Sep 11, 2018 04:15 UTC
  • Jumanne 11 Septemba 2018

Leo ni Jumanne tarehe Mosi Muharram 1440 Hijria sawa na Septemba 2018.

Tarehe Mosi Muharram inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Hijria Qamaria. Mwaka wa Hijria Qamaria unahesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa mwezi na katika nchi nyingi za Kiislamu unatumiwa kwa ajili ya masuala ya kidini au hata kijamii. Mwaka wa Hijria Qamaria pia unatumika katika masuala mengi ya kiibada kama vile kuainisha mwanzo wa funga ya mwezi wa Ramadhani, Hija, kuainisha miezi mitakatifu na kwa ajili ya historia ya matukio mbalimbali. Baadhi ya maulamaa wanasema mwaka wa Hijria ulianzishwa katika zama za utawala wa khalifa Umar bin Khattab kutokana na ushauri uliotolewa na Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) ambaye aliagiza mwanzo wa hijra ya Mtume kutoka Makka na kwenda Madina uwe mwanzo wa mwaka wa Kiislamu.  

Siku kama ya leo miaka 1433 iliyopita yaani tarehe Mosi Muharram mwaka wa 7 tangu Mtume (saw) abaathiwe na kupewa utume kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria wa Kiislamu, Makuraishi walifunga mkataba wa kuweka mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Mtume Muhammad (saw) na masahaba zake. Viongozi wa makafiri wa Makka ambao walikuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na kasi ya kustawi Uislamu na vilevile kutokana na kufeli njama zao za kuzuia kuenea dini hiyo, waliamua kuweka mzingiro wa kiuchumi ili kufanikisha malengo yao. Kwa msingi huo waliamua kuweka mkataba dhidi ya Waislamu. Mkataba huo uliwakataza watu wote kufanya muamala wa aina yoyote na wafuasi wa dini ya Uislamu. Mtume Muhammad (saw) na masahaba zake walizingirwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika bonde lililojulikana kwa jina la Shiibi Abi Twalib wakisumbuliwa na matatizo mengi na mashinikizo ya kiuchumi na katika kipindi hicho Mtume (saw) alipoteza wasaidizi wake wawili muhimu yaani ami yake, Abu Twalib na mkewe kipenzi, Bibi Khadija. Waislamu hao walisimama imara kulinda imani yao na hawakutetereka hata kidogo licha ya matatizo makubwa waliyokabiliana nayo. Mzingiro huo wa kiuchumi dhidi ya Waislamu ulikomeshwa mwezi Rajab mwaka wa kumi baada ya kubaathiwa Mtume.

Sura ya sasa ya Shiibi Abi Twalib, Makka.

Miaka 70 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Muhammad Ali Jinnah, mwasisi wa Pakistan. Jinnah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Jinnah alikuwa miongoni mwa shakhsiya walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906. Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kitamaduni na kidini, lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu wa India.

Muhammad Ali Jinnah

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Jenerali Agustino Pinoche kamanda wa wakati huo wa vikosi vya majini vya Chile aliipindua serikali halali ya Salvador Alande katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na Marekani. Alande ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kisoshalisti cha Chile, alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1970 na kuanza mara moja kutekeleza mpango wa kutaifisha mabenki, sekta ya madini na viwanda, suala ambalo lilikomesha maslahi haramu ya makampuni makubwa ya Kimarekani nchini Chile. Alande pia alikabiliana na ushawishi wa Washington nchini humo na kuifanya Marekani ianzishe vitimbi vya aina mbalimbali dhidi ya kiongozi huyo.

Jenerali Agustino Pinoche

Miaka 17 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 11 Septemba mwaka 2001, ndege mbili kati ya nne za abiria za Marekani zilizotekwa nyara ziligonga minara miwili pacha ya jengo la Biashara la Kimataifa la mjini New York huku ndege moja ikigonga jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington. Ndege ya nne ililengwa ikiwa katika anga ya Pensylvania na kuanguka. Baadhi ya ghorofa za jengo la Biashara ya Kimataifa ziliporomoka na sehemu ya jengo la Pentagon pia ikaharibiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. Karibu watu 3200 waliuawa katika mashambulizi hayo. Marekani ilitangaza kuwa mtandao wa al Qaida uliokuwa ukiongozwa na Usama bin Laden raia wa Saudi Arabia, ndio uliohusika na mashambulizi hayo. Baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani, kulianza wimbi la ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu ya dini yao katika nchi za Magharibi.

Mashambulizi ya Septemba 2001 Marekani. 

 

Maoni