Sep 10, 2018 04:12 UTC
  • Jumatatu tarehe 10 Septemba 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 29 Mfunguo Tatu Dhilhija 1439 Hijria sawa na Septemba 10, 2018.

Tarehe 10 Septemba mwaka 1990 Samuel Kanyon Doe aliyekuwa rais wa jamhuri ya Liberia aliuawa na kundi la waasi. Doe alishika madaraka ya nchi mwaka 1980 akiwa sajenti mwenye umri wa miaka 29 tu baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akitumia umaskini, kupanda kwa gharama za maisha na hali mbaya ya wananchi. Hata hivyo utawala wa kidikteta wa Samuel Doe haukufanikiwa kupunguza machungu na mashaka ya Waliberia bali kinyume chake alipanua zaidi hitilafu za kikabila na kuzidisha matatizo ya kiuchumi na kijamii. Vilevile alitayarisha uwanja wa kuporwa zaidi utajiri wa madili ya almasi ya nchi hiyo kupitia njia ya kupanua zaidi uhusiano wa Liberia na Marekani na utawala haramu wa Israel. Mauaji ya Samuel Doe yalifuatiwa na vita vya ndani nchini Liberia ambavyo viliendelea kwa kipindi cha miaka 15 na kusababisah fivo vya watu karibu laki mbili na nusu.  

Samuel Kanyon Doe

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita yaani tarehe 19 Shahrivar aliaga dunia Sayyid Mahmoud Talaqani kiongozi wa kidini, mwanaharakati, mwanamapambano na mfasiri wa Qur'ani Tukufu wa Iran. Ayatullah Talaqani alikuwa akifuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa ya Iran tangu akiwa kijana. Kipindi fulani alitiwa nguvuni na kufungwa jela miaka miwili na utawala wa Kitaghuti wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini kwa kosa la kushiriki katika harakati ya wananchi ya tarehe 15 Khordad. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Imam wa Swala ya Ijumaa ya Tehran.

Ayatullah Talaqani

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulitokea katika eneo la Orleansville kusini magharibi mwa Algeria. Janga hilo la mtetemeko wa ardhi liliharibu kabisa mji mmoja uliokuwa na wakazi 30,000 na watu 10,000 wakapoteza maisha yao. Fauka ya hayo, makumi ya maelfu ya wananchi wa kusini magharibi mwa Algeria walibaki bila ya makazi. Mtetemeko huo pia ulitoa pigo kubwa kwa miundombinu ya uchumi wa nchi hiyo.

Mtetemeko mkubwa wa Orleansville kusini magharibi mwa Algeria.

Na miaka 104 iliyopita yaani tarehe 10 Septemba mwaka 1914 kulitokea vita baina ya majeshi ya Ujerumani na Russia kando kando ya ziwa la Mazury. Vita hivyo vilianza kufuatia kuzuka Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kujiunga Russia na kambi ya nchi Waitifaki. Katika vita hivyo vya Mazury, Wajerumani wakiongozwa na kamanda Paul Von Hindenburg walipata ushindi na kuwauwa takribani wanajeshi 20,000 wa Russia na kuwateka nyara wengine 45,000. Hatimaye mwaka 1917 baada ya kutokea mapinduzi nchini Russia, nchi hiyo ilijiondoa katika VitaVikuu vya Kwanza vya Dunia.

Paul Von Hindenburg

 

Tags

Maoni