ya mara kwa mara ya wananchi na kushindwa serikali kutatua matatizo hayo yaliielekeza hatua kwa hatua Yemen kwenye utayarifu wa kushuhudia mageuzi makubwa na ya kina ya kisiasa.

 

Moja ya hatua ghalati na isiyo sahihi aliyoichukua Ali Abdullah Saleh na ambayo iliongeza kasi ya wimbi la malalamiko ya wananchi ilikuwa ni kumwandalia mazingira mwanawe ya kumfanya mrithi wa utawala wake. Kwa kumuiga Hosni Mubarak, ambaye alikuwa amemtayarishia mazingira mwanawe Jamal ya kukalia kiti cha utawala baada yake, Ali Abdullha Saleh, naye pia alikuwa akijiandaa kumfanya mwanawe Ahmad Ali Saleh rais wa Yemen baada yake; na ili kufanikisha lengo hilo aligawa nyadhifa kadhaa muhimu na zenye ushawishi wa kisiasa, hususan jeshini na kwenye vikosi vya usalama, kwa ndugu na jamaa zake.

Hatua hiyo na nyinginezo zilizochochea malalamiko ziliungana pamoja, ili baada ya kuwasha cheche ya mageuzi makubwa nchini Tunisia yaliyosambaa hadi Misri na hatimaye katika nchi nyingine za Kiarabu za Mashariki ya Kati, kuiingiza Yemen pia kwenye mkondo wa vurugu na machafuko.

Baada ya kuenea nchi nzima wimbi la maandamano ya upinzani na manung’uniko ya wananchi, dikteta Ali Abdullah Saleh alibadilisha msimamo wake wa kutaka kuubadilisha utawala wake wa miaka 32 kuwa urais wa milele na kurithishana kiukoo. Aidha aliahidi kutoa uhuru zaidi kwa wananchi, kuamiliana vizuri na Wahouthi na kuboresha hali ya uchumi. Lakini wakati mipango yake hiyo ilipokabiliwa na changamoto ya harakati ya Al-Ijtimaul-Mushtarak, vuguvugu lililofanikiwa kuviunganisha na kuvihamasisha vyama muhimu na vyenye sauti katika jamii kwa lengo la kuzipapatua hatamu za madaraka kutoka mikononi mwa Ali Abdullah Saleh, na kuzuia jaribio la kuugeuza urais wa nchi hiyo kuwa wa urithi, serikali ya Saleh iliamua kutumia mabavu na mkono wa chuma kuwakandamiza wapinzani, hatua ambayo ilichochea na kuharakisha zaidi mazingira ya kupinduliwa utawala huo.

 

Hatua za ukatili na ukandamizaji zilizochukuliwa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji ziliwafanya wananchi hao pamoja na vyama vilivyounda vuguvugu la Al-Ijtimaul-Mushtarak viwe na azma thabiti zaidi ya kuuangusha utawala wa Ali Abdullah Saleh. Aidha mpasuko mkubwa uliojitokeza miongoni mwa waungaji mkono wa Saleh, kama kujiuzulu viongozi wengi wa jeshi, sambamba na uungaji mkono wa makabila mengi kwa wapinzani hususan baada ya mauaji makubwa ya umwagaji damu yaliyofanywa tarehe 18 Machi, yote hayo yalidhihirisha na kuweka wazi zaidi udhaifu na kuzidi kulegalega mihimili ya serikali ya dikteta huyo. Baada kuwakandamiza waandamanaji katika tukio la Machi 18, mgogoro wa Yemen ulionyesha wazi kuwa umeshachukua sura ya nje na ya kimataifa. Kwa hivyo wakati Ali Abdullah Saleh alipojeruhiwa kwenye mripuko uliotokea ndani ya msikiti wa An-Nahdayn karibu na Ikulu yake, alisafirishwa kupelekwa Saudi Arabia kwa ajili ya matibabu. Sambamba na hayo, utawala wa Aal Saud, ambao ulikuwa na hofu ya wimbi la mapinduzi ya Yemen kusambaa hadi ndani ya nchi hiyo, ulipendekeza kile kilichojulikana kama Mpango wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P) GCC na kumshawishi Ali Abdullah Saleh aukubali mpango huo. Kwa hivyo kwa mujibu wa mpango uliopendekezwa na (P) GCC kwa ushirikiano na Marekani, kupitia uchaguzi wa kimaonyesho na wa mgombea mmoja tu wa urais, Abd Rabbuh Mansour Hadi, makamu wa Abdullah Saleh, alichaguliwa kuwa rais ili kudhibiti mabadiliko ya kimapinduzi nchini Yemen na kukidhi matakwa ya wananchi. Hata hivyo katika kipindi cha utawala wa Mansour Hadi, na kutokana na serikali yake kutojali matakwa ya wananchi, kwa mara nyingine, Yemen iligeuka uwanja wa makabiliano kati ya makundi na mirengo tofauti ya kisiasa na mashindano na mivutano baina ya wadau wa ndani na madola ajinabi ya nje ya nchi hiyo.

Msikilizaji mpenzi, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika, hivyo sina budi kukomea hapa, lakini nikiwa na matumaini kwamba utajiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo katika sehemu ya 66 ya kipindi hiki. Basi hadi wakati huo nakuaga, huku nikikutakia heri na fanaka maishani.

Tags

Maoni